Walinzi wa amani wa UM
Walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa ni vikosi vya wanajeshi wanaotolewa na nchi wanachama chini ya usimamizi wa UM kwa kulinda amani au hali ya kusimamisha mapigano.
Tangu mwaka 1948 vikosi hivyo vimetumwa kwenda mahali pa ugomvi katika sehemu mbalimbali za dunia.
Kikosi cha kwanza kiliundwa mwaka 1948 kusimamia mapatano ya kusimamia mapigano katika Palestina baada ya vita ya kwanza kati ya Israeli na nchi za Kiarabu. Baada ya vita ya Suez mwaka 1956 walinzi wa amani walitumwa mara ya kwanza wakiwa wamebeba silaha. Tangu kuingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Kongo walinzi wa amani huvaa kofia ya buluu na kuandika herufi "UN" (=UM) kwenye magari yao.
Msingi wa kutuma walinzi wa amani ni kibali cha serikali ya nchi husika pande zote katika ugomvi. Vikosi vya walinzi wa amani hawana mamlaka ya kusimama upande mmoja wala kushiriki katika mapigano. Wanatumia silaha kwa ajili ya kujitetea pekee. Hata hivyo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaweza kutoa amri kwa walinzi wa amani kuendelea kuwalazimisha washiriki katika mapigano. Kwa namna hiyo kikosi maalumu cha UM kilianza kushambulia wanamgambo katika mashariki ya Kongo waliokataa kufuata mapatano ya kusimamisha mapigano na uporaji wa wananchi.
Mwaka 2014 kulikuwa na walinzi wa amani mahali 16 duniani wakiwa na jumla ya wanajeshi na wafanyakazi 116.517. Nchi zinazotoa wanajeshi ni hasa Pakistan, Uhindi na Bangladesh, kila nchi takriban 8.000. Hadi 31 Machi 2014 jumla ya walinzi 3,215 waliuawa, 2320 kati ya hao walikuwa wanajeshi, 232 polisi, 322 wafanyakazi wa UM kutoka nchi husika na 228 wafanyakazi raia wa kimataifa.
Zaidi ya nusu ya makisio ya huduma ya walinzi wa amani hutolewa na Marekani, Japani na Ujerumani.
Walinzi wa amani walifaulu mara kadhaa kutekeleza kusudi lao lakini kuna pia mifano ambapo wameshindwa. Kati ya mifano mibaya iliyoleta upinzani ni Vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Rwanda. Hapa Baraza la Usalama la UM ambayo ni bodi pekee kuamulia kuhusu walinzi hao ilisita kupiga kura hadi mauaji nchini Rwanda yalikuwa na mbio tayari. Mfano mwingine ulikuwa Mauaji ya Srebenica nchini Bosnia ambako kikosi cha walinzi wa amani haikuruhusiwa kutumia silaha zake kikapaswa kutazama tu jinsi wanaume raia Wabosnia zaidi ya 8,000 walivyokamatwa na kuchinjwa na wanamgambo wa Serbia.