Zohali
Zohali ni sayari ya sita kutoka Jua katika Mfumo wa Jua. Ni sayari kubwa ya pili baada ya Mshtarii.
Zohali | |
---|---|
Picha ya Zohali na bangili zake kutoka Cassini. | |
Jina | |
Asili ya jina | Kar. زحل (zuḥal) |
Majina mengine | Zuhali, Zohari Saturn (Kng.) |
Alama | |
Tabia za mzunguko | |
Mkaribio | km 1,352,550,000 au 9.0412 |
Upeo | km 1,514,500,000 au 10.1238 |
km 1,433,530,000 au 9.5826 | |
Uduaradufu | 0.0565 |
siku 10,755.70 miaka 29.4475 | |
Mwinamo | 2.485° toka njia ya Jua |
Miezi | 146 |
Tabia za maumbile | |
km 58,232 mara 9.123 ya Dunia | |
Tungamo | kg 5.6834×1026 mara 95.159 ya Dunia |
g/cm3 0.687 | |
Uvutano wa usoni | m/s2 10.44 |
km/s 35.5 | |
saa 10.5433 | |
saa 10.5606 | |
Weupe | 0.342 (Bond) 0.499 (jiometri) |
Halijoto | K 134 (−139.15°C) |
Inaonekana kwa macho matupu si lazima kutumia darubini. Kwa hiyo imeshajulikana tangu zamani ilitambuliwa na wataalamu wa nyakati za kale.
Uso wa Zohali hauonekani kwa sababu angahewa nzito inafunika kila sehemu. Mada ya angahewa ni hasa hidrojeni. Kutokana na uzito wa angahewa shinikizo ndani yake inaongezeka sana katika vilindi vyake na kusababisha gesi za angahewa kuingia katika hali ya giligili inayobadilika kuwa mango hadi metali ndani zaidi.
Njia ya Zohali
Zohali inazunguka Jua kwa kutumia njia ambayo inakaribia kuwa na umbo la mviringo.[1] Sehemu ambako inakaribia Jua zaidi (periheli) ina umbali wa vizio astronomia 9.04, sehemu ambako ni mbali zaidi (afeli) ina umbali wa vizio astronomia 10.12.
Muda wa kumaliza njia ya kuzunguka Jua ni miaka 29 na siku 166. [2]
Mzunguko wa sayari
Zohali inazunguka kwenye mhimili wake katika muda wa takriban saa 10 na nusu. Maanake siku ya Zohali ni fupi kuliko siku ya Dunia, chini ya nusu yake.
Kuna tofauti katika kasi ya mzunguko huu kati ya kanda tofauti za Zohali. Kanda ya ikweta linazunguka haraka zaidi kiasi kuhusu sehemu nyingine.
Kanda ya ikweta linazunguka katika muda wa saa 10 na dakika 14, lakini maeneo yaliyo mbali na ikweta yanazunguka katika muda wa saa 10 na dakika 38.
Hii inatokana na tabia za muundo wake kuwa mwili wa sayari hii imejengwa kwa gesi hasa hidrojeni inayopatikana kama hali ya gesi kwenye sehemu za nje na kiowevu katika tabaka za chini zaidi kwa hiyo sehemu kubwa ya masi yake si mango.
Muundo wa sayari
Zohali huhesabiwa kati ya sayari jitu za gesi yaani sayari kubwa sana zilizojengwa hasa kwa gesi inayopatikana katika hali mbalimbali kutokana na shinikizo kubwa inayotokea katika vilindi vyake.
Kipenyo cha Zohali ni takriban kilomita 120,000 na hii ni nafasi ya pili baada ya Mshtarii katika mfumo wa Jua na sayari zake.
Masi yake ni ndogo kulingana na mjao wake: ina mjao wa 58% za Mshtarii lakini masi ni chini ya theluthi moja ya Mshtarii. Kwa hiyo densiti yake ni ndogo imekadiriwa kuwa 0.687 g/cm³ pekee.
Si rahisi kutofautisha kati ya angahewa ya sayari hii na uso wake kwa sababu sehemu kubwa ya "mwili" wa sayari ni gesi pia. Angahewa inayotazamiwa kwa nje ina kiwango kikubwa sana cha hidrojeni (96.3%) pamoja na kiasi cha heli (3.25%).
"Uso" wa sayari ni kanda ambako kanieneo angahewa inafikia bar 1 (sawa na kanieneo angahewa duniani kwenye uwiano wa bahari).
Ndani zaidi hii shinikizo inaongezeka na kufanya gesi kuwa na tabia ya kiwevu.
Tena ndani zaidi kiwango cha shinikizo ni kubwa kiasi ya kwamba hidrojeni huwa mango na kuonyesha tabia za metali.
Chini ya tabaka ya hidrojeni metalia wataalamu huamini kuna kiini cha mwamba na barafu.
Miezi ya Zohali
Zohari ina miezi mingi. Miezi thelathini imepewa majina. Kati ya miezi hii Titani ni mkubwa mwenye kipenyo cha km 5,150. Ni mwezi wa pekee unaojulikana kuwa na angahewa. Miezi ya Rea, Dioni, Tethisi na Yapetusi ina vipenyo kati ya km 1,050 na km 1,530.
Bangili za Zohali
Tabia ya pekee ya Zohali ni bangili zake. Mtu wa kwanza wa kuziona alikuwa Galileo Galilei alipotazama sayari hii kwa darubini yake. Lakini Galileo alishindwa kutambua alichoona kutokana na kasoro za darubini yake. Aliandika wakati ule ya kwamba Zohali ilikuwa na "masikio". Mwaka 1655 Mholanzi Christiaan Huygens aliweza kutumia darubini kubwa zaidi akatambua "masikio" ya Galilei kuwa bangili inayozunguka sayari.
Siku hizi imejulikana ya kwamba bangili ni vipande vya barafu, vumbi na mawe. Vipande vyake vina ukubwa kati ya milimita chache hadi mita kadhaa kama motokaa. Unene wa bangili ni mita mamia kadhaa.
Tangu kuboreka kwa darubini na kupita kwa vipimaanga karibu na sayari za mbali bangili zimetambuliwa pia kwa sayari za Mshtarii, Uranus na Neptuni lakini ni dhaifu hazionekani kwa darubini sahili ya mkononi.
Marejeo
Viungo vya nje
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Zohali kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |