Galileo Galilei (5 Februari 15648 Januari 1642) alikuwa mtaalamu wa fizikia, hisabati na astronomia kutoka nchini Italia.

Galileo Galilei alivyochorwa.

Anakumbukwa kwa sababu aliweka misingi ya mbinu mpya za sayansi zinazoendelea kutumika hadi leo. Akiwa mtaalamu wa kwanza aliyetumia darubini kwa kutazama nyota na sayari na kwa njia hiyo alipanua ujuzi wa binadamu juu ya ulimwengu.

Ujana wake

Baba yake alikuwa mfanyabiashara aliyejishughulisha pia na masuala ya hisabati.

Galileo alisomeshwa kwenye shule ya monasteri akaendelea kusoma tiba mjini Firenze lakini akaacha masomo hayo akachukua hisabati badala yake.

Kanuni za anguko

Miaka 1589 - 1592 alipata nafasi kama profesa wa hisabati kwenye chuo kikuu cha Pisa. Hapo alifanya utafiti juu ya kanuni za anguko la magimba. Aliweza kuonyesha kwamba magimba yote huanguka kwa mkasi uleule yakianguka pasipo hewa kama ni makubwa au madogo. Kwa tamko hili alionekana kumpinga Aristoteles aliyepokewa na wataalamu na Kanisa kama msingi wa utaalamu wote.

Astronomia na darubini

 
Galileo alivyoonyesha miezi ya Mshtarii kwa viongozi wa Venisi

Alihamia chuo kikuu cha Padua alipofanya kazi kati ya 1592 na 1610. Alisikia kuhusu chombo kipya cha darubini (kionambali) kilichobuniwa na Mholanzi Hans Lipperhey akaiiga na kujenga ya kwake. Alikuwa kati ya watu wa kwanza waliotumia chombo hicho kwa kutazama mwezi, sayari na nyota. Aliona milima kwenye Mwezi. Pamoja na Mjerumani Simon Marius alikuwa mtu wa kwanza aliyeona miezi ya sayari Mshtarii na Galileo alikuwa mtu wa kwanza aliyeeleza utambuzi huu katika kitabu.

Vilevile aliweza kuangalia sayari Zuhura (pia Ng'andu, lat. Venus) jinsi ilivyoonyesha awamu sawa na Mwezi. Zilionekana kama mwezi mwandamo, nusu mwezi au mwezi mpevu. Alitazama pia madoa ya jua.

Mwaka 1610 mtawala wa Toscana, Cosimo II kutoka nasaba ya Medici, aliyewahi kuwa mwanafunzi wake, alimkaribisha kuwa mwanahisabati mkuu na pia profesa huko Pisa.

Alipendwa na watu wengi, pia na kardinali Maffeo Barberini aliyeendelea kufanya hivyo baada ya kuchaguliwa kuwa Papa Urban VIII.

Kesi ya Kanisa dhidi yake

 
Sanamu ya Galileo Galilei kwenye kaburi lake ndani ya Kanisa la Msalaba Mtakatifu mjini Firenze, Italia.

Matokeo ya utafiti wa Galilei yalipinga hoja ya awali iliyofundishwa na wataalamu wa Ugiriki ya Kale na kukubaliwa na wataalamu wa sayansi ya siku zile na pia katika Kanisa Katoliki. Kwa Galilei ilikuwa wazi ya kwamba dunia yetu si kitovu cha ulimwengu, tena aliamini jua ni kitovu chake na kwamba Nicolaus Copernicus pamoja na Johannes Kepler‎ waliwahi kusema ukweli.

Mwanzoni Papa Urban VIII (aliyefuatilia kwa karibu majadiliano ya wataalamu kuhusu elimu ya nyota) alimpa Galilei moyo wa kuandika kuhusu nadharia ya Koperniko, lakini alimwonya kutoionyesha kama ukweli bali kama nadharia mojawapo.

Katika majadiliano na wapinzani mbalimbali Galilei alisogea mbele na kutetea mfumo wa jua kuwa kitovu cha ulimwengu na kukosoa maoni ya kinyume. Sasa mafundisho ya Galilei yalipingwa kwa msingi wa mafundisho ya dini na sayansi. Wengine waliona yalipinga Biblia na imani. Wengine walifuata wataalamu kama Tycho Brahe walioona ya kwamba Galilei hakuweza kueleza vipimo vingi (jinsi vilivyowezekana wakati ule) na hivyo kukosa msingi wa kutangaza ukweli mpya.

Katika kesi mbele ya mahakama ya Kanisa alionywa asitangaze maoni yake mapya kuwa ukweli, badala yake alitakiwa kusema ni uwezekano tu. Sehemu ya vitabu vyake vilipigwa marufuku na mwenyewe aliambiwa kukaa ndani ya nyumba yake.

Mwaka 1992 Papa Yohane Paulo II alisema hivi kuhusu kesi dhidi ya Galilei: « Kama wapinzani wake walio wengi, Galileo hakutofautisha mtazamo wa sayansi kuhusu mambo ya kimaumbile na fikra za kifalsafa juu ya maumbile ambazo kwa kawaida zinadaiwa nao. Ndiyo sababu alikataa pendekezo alilopewa la kuita 'dhana' mafundisho ya Kopernicus, hadi yathibitishwe moja kwa moja, ingawa hilo lilikuwa sharti la mbinu ya majaribio aliyoibuni mwenyewe kwa akili kubwa. [...] Kumbe, suala walilojiuliza wanateolojia wa wakati huo lilikuwa lile la ulinganifu wa mafundisho ya jua kuwa kiini cha ulimwengu na Maandiko Matakatifu. Hivyo sayansi mpya, kwa mbinu zake na uhuru wa ukufanya utafiti unaodaiwa nazo, ililazimisha wanateolojia kujiuliza juu ya vigezo vyao vya kufafanulia Maandiko. Wengi wao wakashindwa kufanya hivyo. Ajabu, Galileo, mwamini mnyofu, alijitokeza anaelewa kuliko wanateolojia waliompinga kuhusu jambo hilo. » (Yohane Paulo II kwa wanasayansi wa Akademia ya Kipapa ya Sayansi, 31 Oktoba 1992)

Viungo vya nje

 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Jua habari zaidi kuhusu Galileo Galilei kwa kutafuta kupitia mradi wa Wikipedia Sister
  Uchambuzi wa kamusi kutoka Wikamusi
  Vitabu kutoka Wikitabu
  Dondoo kutoka Wikidondoa
  Matini za vyanzo kutoka Wikichanzo
  Picha na media kutoka Commons
  Habari kutoka Wikihabari
  Vyanzo vya elimu kutoka Wikichuo

Maandiko ya Galileo

Kuhusu Galileo

Maisha yake

  • Galileo by Bryant, Walter W. (Walter William), Published 1918
  • The Private Life Of Galileo. Compiled principally from his correspondence and that of his eldest daughter, Sister Maria Celeste
  • PBS Nova Online: Galileo's Battle for the Heavens
  • Stanford Encyclopedia of Philosophy entry on Galileo
  • Animated Hero Classics: Galileo (1997) at the Internet Movie Database
  • O'Connor, John J.; Robertson, Edmund F., "Galileo Galilei", MacTutor History of Mathematics archive, University of St Andrews.

Galileo na Kanisa