Historia ya Namibia
Historia ya Namibia inahusu eneo la Kusini mwa Afrika ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Namibia.
Historia ya kale
haririWakazi wa kwanza huaminiwa kuwa wawindaji wa jamii ya Wasani.
Katika karne ya 14 hivi BK walianza kufika wahamiaji Wabantu wenye ujuzi wa kilimo na uhunzi walioshika utawala na hatimaye kuwa wengi kuliko wenyeji.
Chini ya ukoloni
haririNamibia katika mipaka ya sasa ilianzishwa katika karne ya 19 kama koloni la Ujerumani kwa jina la Afrika ya Kusini-Magharibi ya Kijerumani. Maeneo yake yaliunganishwa mara ya kwanza kwenye mwaka 1884.
Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ilivamiwa na Uingereza na Afrika Kusini. Pamoja na makoloni mengine ya Ujerumani iliwekwa chini ya mamlaka ya Shirikisho la Mataifa. Tangu mwaka 1919 ilikuwa eneo la kudhaminiwa kwa niaba ya Shirikisho la Mataifa chini ya serikali ya Afrika Kusini.
Afrika ya Kusini-Magharibi (kwa Kiingereza South-West Africa) ilikuwa jina la eneo hilo kuanzia mwaka 1922 hadi uhuru wa nchi ya Namibia mwaka 1990.
Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, wakati wa kuvunjwa kwa Shirikisho la Mataifa mwaka 1946, Umoja wa Mataifa ulichukua jukumu la kuratibu maeneo ya kudhaminiwa.
Afrika Kusini haikutambua badiliko hilo ikitangaza ya kwamba hali ya udhamini ilikuwa ya Afrika ya Kusini-Magharibi tangu kuvunjwa kwa Shirikisho la Mataifa.
Mwaka 1949 bunge la Afrika Kusini lilitangaza sheria ya kufanya eneo kuwa jimbo la tano la Afrika Kusini na kueneza siasa ya apartheid (ubaguzi wa rangi) hadi hukoikijaribu kulitendea eneo hilo kama sehemu kamili ya Afrika Kusini. Hii haikukubaliwa na Umoja wa Mataifa na nchi nyingi za dunia.
Baadaye mfumo wa bantustans sawa na Afrika Kusini ulianzishwa pia huko ambako maeneo makubwa yenye rutuba yalitengwa kwa ajili ya Wazungu ilhali Waafrika walitakiwa kuwa na maeneo kadhaa tu kama "homeland" walipokuwa na haki ya kukaa, lakini katika maeneo mengine waliruhusiwa kukaa kama wafanyakazi kwa muda tu. Mfumo huo haukutekelezwa kwa ukali, tofauti na Afrika Kusini yenyewe.
Hii haikukubaliwa na Umoja wa Mataifa ulioendelea kudai ya kwamba Afrika Kusini ilipaswa kuandaa eneo kwa uhuru.
Mwaka 1966 Mkutano Mkuu wa UM uliamua kuondoa mamlaka ya Afrika Kusini na kuweka eneo moja kwa moja chini ya Umoja wa Mataifa. Azimio hilO halikuweza kutekelezwa kwa sababu Afrika Kusini ilikataa.
Hapo wanamgambo wa chama cha SWAPO walichukua silaha wakajaribu kupigania uhuru.
Azimio la Mkutano Mkuu wa UM la mwaka 1968 lilibadilisha jina la eneo kuwa Namibia.
Mwaka 1971 Mahakama ya Kimataifa ya Haki ikaamua ya kwamba utawala wa Afrika Kusini si wa haki. Mwaka 1978 Umoja wa Mataifa uliamua ya kwamba Afrika ya Kusini-Magharibi unapaswa kupewa uhuru. Hapo serikali ya Afrika Kusini ikaanza kuchukua hatua za kuandaa uhuru wa eneo hili, lakini vita kati ya jeshi lake, SWAPO na wanajeshi wa Angola na Kuba iliendelea.
Baada ya miaka ya vita vya kupigania uhuru, mchakato wa kimataifa wa kuelekea uhuru ulianza na kufikia mapatano ya kumpumzisha silaha mwaka 1988. Hatimaye mwaka 1990 nchi ilipata uhuru wake kwa jina la Namibia.
Tazama pia
hariri- Afrika ya Kusini-Magharibi ya Kijerumani
- Afrika ya Kusini-Magharibi (chini ya Afrika Kusini)
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Namibia kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |