Emily Ruete

Mwandishi wa Kijerumani, mprincesa wa Zanzibar aliyekimbia (1844-1924).

Emily Ruete (awali: Sayyida Salme; 30 Agosti 184429 Februari 1924)[1] alizaliwa Zanzibar kama “Salama binti Said’’, [2] alikuwa mtoto wa mwisho kati ya 36 kwenye familia ya Sayyid Said bin Sultan Al-Busaid, Sultani wa Zanzibar, Muscat na Oman.

Emily Ruete

Emily Ruete katika mavazi ya kitamaduni kama Malkia wa Zanzibar
Amezaliwa 30 Agosti 1844
Zanzibar
Amekufa 29 Februari 1924
Jena, Ujerumani
Kazi yake Malkia Sayyida Salme wa Zanzibar na Oman

Pia ni mwandishi wa kitabu kiitwacho Memoirs of an Arabian Princess from Zanzibar.

Maisha yake Zanzibar

Salama binti Said alizaliwa mnamo tarehe 30 Agosti 1844, mwana wa Sultan Said na mtumwa wake Jilfidan, suria mwenye asili ya Circassia katika Kaukazi. Aliishi katika hekalu la Bet il Mtoni lililopo umbali wa kilomita nane kutoka baharini ukanda wa kusini mwa stone Town. (Hekalu hilo lilibomoka mnamo mwaka 1914). Amekuwa akizungumza lugha mbili ambazo ni Kiarabu na Kiswahili. Mnamo mwaka 1851 alihamia Bet il Watoro, katika nyumba ya kaka yake Majid bin Said wa Zanzibar, aliyewahi kuwa Sultani. Kaka yake alimfundisha jinsi ya kuendesha gari na kulenga shabaha. Mnamo mwaka 1853 alihamia Bet il Tani pamoja na kaka yake. Alijifunza kwa siri jinsi ya kuandika, taaluma ambayo haikuruhusiwa kwa mwanamke kipindi kile.

Pindi baba yake anafariki mnamo mwaka 1856 alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili, hivyo kupewa urithi wake. Urithi huo ulijumuisha mali kama mashamba, makazi pamoja na kiasi cha Paundi 5,429. Baada ya kifo cha baba yake, kaka yake Sayyid Thuwaini bin Said al-Said alikuwa Sultani wa Muscat na Oman, wakati kaka yake Majidi alikuwa Sultani wa Zanzibar.

Mnamo mwaka 1859 mama yake alifariki na Salme akapewa mashamba kama urithi wake. Mwaka huohuo kulizuka mgogoro kati ya kaka zake Majid na Barghash bin Said wa Zanzibar. Ingawa alimpenda kaka yake Majid, dada yake Khwala alikwenda upande wa Barghash. Kwa sababu aliweza kuandika, alikuwa katibu wa kikundi cha Barghash akiwa na miaka kumi na mitano. Kwa msaada wa meli za Wamarekani Barghash alishindwa, na utawala wake kuangushwa. Barghash alipelekwa utumwani Bombay kwa miaka miwili ma Salme alikimbilia Kisimbani kwenye moja ya makazi yake.

Hatimaye Salme akarudi Stone Town na kujiunga na Majid. Hii ilimtengenezea chuki ya kaka yake Barghash na dada yake Khwala .

 
Emily akiwa na mumewe pamoja na watoto wao wawili.

Mapenzi na ndoa na Rudolph Ruete

Kipindi anaishi Stone Town aliweza kufahamiana na jirani yake ambaye alikuwa mfanyabiashara wa Kijerumani, Rudolph Heinrich Ruete (10 Machi 1839 - 6 Agosti 1870) na kupata ujauzito kwake. Agosti 1866 ilionekana dhahiri kuwa Salma ana ujazito, ilibidi akimbilie kwenye manowari sindikiza ya Uingereza H.M.S. Highflyer iliyoongozwa na nahodha Thomas Malcolm Sabine Pasley R.N. na kupewa ruhusa ya kuingia kwenye moja ya makoloni ya Uingereza liitwalo Aden. Huko alipata kuwa Mkristo na kubatizwa kabla ya ndoa yake iliyofanyika tarehe 30 Mei 1867. Salma aljifungua mtoto wa kiume, Heinrich, huko Aden Desemba 1866 na kufariki pindi akiwa katika safari ya kutokea Ufaransa kwenda Ujerumani katika majira ya joto mwaka 1867. Wawili hao walihamia Hamburg Ujerumani.[3]

