Utaridi
Utaridi ni sayari iliyo karibu zaidi na Jua katika Mfumo wa Jua.
Utaridi | |
---|---|
Picha yenye rangi halisi ya Utaridi kutoka MESSENGER. | |
Jina | |
Asili ya jina | Kar. عطارد (ʿuṭaarid) |
Majina mengine | Mercury (Kng.) |
Alama | |
Tabia za mzunguko | |
Mkaribio | km 46,000,000 va 0.307499 |
Upeo | km 69,818,000 va 0.466697 |
km 57,909,000 va 0.387098 | |
Uduaradufu | 0.205630 |
siku 87.9691 miaka 0.240846 | |
Mwinamo | 7.005° toka njia ya Jua |
Tabia za maumbile | |
km 2,439.7±1.0 mara 0.3829 ya Dunia | |
Tungamo | kg 3.3011×1023 mara 0.055 ya Dunia |
g/cm3 5.427 | |
Uvutano wa usoni | m/s2 3.7 |
siku 176 | |
Weupe | 0.088 (Bond) 0.142 (jiometri) |
Halijoto | K 437 (164°C) |
Asili ya jina
haririJina lake limetokana na Kiarabu عطارد (soma ʿuṭaarid) inayomaanisha "mwendo wa haraka"[1] kwa sababu kasi ya Utaridi inapita mwendo wa sayari nyingine kutokana na njia yake fupi ya kuzunguka Jua katika siku 88 pekee.
Majina ya Wagiriki wa Kale "Hermes" na Waroma wa Kale "Mercurius" yalikuwa majina ya mungu wao aliyekuwa na kazi ya kuwasilisha habari za miungu wengine aliyeaminiwa kuwa na kasi kubwa kwa kazi hii: chaguo hili lilitokana na tabia ileile ya sayari. Jina hili la Kiroma Mercurius limeingia katika lugha nyingi za Ulaya.
Umbo la Kiarabu limekuwa jina la watu katika nchi nyingi zilizoathiriwa na utamaduni wa Kiislamu, pia jina la sayari ya kwanza kwa mfano katika Kituruki na Kimalaysia.
Katika vitabu kadhaa vya Kiswahili sayari inaitwa Zebaki lakini hii inaonekana ni kosa lililotokana na jina la Kiingereza "Mercury" kwa sayari hii. Mercury ni pia jina la metali inayoitwa zebaki kwa Kiswahili kutokana na Kiarabu زئبق (soma ziʾbaq). [2]
Mara chache neno "Utaridi" limetumiwa kutaja sayari kibete ya "Pluto" lakini hii ni kwa kukosea pia.[3]
Tabia za Utaridi
haririUtaridi ni sayari ndogo. Kipenyo chake kwa ikweta ni km 4879.4. Kwa sababu iko karibu sana na Jua ina mbio za haraka. Mwaka wa Utaridi ambayo ni muda wa kuzunguka Jua ni siku 88 za Dunia pekee.
Inazunguka kwenye mhimili wake katika muda wa siku 58.6 za Dunia. Kutokana na kuwa karibu na Jua kuna joto kali upande unaotazama Jua lakini upande wa usiku ni baridi kabisa kutokana na uhaba wa hewa inayoweza kutunza halijoto. Halijoto ya wastani ni +178.8°C, (usiku -183.15°C na mchana +426.85°C).
Mwaka 2012 barafu ya maji ilitambuliwa kwenye data kutoka chombo cha angani MESSENGER iliyochunguza sayari hii. Barafu inapatikana karibu na ncha ya kaskazini isiyofikiwa na miale ya Jua.[4]
Uhaba wa hewa umesababisha uso wa sayari kujaa mashimo ya kasoko. Kasoko hizi zimesababishwa kwa kugongwa na vimondo. Angahewa kama Duniani ingeangamiza vimondo vidogo na kusababisha kupasuka kwa kubwa lakini Utaridi zote zinafika usoni bila kizuizi. Alama za vimondo ni mmomonyoko wa pekee unaoonekana hakuna dalili ya mmomonyoko kutokana na hewa au maji ya awali.
Kutokana na kuwa karibu sana na Jua Utaridi inaonekana kama nyota kwa macho katika masaa ya pambazuko na machweo pekee.
Marejeo
hariri- ↑ ling. طرد ṭarada: drive way, chase away; مطارد muṭarid: chaser, hunter; cf "Dictionary of Modern written Arabic3" ya Hans Wehr
- ↑ kuhusu majina ya sayari zilizojulikana kwa Waswahili na hivyo kuwa na majina ya asilia linganisha Jan Knappert, Swahili Islamic poetry, Brill 1971, Vol 1 uk 96-97 - taz google booksearch [1]
- ↑ Soma hapa kuhusu matatizo ya matumizi ya majina ya sayari katika kamusi za Kiswahili.
- ↑ Water Ice Discovered on Mercury (space.com tar. 3 Dis 2012)
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Utaridi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |