Wikipedia ya Kiswahili

Wikipedia ya Kiswahili (au Wikipedia kwa Kiswahili) ni toleo la kamusi elezo ya Wikipedia kwa lugha ya Kiswahili.

Wikipedia ya Kiswahili
Wikipedia-logo-v2-sw.svg
Ukurasa wa "Mwanzo" mwaka 2004

Wikipedia ya Kiswahili ilianzishwa tarehe 8 Machi 2003, na tarehe 21 Oktoba, 2020, imefikia makala zipatazo 59,799, idadi inayoifanya iwe Wikipedia ya 86 (kati ya 303 zilizo hai) kwa hesabu ya makala zote.[1]

Kwa hesabu ya makala zenye zaidi ya herufi 200 (yaani bila makala fupi mno) mwaka 2014 ilifikia nafasi ya 71. [2]

Wikipedia ya Kiswahili ilikuwa inafunguliwa na 0,01% ya wanaofungua Wikipedia duniani kote kwenye Septemba 2018, ikiwa katika nafasi ya 65 kati ya lugha zote. Walioivinjari mwezi Septemba 2018 walikuwa katika nchi zifuatazo: Marekani 37.1 %, Tanzania 32 % na Kenya 14.6 %: (mwaka 2017 ugawaji huu ulikuwa: Tanzania 48.5%, Marekani 18.6%, Kenya 14.4%, Ireland 5.1%, Ujerumani 4.9%, kwingineko 8.5%;[3] lakini namba hizo zinacheza kirahisi kama, kwa sababu fulani, labda habari zinazotangazwa kwenye vyombo vya habari, watu wengi wanatafuta habari fulani kwenye intaneti, maana huko Marekani ni rahisi kwa Waswahili walioko pale wasio wengi sana, lakini wana urahisi kutumia intaneti, wanaweza kuzidi watumiaji wa Tanzania ambako watu wengi bado hawana njia ya kutumia mtandao).

Mwezi huohuo, waliofungua Wikipedia nchini Kenya walikuwa 0,10% za wasomaji wote duniani; kati yao waliofungua Wikipedia ya Kiswahili walikuwa 1%. Kumbe nchini Tanzania waliofungua Wikipedia walikuwa 0,04% za wasomaji wote duniani, lakini kati yao 8.6% waliifungua kwa Kiswahili.

Kumbe mnamo Septemba 2018, Wikipedia ya Kiswahili imekuwa inafunguliwa na 0,01% ya wanaofungua Wikipedia duniani kote, ikiwa na nafasi ya 65 kati ya lugha zote. Walioivinjari mwezi huo walikuwa katika nchi zifuatazo: Marekani 37.2 %, Tanzania 32%, Kenya 14.6%, China 5.4%, Ufaransa 3%, kwingineko 7.8%.

Mwezi huohuo, waliofungua Wikipedia nchini Kenya walikuwa 0,08% za wasomaji wote duniani; kati yao waliofungua Wikipedia ya Kiswahili walikuwa 1.7%. Kumbe nchini Tanzania waliofungua Wikipedia walikuwa 0,03% za wasomaji wote duniani, lakini kati yao 11.2% waliifungua kwa Kiswahili, asilimia inayozidi kukua kadiri makala zinavyoongezeka na kuwa bora zaidi.

Katika mwezi Julai 2020 Wikipedia ya Kiswahili iliangaliwa mara milioni 2 hivi, ambayo ni sawa na mara 67,200 kwa siku au mara 2,800 kwa saa. Karibu nusu ya wasomaji wetu wako Tanzania, asilimia 10 wako Kenya, na asilimia 17 wako Marekani. Asilimia 25 za wasomaji wako sehemu nyingine duniani.

MaendeleoEdit

Mnamo Julai 2006 Wikipedia ya Kiswahili ilifikisha makala 1,000.

Mnamo tarehe 14 Septemba mwaka huohuo ilifikia makala ya 2,000.

Mnamo Julai 2007 ilifikisha makala 5,000 na tarehe 26 Septemba 2007, 6,000.

Mnamo tarehe 21 Aprili 2008, Wikipedia ya Kiswahili ilifikisha makala 7,000.

Ilipofika tarehe 19 Desemba 2008 ilifikisha makala 8,000, hasa baada ya kuanzishwa makala nyingi za mbegu za kata za Tanzania.

Makala za mbegu za Tanzania, ziliendelea kuisukuma Wikipedia ya Kiswahili hadi kufikia kiwango cha makala 9,000 tarehe 2 Februari 2009 na makala 10,000 tarehe 21 Februari 2009.

Ilipofika tarehe 9 Aprili 2009, Wikipedia ya Kiswahili ilifikia kiwango cha makala 11,000 na tarehe 25 Aprili 2009 ilifikia makala 12,000.

Mnamo tarehe 20 Juni 2009, Wikipedia ya Kiswahili ilibadilisha ukurasa wake wa mwanzo katika sura mpya.

Mnamo tarehe 17 Agosti 2009 ilifikia makala zipatazo 13,000, na kuendelea kuifanya iwe Wikipedia ya kwanza kwa ukubwa katika Afrika.

Haikushia hapo na ilivyofika tarehe 11 Septemba 2009, Wikipedia hii ilifikia makala 14,000 na tarehe 25 Desemba 2009 makala 15,000.

Tarehe 31 Mei 2010 ilifikia makala 18,000 na tarehe 21 Agosti mwaka huohuo makala 20,000.

Tarehe 28 Oktoba 2011 ilifikia makala 22,000.

Tarehe 15 Februari 2014 ilifikia makala 26,000 na tarehe 28 Oktoba mwaka huohuo makala 27,000.

