Wikipedia

kamusi elezo huru mtandaoni
(Elekezwa kutoka Kamusi Elezo za Wiki)

Wikipedia ni kamusi elezo huru ya lugha nyingi katika mtandao wa wavuti. Inalenga kukusanya elimu nyingi iwezekanavyo na kuisambaza kwa njia ya intaneti.

WIKIPEDIA


Inatumia taratibu za wikiwiki. Ni bure kabisa, na inaweza kusomwa, kuandikwa, na kuhaririwa na mtu yeyote, popote pale. Yaani kila mtu anaweza kuchangia makala akiwa na uhuru wa kuboresha makala zilizopo kwa kuzihariri.

Kamusi hii inajengwa kwa utaratibu huria ambao unategemea falsafa ya ushirikiano ambako watu wengi hushirikiana kwa kujitolea bila kupokea malipo yoyote.

Falsafa hii inaonekana katika vuguvugu la programu huria ya tarakilishi, mikutano huria, demokrasia huria, n.k.

Wikipedia inaweza kusomwa pia nje ya mtandao kwa kutumia programu huria ya Kiwix.

Historia

Wikipedia ilianzishwa kwa Kiingereza mwezi Januari mwaka 2001.

Mwaka 2003 kamusi elezo hii ilianzishwa katika lugha ya Kiswahili.

Wikipedia imeshachukua nafasi za kamusi elezo mashuhuri kama Encyclopedia Britannica zilizotazamwa kuwa mkusanyo wa elimu ya Dunia kabla ya kutokea kwa intaneti. Kwa lugha za Kiafrika kama Kiswahili ni mara ya kwanza ya kwamba jaribio la kukusanya elimu za fani mbalimbali limeanzishwa.

Hadi mwaka 2018 wachangiaji wa Wikipedia walishirikiana kuunda zaidi ya makala milioni 47[1] kwa lugha 300.

Wikipedia kubwa zenye makala zaidi ya milioni mbili zilikuwa kwenye Novemba 2018: Wikipedia ya Kiingereza (makala 5,758,502), ya Kicebuano (makala 5,379,917), ya Kiswidi (makala 3,764,225), ya Kijerumani (2,243,097) na ya Kifaransa (makala 2,060,362). Kwa jumla kulikuwa na Wikipedia zenye zaidi ya makala milioni moja kwa lugha 15.

Taasisi ya Wikimedia Foundation

Kisheria maudhui yote ya Wikipedia si mali ya mtu yeyote kwa kuwa ni maudhui huria. Seva za wikipedia na programu zake zinatunzwa na taasisi ya Wikimedia Foundation ambayo ni shirika lisilo la kiserikali lililoandikishwa chini ya sheria za jimbo la Kalifornia, Marekani. Taasisi hii inapokea mapato yote kutoka kwa wafadhili wa kujitolea kote duniani.

Taasisi ya kitaifa na makundi ya watumiaji

Katika nchi mbalimbali kuna shirika za kitaifa zinazojumuisha wanawikipedia ama kwa umbo la taasisi au kwa umbo la makundi ya watumiaji (Wikimedia User Groups).

Nchini Tanzania kuna kundi la Wikimedia Community User Group Tanzania. Kundi la Jenga Wikipedia ya Kiswahili ni jumuiya ya wachangiaji kutoka nchi mbalimbali wanaoangalia maendeleo ya Wikipedia ya Kiswahili.

Tazama pia

  Makala hii kuhusu mambo ya elimu bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wikipedia kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  1. [meta:List_of_Wikipedias List of Wikipedias by article count, users, file count and depth], iliangaliwa tar. 27-11-2018