Roma (maana)
Roma (pia: Rumi) ni jina linalotumika kwa mji wa Roma (mji mkuu wa Italia), ama kwa dola la Roma lililokuwa kwa karne kadhaa kabla na baada ya Kristo dola kubwa kuliko zote duniani, tena kwa Kanisa la Roma ambalo ni kiini cha Kanisa Katoliki lote. Lilikuwa pia jina la mungu wa kike katika dini ya Roma ya Kale.
Roma au Rumi?
haririRoma ni umbo asili la jina katika Kilatini na Kiitalia; limekuwa pia la kawaida katika Kiswahili cha kisasa.
Kumbe "Rumi" ilikuwa kawaida katika Kiswahili cha zamani kutokana na kawaida ya lugha ya Kiarabu (الرُّومُ ar-Rūm).
Matoleo ya Biblia ya "Union Version" iliyochapishwa tangu 1952 hutumia "Rumi", "Warumi". Kumbe tafsiri ya Biblia ya "Kiswahili cha Kisasa" hutumia "Roma", "Waroma".
- Mji wa Roma, jina la mji mkuu wa nchi ya Italia
- Dola la Roma, dola kubwa katika eneo lote kandokando ya Mediteraneo (Ulaya ya Kusini na magharibi, Asia ya Magharibi, Afrika ya Kaskazini) mnamo miaka 2400-1600 iliyopita. Liliendelea katika Dola ya Roma ya Mashariki au Bizanti hadi mwaka 1453 B.K..
- Miji mingine inayoitwa kwa jina la "Roma" iko Australia, Ecuador na Marekani; pia ni jina la eneo ndani ya mji wa Mexiko.
- Jina la mji limetumika pia kwa meli ya kijeshi ya Italia; filamu mbalimbali n.k.
- Kanisa la Roma ni jina la jimbo ambalo majimbo yote ya Kanisa Katoliki yanalitegemea ili kudumisha umoja wa imani na upendo duniani kote. Kwa sababu hiyo jina hilo linatumika pia kumaanisha Kanisa Katoliki lote. Kwa mfano, mtu akisema, "Mimi nasali Roma", anamaanisha kuwa ni muumini wa Kanisa hilo.
Historia
hariri21 Aprili 753 KK ndiyo tarehe ya kimapokeo ambayo mji huo ulisemekana kuundwa na mapacha Romulo na Remo. Ukweli ni kwamba ulianzishwa mapema zaidi (1000 K.K. hivi).