Mirerani
Mirerani ni kata ya Wilaya ya Simanjiro katika Mkoa wa Manyara, Tanzania.
Katika milima iliyo karibu na mji huo kuna migodi mingi ambako vito vilivyopendwa vya tanzanaiti kuchimbwa. Hata kama ni mahali pekee duniani ambako vito hivyo vinapatikana, bado Mirerani ni mahali pa umaskini bila dalili nyingi za maendeleo.[1]
Katika sensa ya mwaka 2022 wakazi wa kata walihesabiwa kuwa 21,250 [2]. Wakati wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 13,450 waishio humo. [3] lakini hali halisi idadi ya wakazi ni kubwa zaidi kutokana na uchimbaji na biashara ya vito vya [[tanzanaiti]].[4]
Uchimbaji wa madini
haririEneo ambako tanzanaiti inapatikana lina urefu wa kilomita 50 na upana wa kilomita mbili.[5] Tangu kugunduliwa kwa tanzanaiti mnamo mwaka 1967 kampuni ya serikali ya Tanzania Gemstone Industries (TGI) ilipewa haki pekee ya kuchimba vito Mirerani. TGI ilishindwa kuendesha kazi hiyo; ikaruhusu wachimbaji wadogo kuanzisha migodi pia kwa sharti la kwamba wauze vito vyote kwa kampuni. Lakini mapato yalikuwa duni mno, inaaminiwa kuwa sehemu kubwa ya vito haikuonyeshwa na kupelekwa nje ya nchi kwa siri. TGI ikatoka mnamo 1986 wakati serikali iliruhusu kampuni za kigeni kufanya shughuli nchini. Wachimbaji wadogo waliingia katika sehemu zilizowahi kumilikiwa na TGI.
Mwaka 1991 serikali iligawa eneo katika kanda nne zinazoitwa Block A, B, C na D. Wachimbaji wadogo walipewa block D, wafanyabiashara Watanzania walipewa block A na B. Block C ilitolewa kwa kampuni ya Graphtan, ushirikiano wa TGI na kampuni ya Uingereza. Graphtan walilenga si vito bali madini ya grafati (ing. graphite). Baada ya kushindwa kwa Graphtan, haki za kuchimba kwenye Block C ilinunuliwa kwanza na kampuni ya Afrika Kusini Mererani Mining Ltd iliyonunuliwa mwaka 2004 na kampuni ya TanzaniteOne ambayo ni kampuni ya kigeni ulioandikishwa kwenye visiwa vya Bahamas.
Leo hii TanzaniteOne inaendelea kuchimba vito katika mashimo ya migodi sita yenye kina cha mita 250 hadi 350. Kampuni ina wafanyakazi 560. Block B na D zinachimbwa na wachimbaji wadogo na kuna mashimo yapatao 700 [6]. Kampuni za Kilimanjaro Mining na Tanzanite Africa Ltd. zinachimba kwenye Block A na pia kando ya Block D: yote mawili ni makampuni ya Kitanzania.
Vito vya tanzanaiti vinapatikana chini ya ardhi katika mabonge hapa na pale; wachimbaji wanaweza kuendelea kwa siku au hata miezi bila kukuta kitu. Migodi pekee inayoendelea kutoa vito mfululizo ni ya TanzaniteOne.
Mara kwa mara kuna matatizo kati ya kampuni kubwa na wachimbaji wadogo ilhali kampuni inalalamika ya kwamba wachimbaji wadogo wanaingia ndani ya block C kupitia chini ya ardhi na kuvuna kwa siri[7]. Vivyo hivyo wachimbaji wazawa mara nyingi wanasikitika kuwepo kwa kampuni ya kigeni.
Marejeo
hariri- ↑ Tanzania: Mererani Still Has Nothing to Show for Its Resources, 7 September 2014 Tanzania Daily News (Dar es Salaam) , ilitazamiwa X-2015
- ↑ https://www.nbs.go.tz, uk 205
- ↑ Sensa ya 2012, Manyara Region – Simanjiro District-Council
- ↑ Linganisha Helliesen uk. 73: inakadiriwa ni angalau theluthi 1 ya wakazi wote wa Simanjiro hukaa Mererani na karibu.
- ↑ Tanzanite on the Mineral Database mindat.org
- ↑ Helliesen, uk 74
- ↑ Helliesen, uk 77
Viungo vya Nje
hariri- M. S. Helliesen, Tangled up in Blue: Tanzanite Mining and Conflict in Mererani, Tanzania, Critical African Studies, 4:7, 58-93, DOI:10.1080/21681392.2012.10597799, to link to this article: http://dx.doi.org/10.1080/21681392.2012.10597799, published online: 18 Dec 2012 Ilihifadhiwa 11 Agosti 2021 kwenye Wayback Machine.
Kata za Wilaya ya Simanjiro - Mkoa wa Manyara - Tanzania | ||
---|---|---|
Emboreet | Endiamutu | Endonyongijape | Kitwai | Komolo | Langai | Loiborsoit | Loiborsiret | Mirerani | Msitu wa Tembo | Naberera | Naisinyai | Ngorika | Oljoro No.5 | Orkesumet | Ruvu Remit | Shambarai | Terrat |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Manyara bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Mirerani kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
|