Rosetta (kipimaanga)

(Elekezwa kutoka Rosetta (chombo cha angani))

Rosetta ni kipimaanga cha Mamlaka ya Ulaya ya Usafiri wa Anga. Mwaka 2004 Kilirushwa kutoka kituo cha angani Kourou kwa roketi ya Ariane 5 kwa kusudi la kufikia nyotamkia ya 67P/Churyumov–Gerasimenko.

Rosetta
Njia ya Rosetta hadi kufikia nyotamkia 67P/Churyumov-Gerasimenko. Njia za Rosetta (nyeusi), Dunia (kijani), Mirihi (nyekundu), Mshtarii (kahawia) na 67P/Churyumov-Gerasimenko (buluu). Karibu na na. 9 chombo kilifikia njia ya nyotamkia, kwenye na. 10 kilianza kuzunguka lengo, kwenye na. 11 lander Philae ilishuka juu ya uso wa nyotamkia.

Teknolojia hariri

Ilhali hakuna roketi bao yenye nguvu ya kufikisha chombo moja kwa moja hadi nyotamkia, Rosetta ilitumia njia ya kuzunguka mara kadhaa Dunia yetu na sayari ya Mirihi kwa kusudi la kuongeza mwendo wake kwa msaada wa graviti ya sayari hizi.

Rosetta inapata nguvu yake kwa kutumia seli za umemenuru. Ilhali nuru ya jua inapungua sana nje ya njia ya Mirihi, chombo kiliingia katika kipindi kirefu cha usingizi wa miezi 31 kwa kusudi la kutunza nishati ya betri zake hadi kukaribia lengo lake. Tarehe 20 Januari 2014 chombo kiliamka tena wakati wa kukaribia nyotamkia.

Kufikia nyotamkia hariri

Mwezi wa Agosti 2014 ilifika ikaanza kuzunguka nyotamkia hiyo. Mwezi wa Novemba 2014 ilirusha lander yake Philae ambayo ilishuka kwenye uso wa nyotamkia tarehe 11 Novemba 2014 ikiwa mara ya kwanza ya chombo kilichotengenezwa na binadamu kufikia kwenye nyotamkia yoyote.

Mwisho hariri

Tarehe 30 Septemba 2016 mnamo saa nane na nusu mchana (saa 13:19 h wakati wa Afrika ya Mashariki) shughuli za Rosetta zilifikia mwisho ilhali chombo hiki kiligonga uso wa nyotamkia 67P.

Viongozi wa mradi wake waliamua kumaliza kazi yake kwa njia hiyo kwa sababu chombo kilifuatana na nyotamkia kwenye njia yake kuelekea ng'ambo ya mzingo wa sayari ya Mshtarii ambako nuru ya jua haitoshelezi tena mahitaji ya nishati ya chombo.

Hivyo mabaki ya umeme katika betri yalitumiwa kuwasha injini mara ya mwisho na kukilenga chombo kwenda usoni mwa nyotamkia na kutumia safari hii ya mwisho kuchukua tena picha za karibu na kuzituma duniani.

Viungo vya Nje hariri