Irugwa
Irugwa ni kata ya Wilaya ya Ukerewe katika Mkoa wa Mwanza, Tanzania.
Kata hiyo inaundwa na kisiwa cha Irugwa na visiwa vingine vidogo vya Kulazu, Buluza na Lyegoba.
Irugwa inavyo vijiji viwili: Sambi (yalipo makao makuu ya kata) na Nabweko. Kitongoji maarufu ni Buyanza (wenyewe wakijiita Washabunda) maana ndipo hasa zilipo huduma muhimu za jamii kama zahanati, ofisi ya kata, shule ya msingi na mitambo ya maji safi na maji taka bila kusahau mitambo ya kuzalisha umeme.
Kata ina shule za msingi tano ambazo ni Irugwa, Nabweko, Kulazu, Buluza na Lyegoba. Kuna shule ya sekondari moja iitwayo Irugwa.
Wakazi
haririKatika sensa ya mwaka 2022 wakazi wa kata walihesabiwa kuwa 13,314 [1]. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 11,873 waishio humo.[2] Msimbo wa posta ni 33624.
Wakazi wengi ni kabila la Wakerewe wakiwa ndio wenyeji haswa wa kata hiyo; lakini pia kuna mchanganyiko wa makabila mbalimbali hasa Wajita, Wasukuma, Wakara (kutoka kisiwa cha Ukara) na watu wa jamii tofautitofauti.
Katika kata ya Irugwa kuna koo mbalimbali. Mmoja kati ya koo hizo ni ule mkubwa wa Wasilanga, na koo nyingine ni kama Wasonge na Wabhwarumi.
Uchumi
haririShughuli kubwa ya kiuchumi ni uvuvi wa dagaa na samaki wengine, hasa aina ya sangara lakini pia sato. Maeneo muhimu ya shughuli hizo ni Nabweko maeneo ya Mchangani, Nabweko shule, Bhuluza, Ngera, Kulazu na Ryegoba.
Shughuli nyingine zinazofanywa na wakazi wa Irugwa ni ufugaji wa mifugo hasa ng'ombe, mbuzi, kuku na bata; karibia kila eneo ni wafugaji, hasa ukizingatia Irugwa imezungukwa na maji kila kona.
Wakazi wa Irugwa pia ni wakulima: licha ya kuwa na eneo dogo kwa akili ya kilimo, lakini watu wamekuwa wakijishughulisha na kilimo hasa kwa ajili ya chakula. Zao kubwa ni muhogo, lakini kuna mazao mengine yanayolimwa katika kata hiyo, yaani mahindi, viazi vitamu na mpunga, japo mpunga si sana kwa sababu ya ufinyu wa eneo.
Utamaduni, hasa kabla ya mwingiliano na makabila mengine, ulikuwa kutumia ugali wa mhogo kama chakula kikubwa, hasa ugali kwa samaki ambao wanapatikana kwa urahisi katika ziwa Viktoria linalozunguka kisiwa hicho, kama vile sangara (wenyewe wanamuita echengu), sato, furu, dagaa, ngere (samaki ambao wanapatikana kwa msimu, kwa mwaka mara moja, kuanzia mwezi Julai hadi Oktoba au Novemba) lakini pia domodomo (wenyewe wanamuita embete). Kuna samaki wengine wanaoitwa Embozu, Emumi na Emote.
Marejeo
haririKata za Wilaya ya Ukerewe - Mkoa wa Mwanza - Tanzania | ||
---|---|---|
Bukanda • Bukiko • Bukindo • Bukongo • Bukungu • Bwiro • Bwisya • Igalla • Ilangala • Irugwa • Kagera • Kagunguli • Kakerege • Kakukuru • Mukituntu • Muriti • Murutunguru • Nakatunguru • Namagondo • Namilembe • Nansio • Nduruma • Ngoma • Nkilizya • Nyamanga |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Mwanza bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Irugwa kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno. |