Tarehe 25 Januari 2015 ilivuka idadi ya makala 28,000.

Tarehe 13 Juni 2015 ilifikia makala 29,000 na kusonga mbele.

Tarehe 22 Septemba mwaka huohuo ilifikia makala 30,000 na kuendelea tena.

Upande wa maharirio, tarehe 10 Oktoba 2015 yamefikia idadi ya milioni 1.

Tarehe 10 Novemba mwaka huohuo ilivuka makala 31,000 na kupiku Wikipedia ya Kiyoruba.

Tarehe 13 Februari 2016 ilivuka idadi ya makala 32,000 na kusonga mbele kiasi cha kufikia 33,000 tarehe 18 Aprili 2016.

Idadi ya 34,000 ilifikiwa tarehe 20 Agosti 2016 kwa makala Kinung.

Makala juu ya James Tate imeifanya itimize idadi ya 35,000 tarehe 12 Januari 2017. Mwaka huohuo, tarehe 20 Mei 2017 idadi ya makala ilifikia 36,000, tarehe 30 Julai ilifikia 37,000 kwa makala juu ya Ziwa Ambussel, tarehe 12 Oktoba 38,000 kwa makala juu ya mto Jubba na tarehe 24 Desemba ilifikia 39,000.

Tarehe 17 Machi 2018 mradi wa milima umeleta makala ya 40,000: Nidze.

Mradi wa mito ya Tanzania umesukuma Wikipedia hii kufikia idadi ya makala 41,000 kwa ukurasa wa Mto Ligunga tarehe 2 Mei 2018 na 42,000 kwa ukurasa wa mto Jigulu tarehe 21 Mei.

Mradi wa mito ya Kenya umefikisha idadi ya makala kuwa 43,000 kwa ukurasa juu ya Mto Kaptarit tarehe 7 Julai 2018, kuwa 44,000 tarehe 30 Julai kwa ukurasa juu ya mto Nyairoko, kuwa 45,000 tarehe 12 Agosti kwa ukurasa juu ya Mto Ilangi, kuwa 46,000 tarehe 15 Oktoba kwa ukurasa juu ya mto Wakavi, tena kuwa 47,000 tarehe 8 Novemba kwa ukurasa juu ya mto Olkimatare.

Tarehe 7 Februari 2019 mradi wa visiwa vya Tanzania umevusha Wikipedia yetu katika elfu ya 48 kwa ukurasa juu ya kisiwa cha Musira.

Tarehe 23 Machi 2019 mradi wa Mito ya Uganda umevusha Wikipedia yetu katika elfu ya 49 kwa ukurasa juu ya mto Wangodugu, tarehe 3 Mei 2019 umeifikisha katika idadi ya 50,000 kwa ukurasa juu ya mto Ocere, tarehe 31 Mei umeivusha tena katika elfu ya 51 kwa makala juu ya mto Osia na tarehe 16 Julai umeifikisha idadi ya 52,000 kwa makala juu ya Mto Rwoho.

Tarehe 10 Agosti 2019 mradi kuhusu ugatuzi nchini Cote d'Ivoire umezaa makala ya 53,000 kuhusu Tarafa ya Tiémélékro. Tunawashukuru wachangiaji wetu kutoka nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Tarehe 4 Oktoba 2019 mradi kuhusu watakatifu wa Afrika umefikisha makala za Wikipedia hii katika idadi ya 54,000 kwa ukurasa juu ya wafiadini Suksesi na wenzake 17.

Tarehe 13 Desemba 2019 mradi huohuo umefikisha idadi ya makala hadi 55,000 kwa ukurasa juu ya Yusto askofu.

Tarehe 10 Machi 2020 mradi wa Makabila ya Uganda umefikisha Wikipedia yetu kwenye makala ya 56,000 kwa ukurasa juu ya Wakumam.

Tarehe 17 Machi 2020 mradi wa wachezaji wa mpira wa miguu umefikisha Wikipedia yetu kwenye makala ya 57,000 kwa ukurasa juu ya Gilmar Rinaldi. Kurasa elfu kwa juma moja tu!

Tarehe 3 Aprili 2020 mradi wa mito ya Burundi umefikisha Wikipedia yetu kwenye makala ya 58,000 kwa ukurasa juu ya Mto Gihororo (Karuzi).

Tarehe 22 Mei 2020 mradi wa miji ya Rwanda umefikisha Wikipedia yetu kwenye makala ya 59,000 kwa ukurasa juu ya Mukarange.

Tarehe 20 Agosti 2020 mradi wa mito ya Burundi umefikisha Wikipedia yetu kwenye makala ya 60,000 kwa ukurasa juu ya Mto Rubirizi (Muramvya).

Kati ya Wikipedia za AfrikaEdit

Kwa lugha zenye asili ya Afrika na visiwa vya jirani, Wikipedia kwa Kiswahili ndiyo ya tatu kwa idadi ya makala zote ikifuatia Wikipedia ya Kimalagasy na Wikipedia ya Kiafrikaans. Kwa kuangalia yaliyomo halisi (bila makala mafupi sana) ndiyo ya pili baada ya Kiafrikaans.

Pia, ndiyo ya kwanza kati ya Wikipedia za lugha za Niger-Kongo kuvuka kiwango cha makala 1,000. Sasa ziko nne.

Wikipedia kwa Kiswahili, ndiyo ya pili katika Afrika kuvuka kiasi cha makala 10,000 baada ya Wikipedia ya Kiafrikaans. [4]

Tazama piaEdit

MarejeoEdit

Viungo vya njeEdit