Kwa gari la kijeshi linalobeba silaha tazama hapa: Kifaru (jeshi)

Kifaru
Rhino-216.jpg
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mammalia (Wanyama wenye viwele wanaonyonyesha wadogo wao)
Oda: Perissodactyla (Wanyama wenye kidole kimoja au vitatu mguuni)
Familia: Rhinocerotidae
Gray, 1820
Ngazi za chini

Jenasi 4:

Ceratotherium Gray, 1868
Dicerorhinus Gloger, 1841
Diceros Gray, 1821
Rhinoceros Linnaeus, 1758

Vifaru au faru ni wanyamapori wakubwa wa familia Rhinocerotidae. Spishi mbili zinapatikana Afrika na nyingine tatu huko Asia. Nchini Uhindi wanabaki faru 2700 tu na hata faru weupe nao wameadimika sana duniani.

Faru hufahamika sana kwa umbo lake kubwa (ni miongoni mwa wanyama walanyasi wakubwa sana ambao wanabakia); huku kila spishi ya faru ikikaribia kuwa na uzito wa tani moja na ngozi ngumu ya kujilinda, yenye unene wa sentimeta 1.5 – 5.0; ubongo mdogo wa mamalia (gramu 400 – 600) na pembe kubwa. Hula sana majani.

Faru wana uwezo mkubwa wa kusikia na kunusa, lakini uoni wao si mzuri sana. Weusi huishi kwa miaka 60 na zaidi.

Faru huthaminiwa sana kutokana na pembe zao. Pembe hizo zimetengenezwa kwa keratini, protini, sawa na ile inayopatikana kwenye nywele na kucha.[1] Faru wa Afrika na Sumatra wana pembe mbili huku wale wa Uhindi na Java wakiwa na pembe moja tu. Faru wa Afrika hukosa meno ya mbele na kutegemea zaidi magego katika kusaga chakula.

UainishajiEdit

Kuna spishi tano zinazoweza kuwekwa katika makundi matatu. Spishi mbili za Afrika, faru mweupe (white rhinoceros) na faru mweusi (black rhinoceros) walitokea kama miaka milioni 5 iliyopita. Tofauti kubwa kati ya faru mweupe na faru mweusi ni muundo wa midomo yao. Faru mweupe ana mdomo mpana kwa ajili ya kula nyasi huku mdomo wa faru mweusi ikiwa imechongoka kiasi.

Faru mweupeEdit

 
Faru mweupe huyu, White Rhinoceros, kimsingi ni wa kijivu

Faru weupe kwa muonekano ni wa kijivu. Maana ya neno weupe ilikosewa tu kutokana na neno la kiholanzi ‘wijd’ lenye maana ya upana ‘wide’ ambalo lilizoeleka kama ‘white’ ambalo sasa laeleweka hivyo kama mweupe. Aliitwa hivyo kwa maana ya upana, sababu wa mdomo wake mpana wenye umbo la mraba.

Faru mweupe ndiyo mnyama mkubwa wa ardhini baada ya tembo. Anakaribiana kidogo na faru wa India na kiboko. Faru weupe wana mwili uliojaa, na kichwa kikubwa, shingo fupi na kifua kipana. Faru anaweza kuzidi uzito wa kilogramu 3,500 na urefu wa mita 3.5 – 4.6 kuanzia kichwani na mabega ya urefu wa sentimeta 180 – 200. Uzito wa faru mweupe uliovunja rekodi ni ule wa kilogramu 4,500.[2] Ana pembe mbili huku ile ya mbele ikiwa kubwa zaidi hata kufikia urefu wa sentimeta 90 – 150. Faru weupe pia wana nundu kubwa inayoshikilia vichwa vyao vizuri. Huwa na nywele kadhaa hasa kwenye masikio yao na mkiani, sehemu nyingine za mwili zikiwa zimesambaa kidogo tu.

Faru mweusiEdit

 
Faru mweusi ana mdomo uliochongoka.

Faru weusi wana mdomo uliochongoka. Wanafanana kwa rangi na faru weupe. Hii inachanganya sana, sababu majina yao ni tofauti lakini rangi zao ni sawa kabisa. Spishi hii ina spishi nyingine nne ndani yake. Faru mkubwa mweusi huwa na urefu wa sentimeta 132 – 180 mabegani mwake na urefu wa mita 2.8 – 3.8 kuanzia kichwani mwake.[3] Huwa na uzito wa kilogramu 850 mpaka 1600, na wachache mpaka kg 1800, huku faru jike wakiwa na umbo dogo kiasi kuliko wanaume. Pembe kubwa mbili zimetengenezwa kwa keratini huku ile kubwa ya mbele ikiwa ina urefu wa mpaka sentimeta 50, na mmoja aliwahi hata kufikia sentimeta 140. Wakati fulani hata pembe la tatu hujitokeza. Faru weusi ni wadogo kiasi kuliko faru weupe, na wana mdomo uliochongoka kwa ajili ya kukusanya majani kabla ya kula.

