Mambo yaliyompata Pinokyo

(Elekezwa kutoka Pinokyo)

Mambo yaliyompata Pinokyo: habari za mwanasesere (kwa Kiitalia jina linalotamkwa hivyo linaandikwa Pinocchio) ni hadithi ya karagosi hai ya ubao na shani zake. Hadithi hiyo ilitungwa na mwandishi Mwitalia Carlo Collodi tangu mwaka 1881 hadi 1883 ilipotolewa kama kitabu, kwa jina la Kiitalia "Le avventure di Pinocchio: Storia di un burattino".

Pinokyo (Pinocchio) alivyochorwa na Enrico Mazzanti kwa toleo la kwanza la "Le avventure di Pinocchio: Storia di un burattino"

Simulizi la Pinokyo

hariri

Siku moja seremala Maestro Ciliegia anakuta kipande cha ubao kinachoanza kusema akitaka kukikata. Kwa kuogopa anampa rafiki yake Geppetto (jina linasomeka Jepeto) aliye mchongaji. Geppetto anatumia ubao huo kuchonga karagosi anayeendelea kusema na mara baada ya kukamilika anatoroka. Akirudi nyumbani kwa njaa anaahidi kuwa mtoto mzuri na mtiifu lakini baada ya muda anatoroka tena. Anapatwa na shani nyingi hadi kukutana na baba yake Geppetto ndani ya tumbo la nyangumi. Pamoja wanajiokoa na Pinokyo anaahidi tena kuwa mtoto mzuri na safari hii anaacha utundu wake. Baada ya kutenda mema, anaamka siku moja anajikuta amebadilika umbo lake na sasa yu mvulana mwenye mwili wa kibinadamu.

Pua la Pinokyo lina tabia ya pekee; kila anaposema uwongo pua lake linakua kuwa ndefu zaidi. Kwa hiyo hawezi kuficha uwongo, na tbia hiyo ya pua inamsaidia kuachana na uwongo.

Kutokea kwa simulizi

hariri

Collodi alianza kutoa habari za Pinokyo kama simulizi mfululizo katika gazeti la kila wiki kwa ajili ya watoto. Hadithi ilipendwa sana na wasomaji ikamhamasisha mhariri kumwambia Collodi aiendeleze na hatimaye ikawa kitabu. Labda awali "Pinokyo" haikulenga watoto, na mwishowe Pinokyo alikufa vibaya wa kunyongwa kwa makosa yake mengi.

Lakini mhariri alimwomba kuendeleza simulizi na kuipeleka kwenye mwisho mwema kama kitabu kwa watoto. Hivyo masimulizi yaliyowahi kutolewa katika gazeti yalikuwa sehemu ya kwanza ya kitabu na Collodi aliendelea kuongeza shani mpya za Pinokyo anapokutana na roho jike mwema mwenye nywele za buluu anayemwokoa mara kadhaa katika matatizo yake.

Kitabu kilichapishwa pamoja na katuni za Enrico Mazzanti mwaka 1883.

Yafuatayo

hariri

Tangu 1892 kitabu kilitafsiriwa kwa lugha nyingi; kwanza kwa Kiingereza, baadaye pia kwa lugha zote za Ulaya na baadaye hata nje ya Ulaya.

Hadithi ilitafsiriwa na kutolewa kwa Kiswahili mwaka 1956 na Tanganyika Mission Press mjini Tabora.

Nje na tafsiri katika lugha zaidi ya 240, kuna pia tamthilia, opera na angalau filamu 14 juu ya Pinokyo.

Tabia muhimu ya Pinokyo katika hadithi ni pua lake linaloanza kuwa ndefu sana kila akisema uwongo. Kutokana na hilo wachoraji wa katuni za kisiasa hupenda kumchora mtu kwa pua ndefu wakitaka kuonyesha huyu ni mwongo.

Tazama pia

hariri

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  Makala hii kuhusu mambo ya fasihi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mambo yaliyompata Pinokyo kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.