Miraa
Miraa (au mirungi) ni majani na vitawi ya mrungi, mti ulio na asili ya Pembe ya Afrika na Rasi ya Uarabuni. Majani machanga ya miraa hutafunwa na kutumika kama kichochezi cha mwili na akili. Moja ya madhara yake ni kupoteza hamu ya chakula.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeiweka miraa kwenye kundi la madawa ya kulevya. Kwa msingi huo, miraa huthibitiwa kwenye nchi mbalimbali kama vile Kanada, Ujerumani, Uingereza, na Marekani kumbe biashara na matumizi yake ni halali kwenye nchi za Jibuti, Kenya, Uganda, Ethiopia, Somalia na Yemeni.
Miraa hujulikana kwa majina mbalimbali yanayotokana na lile la Kiarabu Khat (قات, Catha edulis) kama vile qat na gat huko Yemeni, qaat na jaad nchini Somalia, na chat huko Ethiopia. Pia inajulikana kama jimaa kwa Kioromo, mairungu kwa Kikikuyu na mayirungi kwa Kiganda.
Majani mabichi hutafunwa na wakati mwingine hukaushwa na kutumiwa kama chai. Majani au sehemu nyembamba ya tawi huweza kutafunwa kwa karanga za kukaanga au gamu ili iwe rahisi kutafuna. Katika nchi nyingi ambako miraa inatumika, mara nyingi watumiaji wake ni wanaume.
Miraa imekuwa ikitumiwa kwa karne nyingi katika Pembe ya Afrika na Peninsula ya Uarabuni. Huko, kutafuna miraa kulianza hata kabla ya matumizi ya kahawa.
Miraa ni maarufu sana Yemeni ambapo kilimo chake hutumia rasilimali nyingi za kilimo. Inakadiriwa kuwa asilimia 40 ya maji ya nchi huelekea kumwagilia miraa na uzalishaji unaongezeka kwa asilimia 10 hadi 15 kila mwaka. Sababu moja kubwa ya kulimwa kwa miraa Yemeni ni mapato yanayotokana na zao hilo. Huko Uganda miraa hulimwa katika Mkoa wa Kati na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Magharibi. Nchini Kenya hulimwa katika eneo la Meru kwa ajili ya soko la Somalia.
Ingawa tabia ya kutafuna miraa iko zaidi katika nchi ilipotokea, mmea huo hulimwa pia katika nchi za Afrika Kusini, Msumbiji, na Eswatini.
Viungo vya Nje
haririMakala hii kuhusu mambo ya kemia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Miraa kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |