Ari (kutoka neno la Kiarabu; kwa Kiingereza: zeal) ni adili linalompasa mtu katika utumishi wa Mungu. Ari kwa utukufu wake na kwa wokovu wa watu ni ari moja, ni umotomoto wa upendo uleule unaotakiwa kuwepo hata katika ukavu na majaribu ya kila aina; pengine huo umotomoto wa utashi una juhudi na stahili kadiri mtu asivyouhisi.

Sababu za ari hiyo katika Ukristo hariri

Sababu ya kwanza ni kwamba Mwenyezi Mungu anastahili kupendwa kuliko yote: amri kuu isiyo na mipaka inatudai tukue daima katika upendo. Amri hiyo ilitolewa tayari katika Agano la Kale kwa maneno yaleyale ambayo Yesu akaja kuyatumia. Manabii pia walikuwa na ari ya kuikumbusha mfululizo itimizwe na taifa la Mungu, hasa Eliya, nabii wa moto. “Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana, Mungu wa majeshi, kwa kuwa wana wa Israeli wameacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga, nami nimesalia, mimi peke yangu: nao wanitafuta roho yangu waiondoe” (1Fal 19:14). “Wivu wa nyumba yako umenila” (Zab 69:9). “Juhudi yangu imeniangamiza” (Zab 119:139). “Finehasi, baba yetu, kwa sababu alikuwa na juhudi nyingi, alipewa ahadi ya ukuhani wa milele… Eliya, kwa kuwa aliona wivu mwingi kwa ajili ya sheria, alichukuliwa juu mbinguni… Basi, ninyi, wanangu, mwe hodari, mfanye kwa kiume kwa ajili ya sheria, maana kwa hiyo mtatukuzwa” (1Mak 2:54,58,64). Ari hiyohiyo ilimfanya Yesu afukuze wafanyabiashara hekaluni na kupindua meza zao. Ari hiyohiyo inadumu hata leo katika Kanisa popote pale unapotolewa ushuhuda wa damu na katika maisha ya wengi waliowekwa wakfu kama sadaka ya kuteketezwa.

Sababu ya pili ni kwamba Wakristo wanapaswa kumuiga Bwana Yesu Kristo, aliyewaka upendo: “Nimekuja kutupa moto duniani: na ukiwa umekwishawashwa, ni nini nitakalo zaidi?” (Lk 12:49). Tangu atwae mwili alijitoa mfululizo katika maisha yaliyofichika, akituonyesha namna ya kujiandaa kwa unyenyekevu na kwa kujikana tufanye kazi za Mungu. Toka mwanzo wa utume wake akaonja uchungu uliolingana tu na upendo wake: uchungu wa upendo wenye ari unaotaka kujitoa, kumbe unakuta hali ya kutojali, kutobadilika, kutoelewa, ubaya na upinzani wenye chuki. Ari ndiyo iliyosababisha uchungu wake mbele ya dhambi za watu, na uchungu wa Maria chini ya msalaba. Maisha yake yote Yesu aliteseka moyoni, akitamani kutimiza ukombozi wetu: “Nina ubatizo unipasao kubatizwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe!” (Lk 12:50). “Nimetamani sana kula Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu” (Lk 22:15). Uchungu wake ulikoma alipokufa msalabani, lakini kiu ya wokovu wetu anayo hadi sasa: “Maana yu hai sikuzote ili awaombee” (Eb 7:25) hasa katika sadaka ya misa. “Ningependa kukuona unateswa sana na njaa ya wokovu wa watu hadi ufe kwayo, kama alivyofanya Yesu Kristo. Walau ikufanye ufie ulimwengu na kujifisha” (Katerina wa Siena).

Sababu ya tatu ni thamani ya watu wenye roho isiyokufa, waliokombolewa kwa damu ya Yesu Kristo. Kila mmojawao ni bora kuliko ulimwengu wote na anaitwa kufaidi uzima wa milele. Baada ya mitume, wafiadini walikuwa na ari kiasi kwamba ni thibitisho lisilopingika la utakatifu wa Kanisa. Tukiipenda nchi yetu hata kujitoa mhanga kwa ajili yake, zaidi tunapaswa kulipenda Kanisa linalotuongoza kwenda kwetu, ambako waadilifu wa mataifa yote watakusanyika pamoja milele. Vilevile kuna ari ya kuziombea roho za toharani.

Hatimaye sababu ya nne ni juhudi za maadui wa Mungu katika kueneza fujo, upotovu na mauti. Kuna vita vya kishetani dhidi ya Bwana, vita vikali kuliko vyote kwa sababu ni vya roho, vinafikia mioyo ya watoto ili wawe waovu wasioishi kwa Mungu. Sawa na dhambi za roho, uovu wa vita hivyo hausemeki na majukumu yake ni ya kutisha. Kanisa linaona hasa madhara kwa wale wanaovipiga, na linaendelea kuwaombea Mungu awafumbue macho na kuwazuia wasifuate hata mwisho njia ya laana ya milele ambako wanavuta wengine wengi.

