Chuo Kikuu

(Elekezwa kutoka Vyuo vikuu)

Chuo Kikuu ni taasisi ya elimu ya ngazi ya juu ambako wanafunzi wanafundishwa na wataalamu wa fani mbalimbali ambao hufundisha pamoja na kuendesha uchunguzi wa elimu mpya.

Chuo Kikuu cha Bologna (Italia) kilikuwa chuo kikuu cha kwanza cha Ulaya.
Nyumba ya Hekima mjini Baghdad (Iraki) ilikuwa kati ya watangulizi wa vyuo vikuu katika dunia ya Kiislamu tangu mwaka 800 BK.

Wanafunzi husoma kwenye chuo kikuu kwa shabaha ya kupata elimu hadi kupita mitihani ya shahada au digrii kama vile ya bachelor (ya kwanza), ya uzamili (master) (ya pili) na ya uzamivu, PhD (ya tatu).

Sifa za Chuo kikuu

hariri

Siku hizi chuo kikuu kinatakiwa kuwa na sifa kadhaa za kukitofautisha na vyuo au taasisi nyingine kama vile:

  • kuunganisha fani mbalimbali kwa kukitofautisha na vyuo vinavyofundisha fani moja tu; kwa mfano chuo cha ualimu, chuo cha teolojia, chuo cha uganga. Hata hivyo kuna vyuo vikuu vinavyokazia na kufundisha hasa upande mmoja wa elimu
  • kuunganisha kazi ya kufundisha na kazi ya uchunguzi kwa kukitofautisha na taasisi za uchunguzi zisizolenga mafundisho ya wanafunzi wa kawaida isipokuwa kuna nafasi ya kupata udokta
  • kutoa mafundisho ya ngazi ya juu inayokubaliwa kimataifa
  • kwa kawaida chuo kikuu kinatakiwa na kiwango kikubwa cha kujitawala na uhuru wa taaluma. Hali halisi hii inategemea mazingira: kuna tofauti kubwa kati nchi na nchi. Kufaulu katika maendeleo ya uchunguzi kunahitaji uhuru wa kuangalia, kuelewa na kujadili mawazo na fikra kutoka pande zote za dunia hata kama mawazo kadhaa hayakubaliwi katika mfumo wa kisiasa au kijamii ya nchi yenyewe.

Historia ya vyuo vikuu

hariri

Jamii katika tamaduni mbalimbali zilianzisha taasisi maalumu kwa elimu ya ngazi ya juu. Kati ya vyuo vya kwanza vinayofanana kiasi na chuo kikuu cha kisasa kuna hasa taasisi katika Uhindi, Ugiriki ya Kale, Uajemi, Ulaya na nchi za Kiislamu.

Mfumo wa kufundisha na kuratibu elimu ulio msingi wa vyuo vikuu vya kisasa ulianza hasa katika Ulaya ya karne za kati.

Vyuo hivi vya Ulaya viliendelea kuwa mahali pa maendeleo na kukuza sayansi ya kisasa. Kutoka hapa mfumo wa chuo kikuu pamoja na utaratibu wa ngazi zake za elimu ulisambaa kote duniani.

 
Madrasa ya Sankore mjini Timbuktu.

Vyuo vikuu vya Afrika

hariri

Kitovu cha kwanza cha elimu ya hali ya juu barani Afrika kilikuwa maktaba ya Aleksandria nchini Misri lakini ilikuwa taasisi ya kukusanya vitabu na mahali pa uchunguzi, si mafundisho.

Kihistoria vyuo vya kwanza vilivyotoa mafundisho kwenye hali ya juu ya kimataifa ya wakati wake vilikuwa chuo cha Al-Karaouine mjini Fes, Moroko tangu mwaka 859 BK na Al Azhar mjini Kairo, Misri tangu mwaka 975.

Upande wa kusini kwa Sahara ni Madrasa ya Sankore mjini Timbuktu (Mali) iliyotoa mafundisho ya hali ya juu kuanzia takriban mwaka 1400.

Vyuo vikuu vya kisasa vilianzishwa na wamisionari katika karne ya 19 nchini Sierra Leone na Afrika Kusini; vilianzishwa kama vyuo vya ualimu na kuendelea kuwa vyuo vikuu kamili.

Chuo Kikuu cha kwanza katika Afrika ya Mashariki kilikuwa Chuo Kikuu cha Makerere ambacho ni chuo mama cha vyuo vya Nairobi na Dar es Salaam.

Vyuo vikuu bora barani Afrika

hariri

Siku hizi ni hasa vyuo vikuu vya Afrika Kusini vinavyothaminiwa kuwa bora katika bara la Afrika.

Orodha ya utathmini wa vyuo vikuu bora barani Afrika kwa mwaka 2013 ilikuwa kama ifuatayo:

  1. University of South Africa, Afrika Kusini
  2. University of Cape Town, Afrika Kusini
  3. Universiteit Stellenbosch, Afrika Kusini
  4. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania
  5. University of KwaZulu-Natal, Afrika Kusini
  6. University of Pretoria, Afrika Kusini
  7. Chuo Kikuu cha Kairo, Misri
  8. University of the Witwatersrand, Afrika Kusini
  9. University of the Western Cape, Afrika Kusini
  10. Obafemi Awolowo University, Nigeria
  11. Makerere University, Uganda
  12. University of Botswana, Botswana

Kufikia mwaka 2016, vyuo vikuu kumi bora ni vyote vya Afrika Kusini. Cha Dar es Salaam kimekuwa cha 26.[1]

Majereo

hariri