Venera (kwa Kirusi: Венера) ilikuwa mradi wa Umoja wa Kisovyeti wa kutuma vipimaanga kwenda sayari Zuhura katika miaka 1961 hadi 1983. Venera ni jina la Kirusi kwa Zuhura (kwa Kiingereza Venus).

Sehemu ya Venera 7 iliyofika kwenye uso wa Zuhura.

Venera 3 ilikuwa kipimaanga cha kwanza kilichofika mwaka 1965 kwenye uso wa sayari nyingine, lakini kilianguka tu bila kutuma data duniani. Vipimaanga vilivyofuata vilipotea pia. Angahewa zito, kanieneo ndani yake na jotoridi kali vilisababisha kupotea kwa vyombo. Hatimaye wahandisi wa mradi walibuni chombo kizito kilichoweza kuvumilia kanieneo kubwa na jotoridi la juu. Kutokana na uzito wake kiliweza kubeba vifaa vichache tu[1].

Venera 7 ilitua kwenye uso wa Zuhura tarehe 15 Desemba 1970; ilishuka dakika 35 ndani ya angahewa na kutuma vipimo. Baada ya kutua usoni iliweza kutuma tena data kwa dakika 23. Vipimo hivyo vilikuwa vya kwanza vya hakika kuhusu tabia za sayari jirani na Dunia inayofunikwa na mawingu yanayozuia kuona uso wake. Data zilionyesha halijoto kwenye uso wa Zuhura ilikuwa 475 °C (± 20 °C). Kanieneo ya angahewa ilikadiriwa kuwa takriban megapaskali 9 (bar 90, yaani mara 90 kuliko kanieneo ya duniani)[2]. Venera 7 haikuwa na kamera lakini ilionekana ilitua kwenye sehemu ngumu.

Marejeo

hariri
  1. Plumbing the Atmosphere of Venus, tovuti ya Don P. Mitchell, iliangaliwa Mei 2019
  2. The Soviets and Venus, part 1, na Larry Klaes; The Electronic Journal of The Astronomical Society of the Atlantic, Volume 4, Number 7 - February 1993