Ari iwe na sifa gani hariri

Ari inatakiwa iwe motomoto kwa sababu ni mwako wa upendo. Lakini ni umotomoto wa Kiroho wenye kudumu, si ule wa kihisi ambao unatokana na silika na kujitokeza katika utendaji wa kibinadamu tu, unaolenga kujiridhisha na kujipatia sifa hata kukinaisha watu. Ili umotomoto udumu upande wa roho unatakiwa uwe na mwanga, subira, upole na usijitafutie faida.

Kwanza iwe imeangazwa na imani, utiifu, busara ya Kikristo na vipaji vya hekima na shauri. Mwanga wa akili hautoshi, kwa sababu kazi ya kufanywa si ya kibinadamu, bali ya Kimungu na inatakiwa kufuata njia alizotuelezeka Bwana. Umotomoto wa umbile tu, badala ya kuongoza watu kwa Mungu, polepole unaongozwa na ulimwengu na udanganyifu wake. Umotomoto huo wa wasiotulia, wavurugaji na wapendavyeo unasukumwa na matumbo, hauna busara, haujali nafasi, tena unasahau njia za lazima zipitazo maumbile, hasa sala na toba. Kumbe, hasa katika nafasi ngumu ari inatakiwa kumuomba Roho Mtakatifu mwanga ili itimize vizuri iwezekanavyo si mambo ya ajabu bali yale ya kawaida yaliyopangwa na Kanisa na viongozi: kuadhimisha au kushiriki misa, kuwa waaminifu kwa sala inayotupasa na kwa wajibu mwingine wowote. Tusipokuwa na mwanga huo sifa zetu haziwezi kutosha, kwa kuwa pengine tunadaiwa utiifu wa kishujaa.

Halafu iwe na subira na utamu, iepe kukasirikia bure maovu na kukaripia ovyo, ivumilie mabaya kadhaa ili kuepa mengine makubwa zaidi na isigeuke kuwa kali na chungu. Haitakiwi kukomesha yaliyo mema kiasi kana kwamba ni mabaya, wala kuzima “utambi utokao moshi” wala kuvunja “mwanzi uliopondeka” (Math 12:20). Tukumbuke daima kuwa maongozi ya Mungu yanaacha mabaya yatokee ili yapatikane mema makubwa zaidi ambayo hatuyaoni bado, lakini yatang’aa milele.

Ili ari iwe na subira na upole haitakiwi kujitafutia faida, yaani kujitwalia yaliyo ya Mungu na ya watu. Baadhi wana ari kwa kazi za Mungu, lakini wanaziona kama ni za kwao: wanajifanya lengo lake bila kujitambua. Watakapopunguza kujiamini na kujiona wa maana, watakaponyenyekea na kutulia zaidi, Mungu atawatumia kama vyombo visivyozuia kazi yake, nao watajiachia mikononi mwake ambaye pekee anajua yanayohitajika ili kuzaa upya watu. Mara nyingi tunataka kutenda mema, lakini tunatamani mno tuyatende wenyewe na kwa namna yetu, hata tukazuia wengine wasiyafanye wala kufaulu kuliko sisi. Tusiwaonee kijicho kwa mafanikio yao, wala kushughulikia uongozi wa roho tusizokabidhiwa; tukiziondoa kwenye mvuto wa kufaa, Mungu atatudai. Pengine anatukosoa kwa njia ya majaribu yanayoumiza kiburi chetu tusitake tena kutenda kazi yetu. Baada ya kushinda umimi wetu, atatutumia kwa kazi yake ya wokovu. Hapo umotomoto wa Kiroho utakuwa mtulivu, mnyenyekevu na mpole, kama ule wa bikira Maria na wa watakatifu wengine, tena hautakuwa na la kuushinda: “Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?” (Rom 8:31).

Ari hiyo itekelezwe kwa namna mbalimbali za utume: mafundisho ya Kikristo, matendo ya huruma upande wa roho na wa mwili, sala (inayovuta neema izalishe kazi katika shamba la Bwana, hivyo ni roho ya utume wa nje, ingawa imefichika kadiri ilivyo ya dhati), na hatimaye malipizi (ambayo pia yamefichika; ni mwendelezo wa mateso ya Yesu katika mwili wake, ambamo kiungo kimoja kikiteseka kwa upendo, kingine kinapona; kimoja kikijikatalia matakwa yake, kingine kinaongoka na kufufuka).

Basi, katika njia ya utakatifu ari inatakiwa kuwepo, ingawa mara nyingi haipo. Ili idumu inahitaji kulishwa na sala ya dhati na kama ya kudumu katika usikivu kamili.

Tanbihi hariri