Mapigano ya Adowa yalitokea tarehe 1 Machi 1896 katika nyanda za juu za Tigray kati ya jeshi la Italia kwa upande mmoja na la Ethiopia kwa upande mwingine. Waethiopia walishinda na kuhakikisha uhuru wa nchi yao hivyo kufanya Ethiopia nchi ya pekee ya Afrika iliyofaulu kuzuia ukoloni[1].

Picha ya Kiethiopia inayoonyesha mapigano ya Adowa
Negus Menelik II kwenye mapigano ya Adowa - mchoro katika gazeti la Kifaransa Le Petit Journal.
Taswira ya Kiethiopia kuhusu Adowa; inaonyesha mizinga ya Waethiopia na bombomu ya Waitalia
Gazeti la Kifaransa "La Vie Illustree" linaloonyesha sherehe ya mwaka 1904 ya kukumbuka ushindi wa Adowa na wanajeshi Waethiopia kwenye maandamano.

Utangulizi

Mwaka 1889 mtemi wa Shewa Menelik II alijitangaza Negus wa Ethiopia baada ya kushinda mapigano kati ya watemi wa Ethiopia yaliyofuata kifo cha Negus aliyemtangulia Yohane IV. Katika hilo Menelik alisaidiwa na Waitalia ambao walikuwa wameshika Eritrea tayari.

Mnamo Mei 1889 Menelik alifanya mkataba wa Wuchale alimokubali utawala wa Italia juu ya kanda ya pwani pamoja na maeneo kadhaa ya nyanda za juu za Tigray yakiwemo mazingira ya Asmara ya leo.

Italia ilidai, kutokana na nakala ya Kiitalia ya mkataba huo, haki ya ulinzi juu ya Ethiopia. Nakala ya Kiethiopia haikuonyesha vipengele kuhusu ulinzi wa Italia juu ya ufalme wa Ethiopia. Menelik aliimarisha utawala wake na mwaka 1893 alikana mkataba[2].

Italia inavamia Ethiopia

Italia ilijibu kwa kuvamia Ethiopia kwa jeshi kubwa mnamo Oktoba 1895. Menelik aliweza kukusanya takriban wanajeshi 100,000 na kuwaongoza hadi Tigray (jimbo jirani na Eritrea).

Mapigano ya kwanza ndani ya Tigray ya Amba Alagi (7 Desemba) na ya Mekelle hayakuenda vizuri kwa Waitalia. Waethiopia walishindwa kuteka boma la Mekelle, lakini Waitalia walifungwa ndani kwa wiki tatu. Mwishowe waliondoka baada ya mapatano na Negus Menelik II na kurudi Eritrea.

Sehemu kubwa ya jeshi la Italia haikuingia bado katika mapigano. Gavana jenerali Oreste Baratieri alikataa kuwashambulia Waethiopia baada ya kujua idadi yao kubwa. Lakini alijua ya kwamba Menelik hataweza kulisha askari wengi hivi kwa muda mrefu katika milima ya Tigray, akataka kusibiri hadi jeshi la Negus litakapoanza kusikia njaa na kupungua.

Lakini serikali ya Roma ya waziri mkuu Francesco Crispi, baada ya kupokea habari za mapigano ya kwanza, iliona aibu ya kushindwa na Waafrika ikamwamuru gavana ashambulie mara moja.

Adowa

Baratieri aliongoza jeshi lake la vikosi vinne katika milima ya Tigray.

Jeshi lake lilikuwa na vikosi vitatu vya Waitalia na kikosi kimoja cha askari kutoka Eritrea. Jumla ya wanajeshi ilikuwa 17,700 (Waitalia 10,596 na askari Waeritrea 7,104) pamoja na na mizinga 65[3]. Hii ilikuwa nusu ya Waitalia wote waliopatikana katika Eritrea.

Baratieri alijua ya kwamba kulikuwako kambi kubwa ya Waethiopia karibu na mji wa Adowa, alitaka kuwashambulia asubuhi wakati wa kucha kabla hawajaamka[4]. Lakini vikosi vyake vilipotea njia gizani: waliposogea mbele usiku hawakufika kwa utaratibu mzuri mahali walipokutana na jeshi la Negus.

