Said bin Sultani, pia Sayyid Said, (5 Juni, 1797 - 19 Oktoba, 1856) alikuwa Sultani wa Maskat, Oman na Zanzibar.

Umuhimu wake katika historia unatokana na kwamba mwaka wa 1840 alihamisha mji mkuu wa usultani wake kutoka mji wa Maskat hadi Stone Town huko Unguja.

Alifahamika kwa kustawisha kilimo cha makarafuu na biashara ya watumwa.

Maisha

hariri

Sayyid Said alikuwa Sultani wa Omani tangu mwaka 1804. Aliimarisha utawala wa Omani juu ya pwani ya Afrika ya Mashariki.

Mwaka 1829 alifaulu kuteka Mombasa iliyokuwa mji pekee wa kujitegemea kati ya miji yote ya Uswahilini.

Visiwa vya Unguja na Pemba vilikuwa chini ya Omani tangu mwaka 1689, Wareno walipofukuzwa katika pwani za Uswahilini.

Sayyid Said aliona nafasi kubwa ya biashara ya karafuu kwa ajili ya soko la Uhindi na kwingineko. Mwaka 1829 akaanzisha mashamba ya mikarafuu kwa kutumia kazi ya watumwa kutoka bara.

Biashara hiyo ikabadilisha uso wa mji wa Zanzibar wa karne ya 19 uliowahi kuwa kijiji kikubwa tu cha vibanda kando ya boma lililojengwa na Omani kama kizuizi dhidi ya Wareno.

Baada ya azimio la mwaka 1832 la kuhamisha mji mkuu wa Omani kwenda Unguja, idadi ya wakazi wa mji ilikua haraka.

Nchi za nje zikatambua mji mkuu mpya na kujenga uhusiano. Ubalozi wa Marekani ulijengwa mwaka 1837, Uingereza ukafuata mwaka 1841 na Ufaransa mwaka 1844.

Sultani mwenyewe aliondoka kabisa Maskat mwaka 1840. Kukua kwa Zanzibar kulisababisha kukonda kwa mji wa Maskat.

Baada ya kifo cha Sayyid Sultan mwaka 1856, usultani wa Oman uligawiwa kati ya wanawe. Sayyid Majid bin Said Al-Busaid (1834/18351870) akawa Sultani wa kwanza wa Zanzibar na kaka yake Sayyid Thuwaini bin Said al-Said akawa Sultani wa Oman akitawala nchi hiyo bila maeneo ya Afrika ya Mashariki.

  Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Said bin Sultani kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.