Mariamu katika Kurani
Mariamu katika Kurani ni mwanamke pekee kutajwa kwa jina, tena mara 34.
Anatajwa kama mama wa nabii Isa, akichanganywa na dada wa Haruni na Musa, aliyekuwa na jina hilohilo, hivyo anatajwa kama binti Imrani. Pia habari nyingine kadhaa zinapishana na zile za Injili.
Hata hivyo anapewa heshima ya pekee, kama inavyoonekana katika sura ya 3:43: “Na kumbukeni malaika waliposema, ‘Ewe Mariamu, kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuchagua na kukutakasa na kukutukuza kuliko wanawake wa walimwengu”. Tena katika aya 3:46: “Na kumbukeni waliposema malaika: ‘Ewe Mariamu, bila shaka Mwenyezi Mungu anakupa habari njema za Neno litokalo kwake, jina lake Masihi Isa mwana wa Mariamu, mwenye heshima katika dunia na ahera, na yu miongoni mwa waliokaribishwa’”.
Aliambiwa amefanywa “ishara” pamoja na mwanae, ingawa haisemwi ni ishara ya nini. Sura ya 19, yenye jina lake, inaeleza kwamba Malaika Jibrili akimpasha habari ya mimba alisema, ‘Hakika mimi ni mjumbe wa Mola wako ili nikupe mwana mtakatifu’. Akasema, ‘Ninawezaje kupata mtoto hali hajanigusa mwanamume yeyote, wala mimi si mwasherati?’ Akasema, ‘Ni kama hivyo; Mola wako amesema: Haya ni rahisi kwangu, na ili tukufanya ishara kwa mwanadamu na rehema itokayo kwetu, na ni jambo lililokwisha hukumiwa’ ” (19:19-21). “Na mwanamke yule aliyejilinda tupu yake na tukampulizia roho yetu na tukamfanya yeye na mwanawe ishara kwa walimwengu” (21:91).
Pamoja na kusifiwa kwa usafi wake, anaongezewa sifa za imani na unyenyekevu: “Na Mariamu binti Imrani aliyejilinda uchi wake, na tukampulizia humo Roho yetu na kuyasadikisha maneno ya Mola wake, na vitabu vyake; na alikuwa miongoni mwa wanyenyekevu” (66:12).
Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |