Tohara (kutoka Kiarabu: طهارة tahara - safi, tahiri) ni upasuaji mdogo wa kukata na kuondoa govi, yaani ngozi inayofunika ncha ya uume.

Tohara inavyofanyika.
Ndivyo ilivyo kabla na baada ya tohara
Uenezi wa tohara duniani.

Wakati mwingine ukeketaji huitwa "tohara ya mwanamke", lakini matumizi hayo si sahihi, kwa sababu ni aina tofauti za upasuaji, ingawa zote mbili zinahusu viungo vya uzazi.

Tohara inaweza kufanyika katika umri wowote na kwa sababu za kiutamaduni, za kidini au za kiganga. Mara nyingi desturi za kutahiri zinachanganya sababu za kidini na za kiutamaduni. Kwa mfano, Waislamu wa Misri huamini ya kwamba wanatahiri watoto wao kama amri ya kidini lakini Wakristo Wakopti wa nchi hiyo hutahiri watoto vilevile. Ukweli ni kwamba tohara ilikuwa desturi ya Wamisri tangu kale.

Tohara inafanyika hasa mara baada ya kuzaliwa kwa mtoto au wakati wa kubalehe.

Kufuatana na Shirika la Afya Duniani takriban 30% za wanaume wote duniani wametahiriwa, wengi wao wakiwa Waislamu.

Tohara ya kiutamaduni hariri

Katika makabila mengi ya Afrika mvulana anatahiriwa ili kuingizwa katika kundi la wanaume wanaopaswa kuwajibika katika jamii.

Desturi hiyohiyo inaonekana pia kati ya watu wa Pasifiki k.mf. Wapolinesia wa Samoa, Tonga na Niue, vilevile kati ya Wamelanesia wa Fiji na Vanuatu. Wakazi asilia wa Australia huwa pia na tohara ya wavulana.

Tohara na dini hariri

Uyahudi hariri

Kwa Wayahudi tohara ni ishara ya agano lao na Mungu na inapaswa kufanyika siku ya nane baada ya mtoto wa kiume kuzaliwa ili kumwingiza mapema katika taifa la Mungu.

Kufuatana na habari za Biblia (Mwanzo 17), Ibrahimu alikuwa mtu wa kwanza kupokea amri ya kutahiriwa kama alama ya agano.

Ukristo hariri

Yesu mwenyewe alitahiriwa siku ya nane kama Wayahudi wote wa kiume. Tohara ya Yesu inakumbukwa kwa sikukuu maalumu katika makanisa mengi duniani hasa Waorthodoksi, pia kwa sababu ilikuwa ndiyo siku ya kupewa rasmi jina lake hilo.

Agano Jipya linaonyesha jinsi gani suala la tohara lilikuwa motomoto mwanzoni mwa Kanisa, wakati Wakristo wengi walitoka katika Uyahudi.

Kufuatana na kitabu cha Matendo ya Mitume (15:23-29) Mtaguso wa Mitume uliofanyika Yerusalemu uliamua Wakristo kutoka mataifa wasilazimishwe kutahiriwa.

Hasa Mtume Paulo alisisitiza kwamba jambo hilo si muhimu tena, cha maana ni kuwa watu wapya kwa imani.

"Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya" (Waraka kwa Wagalatia 6:15).

"Maana sisi tu tohara, tumwabuduo Mungu kwa Roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala hatuutumainii mwili" (Waraka kwa Wafilipi 3:3).

Hata hivyo Wakopti wa Misri na Ethiopia wameendelea kutahiri watoto wao.

Uislamu hariri

Katika Uislamu tohara hufundishwa kama wajibu wa kidini kwa kila mwanamume.

Hakuna amri katika Kurani kuhusu tohara lakini inatazamwa kama sunna ya mtume Muhamad. Kwa imani hiyo ni ishara ya mitume ya kwamba walizaliwa bila govi katika hali ya kutahiriwa tayari.

Utekelezaji wa tohara huwa tofauti kati ya nchi na nchi; mara nyingi mtoto hutahiriwa akiwa na umri wa miaka 5 hadi 10. Katika mazingira ya mjini wazazi wanawahi kumtahiri mapema.

Tohara kama hatua ya kiafya hariri

 
Mbadala wa tohara.

Siku hizi hata mataifa yasiyokuwa na desturi hiyo yanaanza kuijali kwa sababu za usafi na afya.

Ni kwamba tohara inapunguza hatari ya mtoto kupatwa na fimosis.

Imethibitishwa kuwa inapunguza uwezekano wa kuambukizwa ukimwi pamoja na hatari ya magonjwa mengine kama kansa ya uume.

Katika nchi kadhaa sehemu kubwa ya watoto wa kiume wanatahiriwa mara baada ya kuzaliwa kwa sababu hizo za kiganga. Kwa mfano, huko Marekani asilimia 56 za wavulana waliozaliwa mwaka 2005 walitahiriwa katika hospitali walikozaliwa. Hata hivyo katika nchi hiyo kuna kampeni dhidi ya tohara kutokana na hoja ya kwamba mara nyingine upasuaji hauendi vizuri na kusababisha madhara ya kudumu kwa viungo vya uzazi.

Viungo vya nje hariri