Mtaguso wa Kalsedonia

Mtaguso wa Kalsedonia (kwa Kiingereza: Council of Chalcedon) unahesabiwa na Wakristo wengi kuwa wa nne kati ya mitaguso ya kiekumene katika historia ya Kanisa.

Mtaguso wa Kalsedonia.

Ulifanyika Kalsedonia (leo Kadıköy, sehemu ya jiji la Istanbul, Uturuki upande wa Asia) mwaka 451.

Historia

hariri

Mtaguso huo uliitishwa na Kaisari Marcianus wa Dola la Roma Mashariki pamoja na mke wake Pulkeria wa Konstantinopoli miaka 20 baada ya Mtaguso wa Efeso.

Hao waliona haja ya kudumisha umoja wa Wakristo, uliokuwa msingi wa uimara wa dola hilo, hasa wakati huo ambapo makabila yasiyo na ustaarabu kutoka Asia yalikuwa yanajaribu kuteka Ulaya.

Umoja huo uliingia hatari ya kuvunjika kutokana na uamuzi wa mtaguso mkuu wa Efeso kuhusu imani sahihi juu ya Yesu Kristo kutoeleweka kwa namna moja.

Hasa baadhi ya walioshinda mtaguso huo walionekana kusisitiza mno umungu wake hata kutia shaka kama wanaamini sawasawa ubinadamu wake pia.

Vikao vilianza tarehe 8 Oktoba 451 vikiwa na washiriki zaidi ya 350: mara nyingi inatajwa idadi ya 600 hivi. Hatimaye mafundisho ya Eutike na Dioskoro wa Aleksandria yalilaaniwa.

Ufanisi wa mtaguso ulichangiwa na msimamo wa kaisari Valentiniano III wa Dola la Roma Magharibi, binamu wa Pulkeria. Kaisari huyo alimuunga mkono Papa Leo I (440-461) aliyekuwa ametoa msimamo wake na wa Kanisa la Roma tangu mwaka 449 katika Tomus ad Flavianum, yaani Waraka kwa Flaviano, Patriarki wa Konstantinopoli aliyeuawa na wafuasi wa Eutike.

Ingawa msimamo huo wa kati ulikubaliwa na wengi, wengine waliuona ni kinyume cha uamuzi uliotolewa Efeso, hivyo walishikilia sana mtazamo huo hata walipodhulumiwa na serikali. Ndiyo asili ya farakano la Misri, Syria, Armenia n.k. linalodumu hata leo.

Mtaguso huo ulitunga pia kanuni mbalimbali, kama vile kwa kumpatia Patriarki wa Konstantinopoli nafasi ya pili kati ya maaskofu wote[1].

Mtaguso huo unajulikana sana kwa kile ulichokubaliana kuhusu Yesu.

Kwa hiyo, tukiwafuata mababa watakatifu, sisi sote tunawafundisha watu kwa nia moja kumkiri Mwana mmoja na yuleyule, Bwana wetu Yesu Kristo, kwa wakati mmoja Mungu kabisa na binadamu kabisa, Mungu kweli na mwanadamu kweli, akijumuisha pia roho/nafsi yenye usawaziko (Kigiriki cha kale: ψυχῆς λογικῆς, Kiingereza: of reasonable soul) na mwili; ana Uungu wa Baba, na wakati huohuo ni kitu kimoja nasi kuhusu uanaume wake; kama sisi katika mambo yote, bila dhambi; kuhusu Uungu wake, yu Mwana kabla ya zamani zote [au aliyezaliwa na Baba kabla ya zamani zote, Kigiriki cha kale: πρὸ αἰώνων μὲν ἐκ τοῦ Πατρὸς γεννηθέντα κατὰ τὴν θεότητα, Kiingereza: as regards his Godhead, begotten of the Father before the ages), lakini bado kuhusu utu wake, kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu, wa Maria Bikira, Mama wa Mungu [Kigiriki cha kale θεοτόκου, Kiingereza: God-bearer); Kristo yuleyule, Mwana, Bwana, Mzaliwa Pekee, anayetambuliwa kama Mungu kabisa na binadamu kabisa [Kigiriki cha kale: ἐν δύο φύσεσιν ἀσυγχύτως, Kiingereza: recognised in two natures], bila mchanganyiko, bila badiliko, bila mgawanyiko, bila utengano; tofauti bila kubatilishwa kwa njia yoyote na muungano, bali sifa za uungu na ubinadamu zikihifadhiwa na kuja pamoja na kuunda nafsi moja na kitu kimoja [Kiingereza: coming together to form one person and subsistence, Kigiriki cha kale:  καὶ εἰς ἓν πρόσωπον καὶ μίαν ὑπόστασιν συντρεχούσης], si kama kugawanywa katika nafsi mbili, bali Mwana mmoja na yuleyule na Mungu Mzaliwa-pekee, Neno, Bwana Yesu Kristo; kama vile manabii wa kale walivyonena juu yake, na Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe alitufundisha, na kanuni ya imani ya baba zetu imetukabidhi sisi. [2]

Tanbihi

hariri
  1. All popes since Leo the Great had adamantly rejected the 28th canon of the Council of Chalcedon, which on the basis of political considerations tried to raise the ecclesiastical status of the Patriarchate of Constantinople to equality with that of old Rome. Cfr. Davis, Leo Donald, The First Seven Ecumenical Councils (325–787), (Collegeville: Liturgical Press, 1990) p. 194
  2. "Chalcedonian Definition". earlychurchtexts.com. Iliwekwa mnamo 2023-02-07.

Marejeo

hariri
  • The Ecclesiastical History of Evagrius: A History of the Church from AD 431 to AD 594, transl. Edward Walford, 1846.
  • Charles Joseph Hefele, A History of the Councils of the Church from the Original Documents. 5 voll. (in part. vol. III) Edinburgh 1883
  • John Meyendorff, Christ in Eastern Christian Thought, Washington D.C. 1969
  • R.V. Sellers, Two Ancient Christologies, London 1940
  • R.V. Sellers, The Council of Chalcedon: A Historical and Doctrinal Survey, London 1961

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mtaguso wa Kalsedonia kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.