Usafiri nchini Tanzania

(Elekezwa kutoka Usafiri wa Tanzania)

Usafiri nchini Tanzania ni hasa kwa njia ya barabara. Nyingine ni reli na ndege. Kwenye maziwa makubwa na pwani ya Bahari Hindi kuna pia usafiri wa meli.

Ramani ya Usafiri wa Tanzania ionyeshayo
Buluu: njia za reli; Nyekundu iliyokolea: barabara za lami

Barabara

hariri
 
Mfano wa barabara ya lami Tanzania.

Jumla kuna takriban kilomita 88,200 za barabara nchini Tanzania. Barabara za lami ni kilomita 3,704 pekee, nyingine 84,496 ni za udongo zinazokumbwa na matatizo ya mara kwa mara.

 
Kusukuma basi wakati wa mvua kwenye barabara ya kwenda Mbamba Bay (2012).

Barabara za lami

hariri

Kuna hasa barabara ya TANZAM kutoka Zambia kupitia Mbeya inapokutana na barabara kutoka Malawi halafu kupitia Iringa na Morogoro hadi Dar es Salaam. Mkono mmoja wa barabara hii imefikia Songea kutoka Makambako.

Barabara nyingine muhimu inaanza Chalinze takriban kilomita 90 kutoka Dar es Salaam na kufikia Tanga, Moshi na Arusha inapoendelea hadi Kenya.

Kutoka Morogoro kuna njia nyingine ya lami hadi Dodoma.

Kuna jitihada ya miaka mingi kukamilisha barabara ya pwani kati ya Dar es Salaam na Lindi / Mtwara lakini imeendelea polepole mno kuna sehemu kadhaa za lami kwa mfano karibu na Kilwa. Njia za lami kati ya Lindi, Mtwara na Masasi zinaunganishwa kwa barabara za udongo zinazoharibika mara kwa mwara wakati wa mvua.

Kwenye sekta ya barabara si nzuri, hasa kwa baadhi ya maeneo nchini Tanzania, kwa sababu kuna uhaba wa lami.

Kwa hiyo serikali inapaswa kuliona suala hili, kwa sababu linasababisha ajali kwenye sehemu ambazo magari makubwa kama mabasi na malori hupita.

Kwa kuwa njia ina matope na baadhi ya magari hupeleka nafaka sehemu fulani, hiyo huwa inasababisha uhaba wa chakula kwenye baadhi ya sehemu kama Dar es Salaam.

Shirika mbili za reli zahudumia nchi ni TRL (Shirika ya Reli Tanzania - Tanzania Railways Limited, zamani "TRC") na TAZARA (Tanzania-Zambia Railways Corporation). Kwa upande wa TRL kampuni hililinaendesha usafiri tu ilhali njia za reli zenyewe zinamilikiwa na Reli Assets Holding Company Ltd (RAHCO) kama wakala wa serikali.

Jumla ya njia za reli nchini Tanzania ni kilomita 3,690

 
Treni za TRC kituoni huko Dar es Salaam

Shirika la Reli Tanzania

hariri

Shirika ya Reli Tanzania (Tanzania Railways Limited TRL) limetawala reli ya kati kuanzia Dar es Salaam hadi Kigoma halafu reli ya kaskazini kati ya Tanga na Arusha jumla kilomita 2,721. Reli hii ilijengwa wakati wa koloni ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Sehemu ya kwanza ya kilomita 14 ilikuwa chanzo cha reli ya kaskazini kuanzia Tanga penye bandari muhimu ya Wajerumani hadi Pongwe iliyokamilishwa tar. 16 Oktoba 1894. Reli hii iliendelea polepole ikafikia Mombo wakati wa Februari 1905 ikafikia Moshi mwaka 1912. Reli ya Kati ilianzishwa Februari 1906 ikafikia Morogoro 1907, hadi Tabora 1912 na hadi Kigoma 1914. Njia za Wajerumani ziliunganishwa kati ya Korogwe na Morogoro wakati wa ukoloni wa Uingereza. Njia ya kuunganisha reli ya kaskazini na reli ya Kenya ilifungwa mwaka 1977 wakati wa kuachana kwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki iliyokuwa na reli ya pamoja. Upana wa reli hii ni ya mita moja tu, haikubadilishwa, kwa hivyo haiwezekani kutumia mabehewa na injini moja kwa moja kwenye reli ya TAZARA.

TAZARA au Tanzania-Zambia-Railways ilijengwa na China kuanzia mwaka 1970. Shabaha yake ilikuwa kupatia nchi ya Zambia njia ya reli isiyopita katika Afrika Kusini iliyofuata siasa ya Apartheid au Msumbiji iliyokuwa koloni ya Ureno. Ujenzi uligharamiwa na China na kazi zilitekelezwa na wanfanyakazi Wachina.

TAZARA inakutana na reli za Zambia kuko New Kapiri Mposhi. TAZARA imesaidia mawasiliano katika sehemu za kusini za Tanzania kwenye urefu wa kilomita 969 nchini.

Ujenzi wa njia mpya

hariri

Mwaka 2017 njia mpya inayotumia geji sanifu ya kimataifa ilianzishwa Dar es Salaam kuelekea Morogoro. Tofauti na geji ya mita moja iliyopo hii geji sanifu itaruhusu mwendo wa treni za mkasi zaidi na pia treni nzito zaidi za kubebea mizigo. Njia hii imepangwa kuwa awamu ya kwanza ya njia ya geji sanifu itakayofika hatimaye hadi Kigoma, Mwanza na pia nchi jirani, hasa Burundi ambapo inaweza kukutana na reli mpya ya Mombasa - Bujumbura na njia hizi zote zinafuata mpango mkuu wa reli ya Afrika ya Mashariki.

Usafiri wa ndege

hariri
 
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Mwalimu Kambarage Nyerere.

Huduma kwa ndege zatumia hasa nyanja za ndege 10 penye barabara ya lami kwa ajili ya ndege hasa Julius Nyerere/Dar es Salaam, Kilimanjaro /Arusha-Moshi na Zanzibar-Kisauni. Nyanja za ndege nyingine zinazolengwa na kampuni kulingana na ratiba zao ni: Bukoba, Arusha, Kigoma, Lindi, Musoma, Mtwara, Mwanza, Pemba, Shinyanga, Tabora, Tanga.

 
Usafiri wa majini.
 
Watu wakitumia usafiri wa wanyama (Ngombe)

Usafiri wa majini

hariri

Usafiri kwa maji upo kwenye maziwa makubwa kama vile Viktoria Nyanza, ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa.

Meli ni chombo muhimu cha usafiri upande wa Bahari Hindi kati ya bara na visiwa vya Zanzibar kama Unguja na Pemba.

Meli zinazohudumia bandari za pwani ziliwahi kubeba abiria wengi kati ya Dar es Salaam, Kilwa, Lindi na Mtwara lakini tangu kuboreka kwa mawasiliano ya barabara hazipo tena. Siku hizi bandari zinahudumia usafiri wa mizigo.

Usafiri wa kutumia wanyama

hariri

Usafiri wa kutumia wanyama ni usafiri ambao kwa kawaida unatumia mkokoteni. Mara nyingi wanyama kama punda na ng'ombe ndio wanaotumika kuvuta mkokoteni watu wakiwa ndani yake au mizigo ikiwa ndani yake.

Tanbihi

hariri