Utitiri-utando madoa-mawili

(Elekezwa kutoka Tetranychus urticae)
Utitiri-utando madoa-mawili
Utitiri-utando madoa-mawili
Utitiri-utando madoa-mawili
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia
Faila: Arthropoda
Nusufaila: Chelicerata
Ngeli: Arachnida
Nusungeli: Acari
Oda: Trombidiformes
Familia: Tetranychidae
Jenasi: Tetranychus
Dufour, 1832
Spishi: T. urticae
Koch, 1835

Utitiri-utando madoa-mawili (Tetranychus urticae) ni utitiri wa familia Tetranychidae katika oda Trombidiformes aliye msumbufu mbaya katika mashamba na vibanda vya kukuzia mazao. Anashambulia spishi zaidi ya 1000 za mimea na kwa hivyo ni moja baini ya spishi zinazojilisha kwa mimea mingi zaidi kulingana na spishi nyingine.

Kwa asili spishi hii ilitokea Ulaya na sehemu za Asia lakini siku hizi imevamia takriban nchi zote duniani, isipokuwa si kawaida sana katika nchi za tropiki.

Maelezo

hariri

Hao ni matitiri wadogo na urefu wa majike ni mm 0.4-0.5 na wa madume ni mm 0.4. Rangi ya hatua zote ni njano-kijani na kuna mabaka meusi kila upande wa mwili. Mgongo una jozi 12 za manyoya na makunyanzi ya mgongo yanaunda pembe na urefu. Kizazi kitakachopita msimu wa baridi katika diapause hubadilisha rangi kwa nyekundu-machungwa.

Kwenye mahali fulani ambapo msimu wa baridi sio kali sana kuna matitiri wenye rangi ya nyekundu iliyoiva (“utitiri-utando mwekundu-kolevu”) na hao hawaingii kwa diapause.

Majike wanaweza kutaga mayai zaidi yai 100. Matitiri hao wanahitaji nyuzijoto ya juu ya 10ºC ili kukua. Kwa 25-30ºC hupitia hatua zote za maisha yao katika muda wa wiki mbili. Baada ya yai kuna hatua moja ya lava na hatua mbili za tunutu (protonymph na w:deutonymphdeutonymph) na mwishowe mpevu. Mayai yasiyotungwa ya matitiri-utando hutoa madume na mayai yaliyotungwa hutoa majike (arrhenotoky).

Mimea vidusiwa

hariri

Matitiri hao hujilisha kwa mimea ya spishi nyingi sana, zaidi ya 1000. Wanapenda miharagwe na mimea mingine ya familia Fabaceae sana. Mazao yanayoshambuliwa ni pamoja na mpilipili, nyanya, kiazi, mtango-tamu, mharagwe, muhindi na stroberi. Maua ya mapambo kama miwaridi hushambuliwa pia. Zamani matitiri-utando walikuwa wasumbufu sana katika vibanda vya kukuzia mazao, lakini siku hizi kuna mibinu mizuri ya uthibiti.

Kwa kawaida matitiri wako kwenye upande wa chini wa majani, lakini utando wao unaweza kufunika mmea mzima. Wanaweza kutawanywa na upepo, maji ya umwagiliaji na wafanyakazi (juu ya mavazi na vyombo) na kwa mbali kubwa kwa njia ya biashara ya mimea.

Udhibiti

hariri

Aina fulani za mazao, haswa za nyanya, zinapinga mashambulio kwa sababu ya nywele fupi kwenye majani na shina. Kupogoa na kuweka mashina kwenye waya hufanya iwe rahisi zaidi kudhibiti matitiri.

Dawa nyingi za kikemikali hazina ufanisi sana dhidi ya matitiri-utando. Pirethroidi zimekuwa na ufanisi lakini sasa zinapoteza ufanisi wao. Ufanisi wa bidhaa za mwarobaini na sulfidi ya kalisi bado ni ya kuridhisha. Walakini, siku hizi, udhibiti wa kibiolojia unazidi kupata umuhimu. Njia ya chaguo katika vibanda vya kukuzia mazao ni matumizi ya matitiri-mbuai, kama Phytoseiulus persimilis na Amblyseius andersoni. Katika mashamba ya nje dawa za kibiolojia zinaweza kutumika, kama vile dawa zilizo na kuvu Metarhizium anisopliae au Beauveria bassiana ndani yao.