Kituo cha metorolojia
Kituo cha metorolojia ni mahali ambako hali ya hewa inachunguliwa kwa njia ya upimaji wa mfululizo na kutunza vipimo hivyo kwa muda mrefu. Data kutoka vituo hivyo ni msingi wa kujenga metorolojia ambayo ni tawi la sayansi kuhusu angahewa, tabianchi na halihewa.
Kituo cha metorolojia huwa na vifaa vya kupimia
- kasi ya upepo
- mwelekeo wa upepo
- jotoridi
- kiasi cha mvua
- unyevu wa hewa
- shinikizo la hewa
- kiwango cha mawingu na saa za kuwaka kwa Jua
Vipimo vya upepo vinapaswa kuchukuliwa mahali pasipo vizuizi. Lakini vipimo vya unyevu na vya jotoridi vinapaswa kuchukuliwa pasipo mwanga wa Jua kwa sababu joto la mwanga linabadilisha vipimo hivyo.
Mahali pengi kuna vituo visivyohitaji kuangaliwa kila siku na binadamu kwa sababu vipimo hukusanywa na vifaa vyenyewe na kutumwa ofisi kuu kupitia intaneti au simu. Hata hivyo bado kuna vituo vingi ambako data huangaliwa na wataalamu na waajiriwa wa kituo. Pale ambapo watu wanahudumia kituo vipimo hukusanywa angalau mara moja kwa siku; vipimo vingine kutolewa kila saa.
Kuna pia vituo kwenye bahari ambako boya zinabeba vifaa vya upimaji. Boya hizo zinafungwa mahali fulani lakini nyingine ndogo zinaelea tu kwenye maji na kupelekwa na mikondo ya bahari.