Kreshensi wa Iesi
Kreshensi Grizi wa Iesi (alifariki mwaka 1263) alikuwa na mtawa wa Kanisa Katoliki aliyeongoza Ndugu Wadogo ka mkuu wa shirika lote (1244-1247). Hatimaye akawa askofu.
Alipokufa Aimoni wa Faversham (1244), mvutano ndani ya shirika la Ndugu Wadogo ulijitokeza kwa nguvu. Mtumishi mkuu aliyechaguliwa, Kreshensi wa Iesi akiona kwamba Fransisko wa Asizi alitazamwa bado na wote kuwa kielelezo cha wadogo, aliagiza mapema zikusanywe habari zote juu yake[1], halafu akamuagiza Thoma wa Celano aandike upya maisha ya mwanzilishi[2]. Mkusanyo huo unaitwa Assisi Compilation au kwa majina mengine.[3].
Waliolilia hali ya awali (wenzi wa Mt. Fransisko na ndugu “wenye ari”) walipoona Mtumishi mkuu hakubaliani nao, walichagua wajumbe 72 wakajieleze kwa Papa Inosenti IV (1243-1254) ili aingilie kati. Lakini Kreshensi aliwasema kwa Papa na kumuomba awaadhibu; mwenyewe aliwatawanya wengine ili awavunje nguvu.
Papa, akiwa mwanasheria mwenye hakika kuhusu ukuu wa mamlaka yake, aliona kanuni ya Ndugu Wadogo, kama kanuni nyingine zote, ni sheria tu ambayo Papa anaweza kuifanyia lolote; vilevile aliona shirika lao kuwa kama mengine yote akalisukuma lizidi kutia maanani elimu. Hivyo alitoa (1245) tamko la pili juu ya kanuni ili kuilegeza: hasa alitamka kuwa vitu vyote ambavyo shirika linavyo, kama si vya wafadhili tena, basi ni vya Papa. Hivyo kwa kutofautisha kutumia vitu na kuvimiliki kisheria, Ndugu Wadogo waliweza kujidai mafukara ingawa wanatumia vingi, eti si vya kwao! Lakini wengi hawakuridhika na ujanja huo, usiolingana na roho ya Kiinjili ya Fransisko, wala na dhuluma za Kreshensi dhidi ya ndugu wenye ari.
Basi, katika mkutano mkuu ulioagizwa na Papa walimuondoa madarakani wakamchagua Yohane wa Parma (1247-1257), mtu wa kufaa sana kwa elimu na utakatifu, aliyeongoza hasa kwa mfano wa maisha yake bora.
Tanbihi
haririViungo vya nje
hariri- [1] Ilihifadhiwa 19 Mei 2011 kwenye Wayback Machine.