Unururifu
Unururifu (kwa Kiingereza radioactivity; pia: mbunguo nururishi kutoka Kiingereza radioactive decay) ni tabia ya elementi kadhaa ambazo kiini cha atomi yake si thabiti, bali inaweza kubadilika kuwa kiini cha atomi kingine na katika mchakato huu kinatoa mnururisho. Wakati wa badiliko atomi inatoa chembe nyuklia. Mifano ya elementi ambazo si thabiti ni urani na plutoni.
Kwa jumla elementi zote ambazo zina masi kubwa kuliko risasi (plumbi) ni nururishi. Hizi ni zote katika jedwali la elementi kuanzia namba 83 Bismuti.
Kuna pia hali za elementi kadhaa ambazo kwa kawaida ni thabiti lakini baada ya kupokea nyutroni ya nyongeza zinakuwa nururishi. Kwa mfano kaboni ya kawaida inayoitwa 12C ni thabiti. Lakini kuna pia kiwango kidogo cha 14C ambayo si thabiti, ni nururishi; hali hii huitwa isotopi cha kaboni. Kaboni ya 14C inatengenezwa mfululizo katika tabaka za juu ya angahewa ya dunia ambako atomu za nitrojeni zinagongwa na miale ya jua na kupotewa na nyutroni; hizi nyutroni zinaweza kugongana tena na atomi ya nitrojeni na kujiunganisha nayo na hivyo kuunda atomi ya 14C.
Tabia hii ya unururifu ilitambuliwa mara ya kwanza na Antoine Henri Becquerel mwaka 1896, halafu ni Marie Curie na Pierre Curie waliotunga neno "radioactivity" (=unururifu) kwa tabia hii. Wote watatu walipokea Tuzo ya Nobel ya Fizikia kwa kazi hii mwaka 1903.
Aina za mnururisho nyuklia
haririWakati wa mbunguo nyuklia mnururisho unatokea hasa kwa namna tatu zinazotajwa kwa herufi za Kigiriki alfa, beta na gamma kuwa mnururisho α, mnururisho β na mnururisho γ. Kati ya hizi kila moja inaweza kuwa hatari kwa binadamu na viumbehai kutegemeana na kiwango chake, lakini hatuna mlango wa fahamu unaoweza kuitambua.
Hatari kwa viumbehai
haririMata nururishi inatoa mnururisho ya kuioniza (ionizing radiation). Mnururisho huu unaweza kuvunja kampaundi za kikemia na molekuli. Kama hii inatokea ndani ya kiumbehai kuna hatari za kiafya pamoja na hatari ya kutokea kwa kansa.
Kiwango fulani cha mnururisho hutokea kiasili katika mazingira yetu na miili yetu imekizoea tangu vizazi. Hali ni tofauti kama kiasi cha mnururisho kinaongezeka kwa mfano kutokana na kuingia mara nyingi katika mashine ya eksirei, katika mazingira ya migodi ya urani, penye ajali kwenye tanuri nyuklia ambako mata nururishi inaachishwa hewani au penye milipuko ya bomu ya nyuklia. Penye viwango vya juu vya mnururisho wa kuioniza kuongezeka kwa kansa kumetazamiwa.
Marejeo
haririTovuti za nje
hariri- [Dangerous Particles Chem 4 kids]
- [[http://web.archive.org/20141023073143/http://www.physics.org/article-questions.asp?id=71 Ilihifadhiwa 23 Oktoba 2014 kwenye Wayback Machine. What is radioactivity? physics org]]
- [What is radioactivity? chemistry.org]
Makala hii kuhusu mambo ya kemia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Unururifu kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |