Unyago ni mchakato wa kuingiza mtu katika hatua mpya ya maisha yake ndani ya jamii kwa jumla au jamii maalumu. Bila kupitia unyago mtu anatazamwa kama hayuko tayari kupokea majukumu mapya.

Unyago kwenye mto Sepik, Papua New Guinea, 1975.

Mara nyingi mchakato huo unategemea dini au utamaduni fulani, lakini unapatikana kwa namna moja au nyingine katika makundi yote ya binadamu, kutokana na mang'amuzi kwamba mtu hawezi kufanya ghafla mambo mapya kabisa kwake bila kupata msaada wowote.

Anthropolojia inaonyesha kwamba unyago ulikuwepo tayari katika historia ya awali.

Umuhimu wa pekee ulitiwa katika mtoto kuelekea majukumu ya utu uzima kama mume au mke, baba au mama, kupitia ubalehe.

Sehemu nyingi unyago uliendana na tohara (kwa wanaume) au hata ukeketaji (kwa wanawake).

Pamoja na maumivu yaliyoendana na upasuaji wa aina hizo, mara nyingi mhusika alitakiwa kupitia majaribu mbalimbali na kushinda ili kuonyesha amekomaa.

Pengine wakati wote wa unyago huwa wamefichama ndani ya nyumba au porini, au wamejipaka rangi ili wasitambulike, kama si kujifunika uso kwa ushungi, kinyago n.k.

Hatimaye hali yao mpya inasisitizwa kwa kupewa majina mapya.

Kwa kawaida wahusika wanaunda kundi moja chini ya kiongozi wa nje (k.mf. mzee au mlezi) mwenye jukumu la kuwashirikisha ujuzi na utamaduni wa jamii husika, kama vile methali, nyimbo, taratibu n.k.

Kufifia kwa desturi hizo katika makabila mengi ya Afrika kumeacha pengo kubwa katika malezi ya vijana, hasa upande wa jinsia na maadili.

Ndiyo sababu wengine wanapendekeza unyago mbadala unaoendana zaidi na sayansi na dini. Wanaona mara nyingi mafundisho yanayotolewa katika shule za ngazi mbalimbali hayatoshi au hayaridhishi.

Marejeo hariri