Maikrowevu

Inatumika kuoka na kupasha vyakula mbalimbali
(Elekezwa kutoka Microwave oven)

Maikrowevu (kutokana na Kiingereza: microwave) ni kifaa kinachopika chakula kwa kutumia vijiwimbi, yaani mawimbi mafupi ya sumakuumeme. Hutumiwa pia kupasha moto vyakula vilivyopikwa tayari.

Maikrowevu.

Inapasha moto haraka sana vyakula vyenye unyevu ndani yake. Maikrowevu za kawaida hufaa pia kuchemsha viwango vidogo vya maji au kiowevu kingine.

Mnururisho wa vijiwimbi husababisha mwendo wa haraka wa molekuli za maji zilizopo ndani ya chakula na mwendo huo unazalisha joto.

Maikrowevu za kawaida kwa matumizi ya nyumbani hufaa kwa kiwango cha chakula hadi gramu 500 hivi, au kwa nusu lita ya maji, vilevile kupasha moto chai au kahawa iliyopoa. Inapasha moto katika dakika chache. Kwa viwango vikubwa zaidi haifai. Faida kubwa ni kwamba chakula au kinywaji huwekwa ndani ya maikrowevu kwenye sahani au kikombe cha mezani, kwa hiyo hakuna haja ya kuchafua sufuria.

Inavyofanya kazi

hariri
 
Magnetroni kutoka kwenye maikrowevu

Maikrowevu hutumia magnetroni. Kazi yake inafanana na upelekaji redio. Inatoa mawimbi ya sumakuumeme mafupi sana ambayo huingia kwenye chakula kwa kina cha karibu sentimita 2.5. Mnururishoo husababisha molekuli za maji ndani ya chakula kugeuka mara bilioni 2,5 kila sekunde. Mwendo huo unasababisha joto.

Hii pia hufanyika katika joko la kawaida, lakini nishati ya maikrowevu inaingia ndani zaidi ili chakula kiweze kuiva haraka sana. Katika joko la kawaida nishati hukaa karibu na uso, kwa hivyo inachukua muda zaidi. [1]

Pamoja na hii, maikrowevu linaruhusu kuchagua ukali wa mnururisho kwa vyakula tofauti. Chakula huwekwa ndani ya maikrowevu penye sahani inayozunguka ili mawimbi yaweze kupiga kila upande wa chakula. Maikrowevu huwa pia na saa inayozima kifaa baada ya dakika zilizopangwa.

Tahadhari

hariri

Matumizi yake yanahitaji uzoefu kidogo, ni vema kufuata maelekezo. Kuzidi kwa joto kunatokea haraka. Kama chakula kimefungwa ndani ya chombo kuna hatari ya moto kuwaka. Vyombo mbalimbali vya plastiki havifai kwa sababu vinaweza kuyeyuka.

Kama kiwango cha chakula ni kikubwa kidogo, inawezekana si pande zote cha chakula zinapokea joto kwa namna sawa; hasa kama chakula kimetolewa kwenye jokofu kilipoganda, inawezekana sehemu za nje ni joto sana lakini ndani yake mna sehemu ambazo bado ni baridi. Hapo inafaa kujenga maarifa kuhusu matumizi yake.

Metali kama chuma hutoa cheche katika maikrowevu badala ya kupashwa joto. Kwa hiyo vyombo vya metali havifai humo pamoja na karatasi ya alumini.

Marejeo

hariri
  1. "Teaching the world to ping", The Independent, Thursday 12 May 2011; Viewspaper p.16

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii kuhusu mambo ya teknolojia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hiyo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.