Maisha yake Ulaya

Familia ya Ruete iliishi Hamburg. Rudolph Ruete alifariki mnamo mwaka 1870 mjini Hamburg kwa ajali ya barabarani, na kumwacha Emiliy Ruete katika mazingira magumu ya kiuchumi baada ya mamlaka husika kukataa kumpatia urithi wake. Katika kupunguza matatizo hayo ya kiuchumi aliandika kitabu kinachoitwa Memoirs of an Arabian Princess from Zanzibar, kilichochapishwa kwa mara ya kwanza nchini Ujerumani mnamo mwaka 1886, na baadaye kuchapishwa Marekani na Ireland. Kitabu hicho kilitoa historia ya mwanamke wa Kiarabu kwa mara ya kwanza na kumpa msomaji picha ya maisha ya Zanzibar kati ya mwaka 1850 hadi 1865, pamoja na picha ya ndugu zake Majid bin Said wa Zanzibar na Barghash bin Said wa Zanzibar, Masultani wa kipindi kile Zanzibar.

Kabla ya kifo cha Rudolph, walipata mtoto wa kiume na wa kike wawili. Watoto hao waliitwa:

  • Antonia Thawke Ruete (24 Machi 1868 – ?), aliyeolewa na Eugene Brandeis (1846–1919) mwaka 1898 na kupata watoto wa kike wawili.
  • Rudolph-Said Ruete (13 Aprili 1869 – 1 Mei 1946). Baada ya kipindi katika jeshi la Ujerumani alijiunga na utumishi wa ubalozi wa Ujerumani huko Beirut akaendelea kuwa mkurugenzi wa benki ya Kijerumani huko Kairo. Alijipatia pia jina kama mwandishi. Mwaka 1934, baada ya Hitler na chama cha Nazi kushika utawala, Rudolph-Said aliyewahi kuoa mke kutoka familia ya Kiyahudi, aliondoka Ujerumani akahamia Uingereza na kuchukua uraia wa huko[4]. Baada ya Vita ya Pili ya Dunia aliishi huko Luzern, Uswisi. Mnamo mwaka 1901, alimuoa Mary Therese Matthias (1872 – ?) na kupata mtoto mmoja wa kiume na mwingine wa kike, Werner Heinrich (1902-1962) na Salme Matilda Benvenuta Olga (1910 – ?). Kupitia ndoa hiyo, akawa binamu wa Alfred Moritz, Baron Melchett wa kwanza, aliyekuwa mwenyekiti wa kwanza wa Imperial Chemical Industries.

Baada ya kifo cha mume wake, Emily Ruete alishikiliwa kutokana na mipango ya kikoloni iliyofanya na Otto von Bismarck. Kulikuwa na tetesi kuwa Bismarck alitaka kumfanya mwanaye wa kiume kuwa moja ya ultani wa Zanzibar. Emily alirudi Zanzibar mwaka 1885 na 1886, kitabu chake cha kumbukumbu kiitwacho, Memoirs of an Arabian Princess kilichapishwa nchini Ujerumani. [3] Kati ya miaka 1889 na 1914, aliishi Beirut, Lebanon na Jaffa. Alifariki katika mji wa Jena huko Ujerumani, akiwa na umri wa miaka 79 kwa ugonjwa wa nimonia.

Mnamo mwaka 1992, kitabu cha An Arabian Princess Between Two Worlds kilichapishwa, huku akituma barua nyumbani kwao akiwaelezea maisha aliyoishi huko Ulaya, mwisho habari zake zilienea kwa umma wote.

Kuna maonyesho mbalimbali kuhusu Emily Ruete katika Jumba la makumbusho, Zanzibar iliyopo Stonetown, jumba lililojengwa na kaka yake Sultan Barghash.

Tetesi

Emily Ruete ameonekana kama mhusika mdogo kwenye riwaya ya M.M. Kaye iitwayo Trade Wind. Kitabu hicho kilianzishwa mwishoni mwa mwaka 1850 na kuonyesha uhusika wake na jaribio la kaka yake Barghash kukosa ufalme wa nduguye Majid, masilahi pamoja na ndoa yake na Rudolph.

Tanbihi

  1. https://books.google.com/books/about/An_Arabian_Princess_Between_Two_Worlds.html?id=mU2w8K8IyoEC&printsec=frontcover&source=kp_read_button#v=snippet&q=Sayyida%20Salme%20bint%20ibn%20sultan%20oman%20born&f=false
  2. Sayyida ni wadhifa aliopewa mwanamke mwenye cheo kikubwa, hasa kutoka kwenye uzao wa Mtume Muhamad; Salme ni kifupi cha jina Salama
  3. 3.0 3.1 "Memoirs of an Arabian Princess: An Autobiography". World Digital Library. 1888. Iliwekwa mnamo 2013-09-19.
  4. Maxwell, Katherine: Sayyida Salme / Emily Ruete: Knowledge Flows in an Age of Steam, Print, and Empire, Global Societies Journal, 3, mwaka 2015

Marejeo

  Makala hii kuhusu mwandishi fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Emily Ruete kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.