Kutokana na umuhimu wa wanyama hawa nchi ya Tanzania imeamua kuwatunza faru kwa kuwaweka sehemu isiyorasmi kwao kwa uangalizi mkubwa, maeneo kama grumeti na pia kwa kuwapa majina, kwa mfano Faru John.

Faru wa IndiaEdit

 
Faru wa India na mwanae.
 
Sanamu ya Faru wa shaba, wa Western Han (202 K.K – 9 BK) nyakati za China

Faru wa India hasa wanapatikana sana huko Nepal na hasa kaskazini – mashariki mwa India. Sasa wanapatikana Pakistan mpaka Bama na wamefika hadi China. Lakini kutokana na mwingiliano wa binadamu, uwepo wao umeathirika na wameanza kupungua. Ngozi yao pana ya kahawia karibu na kijivu yenye mikunjo. Juu ya miguu yao na mabega yao kuna vijinundu, na wana nywele kidogo kwenye miili yao. Faru dume huwa wakubwa kiasi kuliko faru jike kufikia uzito wa kilogramu 2500 – 3200. Faru hawa wana urefu wa sentimeta 175 – 200 mabegani. Faru jike wa india hufikia mpaka uzito kilogramu 1900. Faru hawa hufikia mpaka urefu wa mita 3.0 – 4.0. Karibu theluthi mbili ya faru wote waliobaki duniani, wanapatikana katika mbuga ya Taifa Kaziranga huko India.

Faru wa JavaEdit

Hawa ndio mamalia wakubwa walio hatarini kutoweka. Mpaka mwaka 2002, walikuwa wamebaki faru 60, huko Java Indonesia na Vietnam. Hii ndio spishi ndogo kuliko wote. Wanyama hawa wanapenda kukaa kwenye misitu ya mvua, nyasi ndefu na maeneo yenye mafuriko ya hapa na pale na matope.

Faru wa Java pia wana pembe moja. Pia ngozi yao ya kijivu ina mikunjo na wana nundu kama faru wa India, na hawana nywele. Urefu wa mwili wake ni mita 3.1 – 3.2, pamoja na kichwa na urefu wa mita 1.5 – 1.7. Faru wakubwa wanaripotiwa kufikia uzito wa kilogramu 900 – 1400 au 1360 – 2000, kwa chanzo tofauti. Pembe za faru dume hufikia mpaka sentimeta 26 huku faru jike huwa na nundu tu, na wakati mwingine hawana kabisa.

Faru wa SumatraEdit

 
Faru wa Sumatra huko Bronx Zoo

Hawa ndio faru wadogo kabisa katika spishi zote za faru na ndiye huyu pekee mwenye manyoya mengi na anayeweza kuishi katika sehemu za juu hasa za Borneo na Sumatra. Kutokana na kuharibika kwa makazi yao na ujangili, wameadimika sana na miongoni mwa mamalia walioadimika sana. Mpaka sasa inaaminika sana kwamba wamebaki faru 275 wa spishi hii.

Faru wa Sumatra wana kimo cha urefu wa sentimeta 130 mpaka mabegani, na mwili wake wa urefu sentimeta 240 – 315, na wana uzito wa kilogramu 700, japo baadhi yao wana uzito hata kufikia kilogramu 1000. Kama faru wa Afrika, hao wana pembe mbili zenye urefu mpaka sentimeta 25 – 27 na ile pembe ya pili ni ndogo na huwa ndogo kufikia sentimeta 10. Faru dume wana pembe kubwa kuliko faru jike. Nywele/manyoya ya miili yao hupungua kadiri wanavyoongezeka umri. Rangi ya faru hawa ni kahawia – nyekundu. Mwili wao ni mfupi na miguu yao pia na midomo yao ina nguvu sana.

MarejeoEdit

  1. Scientists Crack Rhino Horn Riddle?. Ohio University (11 November 2006). Iliwekwa mnamo 15 October 2014.
  2. African Rhinoceros?. Safari Now (18 December 2013). Iliwekwa mnamo 15 October 2014.
  3. Black Rhinoceros?. Bisbee's Conservation Fund. Iliwekwa mnamo 15 October 2015.