Jeshi la Menelik lilikuwa la wanajeshi 80,000 hadi 100,000. Wengi wao walikuwa na bunduki zilizonunuliwa katika miaka iliyotangulia na Menelik kutoka kwa wafanyabiashara Waitalia[5].

Wakati wa asubuhi wa tarehe 1 Machi 1886 kikosi cha kwanza cha askari Waeritrea chini ya maafisa Waitalia kiligonga moja kwa moja kambi la Ras Alula aliyekuwa tayari. Makelele yaliamsha Waethiopia wote waliochukua haraka nafasi zao juu ya milima wakiwashambulia Waitalia waliosogea mbele bondeni.

Baada ya masaa sita mapigano yalikwisha. Waitalia walishindwa, wengi kuuawa na wengine walikimbia wakirudi Eritrea. Wanajeshi wao 7,000 waliuawa na 1,500 kujeruhiwa, 3,000 wakawa wafungwa, kati yao jenerali mmoja. Waethiopa walipoteza watu 4,000 - 5,000 na 8,000 kujeruhiwa[6]. Waitalia walipaswa kuacha nyuma mizinga yote, bunduki 11,000 na vifaa vingi.

Menelik hakuwafuata Waitalia ndani ya Eritrea. Sababu hazieleweki waziwazi lakini wataalamu hutaja sababu mbalimbali[7]:

  • Menelik alijua hata kama angewafukuzwa Waitalia wote katika Eritrea angejiweka katika hatari ya kuletwa kwa jeshi lote la Italia dhidi yake, kwa sababu Italia ingejaribu kuondoa aibu. Alijua ya kwamba asingeweza kushinda vita kamili dhidi ya nchi iliyoendelea.
  • Menelik alikuwa ameandaa kuvunja jeshi kabla ya mapigano juu ya upungufu wa vyakula Tigray na kutokana na idadi kubwa ya wanajeshi wake kuwa wenyeji wa sehemu zingine. Pia Menelik aliona vigumu kulisha jeshi kubwa kiasi hicho.
  • Menelik alikumbuka mkataba wake wa kwanza alimokubali utawala wa Italia katika Eritrea.

Baada ya mapigano

Waethiopia waliwatendea wafungwa Wazungu vizuri lakini walikata askari wafungwa Waeritrea 800 mkono na mguu wa kuume.

Baada ya habari hizi kufika Italia serikali ya Crispi ilipinduliwa. Serikali mpya ilipaswa kukubali uhuru wa Ethiopia katika mkataba wa amani tarehe 26 Oktoba 1896. Ethiopia ilikubali mamlaka ya Italia juu ya koloni lake katika kaskazini. Wafungwa walirudishwa[8].

Ushindi wa Menelik ulihakikisha uhuru wa Ethiopia kama nchi pekee pamoja na Liberia isiyowekwa chini ya ukoloni wa Ulaya katika bara la Afrika.

Tanbihi

  1. "5 Fascinating Battles of the African Colonial Era". Encyclopaedia Britannica. https://www.britannica.com/list/5-fascinating-battles-of-the-african-colonial-era. Retrieved 14 June 2020.
  2. Piero Pastoretto. Battaglia di Adua (it). Jalada kutoka ya awali juu ya 2006-05-31. Iliwekwa mnamo 2021-12-02.
  3. * Lewis, D.L. (1988) ''The Race to Fashoda: European Colonialism and African Resistance in the Scramble for Africa'', 1st ed., London: Bloomsbury, uk. 116f.
  4. Harold G. Marcus, The Life and Times of Menelik II: Ethiopia 1844–1913, 1975 (Lawrenceville: Red Sea Press, 1995), uk. 170.
  5. * Pankhurst, K.P. (1998) The Ethiopians: A History, The Peoples of Africa Series, Oxford: Blackwell Publishers, uk. 190f
  6. Pankhurst. The Ethiopians, uk. 191–92.
  7. Lewis, Fashoda, uk. 120.
  8. Margery Perham, The Government of Ethiopia, second edition (London: Faber and Faber, 1969), uk. 58f;