Oreste Baratieri
Oreste Baratieri (Condino 13 Novemba 1841 – Vipiteno 7 Agosti 1901) alikuwa mbunge wa Italia, jenerali wa jeshi na gavana wa koloni la Eritrea aliyeongoza Waitalia katika mapigano ya Adowa waliposhindwa vibaya na Ethiopia.
Maisha
haririBaratieri alikuwa mwenyeji wa jimbo la Tirol, sehemu ya Dola la Austria-Hungaria, leo upande wa kaskazini wa Italia. Ubini wake asili ulikuwa wa Kijerumani, Baratter, lakini aliubadilisha.
Alishiriki katika mapigano ya vita vya maungano ya Italia chini ya Giuseppe Garibaldi miaka ya 1860 na 1861.
Mwaka 1891 alipewa cheo cha jenerali na kuwa mkuu wa jeshi la Italia katika Eritrea. Mwaka 1892 alipata kuwa pia gavana.
Baratieri aliongoza wanajeshi wake katika ushindi wa mapigano mbalimbali dhidi ya vikosi vya watemi na makabila ya Ethiopia.
Mwaka 1895 alipokea amri za serikali yake ya kushambulia Ethiopia baada ya Negus Menelik II kukana mkataba wa Wuchale.
Hapo Baratieri alitembelea Italia na kuwahutubia wananchi akiwaahidia atamleta Menelik kama mfungwa.
Mnamo Oktoba 1895 Baratieri alivuka mto Mareb na kuingia Ethiopia. Baada ya mapigano ya kwanza alijifunza kuhusu jeshi kubwa la Menelik, akaamua kusubiri hadi akiba za chakula cha Waethiopia ziishe. Lakini serikali ya waziri mkuu Francesco Crispi ilitaka kutangaza mapema ushindi, ili kunyamazisha upinzani wa ndani, hivyo iliamua kumtuma jenerali Baldissera kushika nafasi ya Baratieri.
Shinikizo hilo lilisababisha Baratieri ashambulie mara moja, ila katika mapigano ya Adowa wanajeshi 17,000 Waitalia na Waeritrea walipigwa vibaya na jeshi la Menelik, lenye wanajeshi kati 80,000 hadi 100,000. Waitalia walipoteza wanajeshi 10,000 waliokufa au kutekwa wafungwa na adui, pamoja na mizinga yote na bunduki 11,000. Wengine waliweza kukimbia na kujiokoa kwenda Eritrea.
Baratieri aliweza kujiokoa lakini alisimamishwa mbele ya mahakama ya kijeshi iliyoona ya kwamba alifanya makosa lakini hana hatia. Mwaka 1897 alijiondoa madarakani na kuchukua pensheni yake.
Aliishi katika Tirol ya Kiaustria alipoaga dunia tarehe 7 Agosti 1901 mjini Sterzing-Vipiteno.