Vita kati ya Irak na Uajemi
Vita kati ya Irak na Uajemi ilitokea kuanzia Septemba 1980 hadi Agosti 1988. Ilipigwa kati ya majeshi ya nchi jirani za Irak na Uajemi (Iran) ikisababisha vifo vya watu milioni moja na kwisha bila mshindi. Iliitwa pia "Vita ya ghuba" kutokana na ghuba ya Uajemi ambayo nchi zote mbili zinapakana nayo; baadaye iliitwa pia "vita ya kwanza ya ghuba" kutokana na vita za Marekani dhidi ya Irak zilizofuata.
Vita ilianza kwa mashambulio ya Irak dhidi ya Uajemi. Dikteta Saddam Hussein wa Irak alitaka kutumia nafasi ya kudhoofishwa kwa jeshi la Uajemi baada ya mapinduzi ya mwaka 1979. Mwaka ule serikali ya shah wa Uajemi ilipinduliwa na harakati iliyoongozwa na kiongozi Mwislamu Ruhollah Khomeini na maafisa wengi wa jeshi la shah ama waliuawa ama walikimbia nchi. Saddam Hussein alilenga kushika utawala juu ya Shat al Arab ambayo ni mdomo wa mito Frati na Hidekeli kwenye ghuba ambako mizigo ya mafuta ya petroli ya Irak inapaswa kupita ikiuzwa nje. Alilenga pia kutwaa sehemu za Uajemi zilizokuwa na wasemaji wa lugha ya Kiarabu na sehemu hizo zinaitwa Khuzistan; Saddam alidai ya kwamba ilikuwa eneo la kihistoria ya Irak iliyotekwa na Uajemi.
Mwanzoni Wairaki walifaulu kuteka maeneo karibu na mpakani upande wa Uajemi lakini serikali mpya ya Kiislamu iliweza kutuma wanamgambo hasa vijana wengi ambao walikuwa tayari kufa hata kama hawakufundishwa kazi ya askari. Mtindo huo ulirudisha Wairaki nyuma lakini ulikuwa pia sababu ya kwamba Waajemi wengi walikufa kushinda Wairaki. Ila tu Uajemi ni nchi yenye watu wengi zaidi na Waajemi wengi walikuwa tayari kwa kifo kwa sababu waliona ya kwamba nchi yao ilishambuliwa. Viongozi wa kidini walitangaza ya kwamba ulikuwa wajibu wa kidini kushika silaha.
Nchi za nje kama Marekani zilihofia mapinduzi ya Kiislamu zikasaidia Irak kwa silaha na habari kama picha kutoka vyombo vya angani. Vita hii ilikuwa maarufu kwa sababu Irak ilitumia silaha marufuku kama gesi ya sumu.
Vita iliendelea ingawa Umoja wa Mataifa ilisihi pande zote mbili kumaliza mauaji. Mwishowe walipatana kusimamisha mapigano na kurudi kwenye mipaka ya kimataifa kwa sababu ya uchovu na uharibifu mkubwa pande zote mbili.
Picha
hariri-
Wanajeshi wa Uajemi wakivaa kinga dhidi ya silaha za sumu
-
Makaburi ya wafu wa vita mjini Yazd (Uajemi)
-
Wanajeshi wa Iraki wakijisalimisha mjini Khoramshahr
-
Vita kati ya Irak na Uajemi vilivyoanza tarehe22 Septemba 1980 - Tehran
Viungo vya nje
haririMakala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Vita kati ya Irak na Uajemi kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |