Virusi vya kompyuta

Aina ya programu ya kompyuta ambayo, inapotekelezwa, inajirudia yenyewe kwa kubadilisha programu nyingine za kompyuta na kuingiza msimbo wake mwenyewe.
(Elekezwa kutoka Virusi za kompyuta)

Virusi vya kompyuta (kwa Kiingereza: computer virus) ni programu haramu yenye uwezo wa kujisambaza ndani ya kompyuta na kujiingiza ndani ya programu halali zinazotakiwa kufanya kazi mle. Ikisambaa inaathiri programu halali na kusababisha hasara. Virusi vinasambaa kwa njia ya intaneti lakini pia kwa njia ya sidii au diski yoyote ya kubebea data kati ya kompyuta tofauti. Virusi vinaweza kuharibu mafaili na kupunguza uwezo na kasi wa ufanyaji kazi wa kompyuta.

Worm aina ya Blaster ilitumika kutuma ujumbe huu kwa mwanzilishi wa kampuni ya Microsoft, Bill Gates.

Jina

Jina la virusi linatokana na neno la Kilatini "virus" linalomaanisha kiasili "sumu"[1]. Kwa kawaida hutumiwa kwa vyembe vidogo vinavyoundwa na maada jenetiki vyenye uwezo vya kujiingiza katika seli za mwili ambako zinasambaa na mara nyingi kusababisha magonjwa. Matumizi ya jina hili kwa programu haribifu za kompyuta hurejelea namna yake ya kusambaa na kusababisha uharibifu.

Historia

Programu za virusi zilianzishwa tangu mwanzo wa kompyuta zenyewe. Wanahisabati maarufu kama John von Neumann walikadiria nadharia ya programu zenye uwezo wa kujiendeleza na hata kujisambaza peke yake tangu miaka ya 1950.

Tangu kupatikana kwa kompyuta ndogo za nyumbani, imeonekana ya kwamba programu za aina hiyo zinaweza kuleta hasara mbalimbali. Mara nyingi programu (c) Brain hutajwa kama kirusi cha kwanza kilichosambaa kwenye kompyuta ndogo tangu mwaka 1986. Usambazaji wake ulikuwa kosa la watungaji wake waliotaka kukinga diski za programu halali waliyouza dhidi ya nakala haramu; waliandika namba ya simu yao ndani ya virusi.

Tangu kupatikana kwa intaneti kuna maelfu ya watu ambao wametunga programu za virusi kwa kusudi mbalimbali; mara nyingi ni vijana wanaotaka kujaribu uwezo wao wa kuandika programu za aina hiyo. Wengine wanakusudia mzaha tu wakitaka kuona mafanikio yao kwenye kompyuta za dunia yote. Kuna wengine wenye hasira dhidi ya kampuni kubwa kama Microsoft, dhidi ya benki, dhidi ya serikali au dhidi ya binadamu kwa jumla. Hao ni hatari zaidi wakijitahidi kusababisha hasara kubwa. Wengine hufuata kusudi za kisiasa wakilenga kompyuta za lugha au nchi fulani hasa. Virusi vingi vina malengo ya kijinai kwa sababu watungaji wao wanajaribu kupata faida ya kifedha kwa njia ya utapeli wakijaribu kuiba maneno ya siri kutoka kompyuta ya watu yanayomruhusu mtumiaji kuwasiliana na benki na kutuma fedha kwa akaunti nyingine.

Hatari za kutumia kompyuta nyingi

Mtandao wa intaneti unaruhusu mamilioni ya watumiaji wa kompyuta duniani kuungana pamoja kwa biashara na hata kwa kujifurahisha. Watu wengi tofauti hutumia intaneti. Yeyote anayetumia intaneti anaweza kupata habari nyingi kuhusu mada tofauti, tena kwa lugha tofauti, yaani, katika kipindi kidogo sana.

Intaneti inawezesha mtu mmoja kuharibu au kupunguza uwezo wa mamilioni ya kompyuta ambazo zimeunganishwa nazo. Wanaweza kufanya hivi kwa kuandika program za kompyuta. Au, wanaweza kuzifanya kompyuta zijiweke taarifa za kipuuzi ambazo zinasabisha kompyuta iache kufanya kazi. Iwapo sio mwangalifu, basi unaweza kusababisha kompyuta iache kufanya kazi.

Hasara kubwa zilizosababishwa na "worm"

Tarehe 24 Januari 2003, aina ya virusi cha kompyuta iitwacho "worm" ilitolewa ili kuathiri Intaneti. Worm ni mfululizo wa maelekezo ya kompyuta ambayo yanajiweka nakala nyinginyingi na kuzituma kwa kompyuta nyingine.

Hiyo worm imetuma nakala kibao zake yenyewe kwenye kompyuta nyingine kupitia Intaneti. Hiyo worm imeharibu milioni kadhaa za kompyuta duniani. Imepunguza uwezo wa kompyuta kibao kupitia mitandao ya kompyuta.

Kampuni za kupiga vita virusi

Sophos P-L-C ni kampuni ya kompyuta ya huko Uingereza ambayo inatengeneza programu za kuilinda kompyuta dhidi ya virusi. Hii ni kampuni ya nne kwa ukubwa ya kutengeneza program za kuzuia virusi.

Hivi karibuni, kampuni ya Sophos imetangaza onyo rasmi watumiaji wa kompyuta kujikinga dhidi virusi vipya vingi na worms. Tangazo lilitoa maelezo juu ya baadhi ya watu wanaofanya kazi kwa juhudi kutengeneza bidhaa pepe haramu za kompyuta. Kampuni ya Sophos ilisema ya kwamba hizi ni ripoti kutoka katika gazeti lililochapishwa nchini Singapore mnamo 14 Januari, siku tu kabla ya shambulio la worm lililofanywa katika Slammer.

Graham Cluley ni mtalaamu wa kompyuta katika kampuni ya Sophos. Alisema kwamba kampuni za utengenezaji wa programu za kulinda kmpyuta zinategemea virusi vingi kwa mwaka huu. Alisema watunzi wa virusi wanataka kubuni virusi vingine vyenye nguvu kupita hata hivi vya worm. Hii itaweza kusambazwa kupitia ujumbe elektronikia au njia ya mawasiliano ya kompyuta iitwayo Instant Messaging (Ujumbe wa Haraka kama vile Yahoo Messenger, Google Talk, Windows Live Messenger, na kadhalika). Bwana Cluley aliendelea kusema kwamba aina hii ya virusi husababisha matatizo makubwa sana.

Wataalamu wa kompyuta wa Kampuni ya Sophos walisema kuna virusi vya kompyuta takriban 40,000 ambavyo kwa sasa vinafahamika kama vipo. Wataalamui hao waliendelea kusema kwamba takriban virusi vipya 200 hutolewa kila mwezi kupitia tovuti.

Bwana Cluley alisema miaka kumi au tisa iliyopita kompyuta nyingi zilizoharibiwa na virusi ni zile ambazo zinatumia Microsoft Windows kama ndiyo mfumo wake wa uendeshaji, yaani, operating system.

Marejeo

  1. Matumizi yangeweza kuwa sawa na maneno mengine ya asili ya Kilatini yaliyofika kwenye Kiswahili kupitia Kiingereza kama vile "video" na "viza" (kibali cha kuingia nchini) ambayo hayamaanishi wingi. Hata hivyo wasemaji wengi wa Kiswahili husikia ni neno la ngeli ya ki-,vi- wakipenda kutumia lugha ya "virusi vya, virusi vingi".

Viungo vya nje