Wilaya ya Nzega Vijijini
Wilaya ya Nzega ni wilaya mojawapo kati ya 8 za Mkoa wa Tabora, nchini Tanzania, yenye postikodi namba 454.
Katika sensa ya mwaka 2012, idadi ya wakazi wa wilaya hiyo ilihesabiwa kuwa 502,252 [1] Katika sensa ya mwaka 2022 walihesabiwa 574,498 [2], baada ya mwaka 2014 maeneo ya Nzega mjini kutengwa na wilaya hiyo na kupata halmashauri ya pekee.
Eneo la Nzega
Imepakana na wilaya ya Kahama (Shinyanga) upande wa kaskazini-magharibi, wilaya ya Tabora mjini upande wa kusini na wilaya ya Igunga upande wa mashariki.
Wilaya hii ina eneo la Km² 9,226 na sehemu kubwa ni ardhi yenye rutuba inayofaa kwa kilimo. Inapokea mvua milimita 9,000 kwa mwaka.
Sehemu kubwa ya eneo ni misitu inayozaa takriban M³ 15,000 za mbao, makaa na kuni.
Kuna mito yenye samaki na milambo 13. Mto muhimu ni mto Igombe unaovuka wilaya yote.
Wakazi
Wakazi wa wilaya ni hasa Wanyamwezi na Wasukuma walio wengi kuna pia Watutsi na Wanyiramba. Vikundi vingine ni Waarabu na Wachagga wanaotazamiwa kama wageni.
Dini
Dini kubwa ni Wakristo, Waislamu na wafuasi wa dini za jadi. Wakristo ni hasa Wakatoliki na Wapentekoste. Asilimia kubwa ya watu wa vijijini ni wafuasi wa dini za jadi.
Mawasiliano
Barabara kuu inayoelekea Rwanda na Burundi inapita wilayani; kuna njia za kwenda Shinyanga, Mwanza na Tabora. Jumla ya barabara ni kilomita 1,137 lakini hakuna barabara za lami, ni theluthi moja tu inayopitika mwaka wote.
Reli ya kati kutoka Dar es Salaam kupitia Tabora kwenda Shinyanga inapita wilayani pia.
Miji ya Nzega na Bukene ina simu na posta. Uenezaji wa simu za mkononi umesaidia mawasiliano nje ya miji hii.
Elimu
Kuna shule za msingi 196 na shule za sekondari 3 pamoja na chuo cha ualimu.
Vituo vya elimu ya watu wazima vilikuwa na wanafunzi 27,857. 65% za wakazi wote walikadiriwa kuwa wasomi. Kuna uhaba wa madarasa, deski na nyumba za walimu.
Afya
Kuna hospitali mbili: moja ni hospitali ya wilaya upande wa serikali na nyingine ni hospitali ya Ndala iliyoko chini ya kanisa katoliki. Kuna sahanati 4 za serikali na 1 ya kanisa katoliki. Kliniki 29 ziko chini ya serikali, 3 za watu binafsi na mbili za kanisa.
Huduma za afya hazitoshi ni chache kulingana na idadi ya watu. Tatizo kubwa ni hali mbaya ya chakula na wakina mama wengi kiasi wanakufa wakati wa kuzaa.
Maji
Takwimu ya 1993 ilionyesha ya kwamba chini ya nusu ya wakazi walikuwa na maji safi. Sehemu kubwa ni kutoka visima na wakati wa ukame maji huwa haba. Kuna hatari kubwa ya maji kuchafuliwa. Watu wengi hawana vyoo wala nafasi za kuacha takataka.
Umeme
Huduma za umeme zinapatikana Nzega mjini na kwenye makazi kadhaa yaliyopo kwenye barabara kuu Dar es Salaam – Rwanda - Burundi.
Usalama
Kuna vituo vya polisi, Force Unit (FFU), wanamgambo wa taifa na sungusungu. Kuna mahakama ya wilaya na mahakama ndogo 13 vijijini.
Utawala na Siasa
Kuna tarafa 4, kata 37, vijiji 134 na vijiji vidogo 969.
Wilaya ina majimbo mawili ya bunge ambayo ni Nzega na Bukene. Vyama vingi vilishindana kwenye uchaguzi. CCM ilipata kura nyingi ikashinda.
Marejeo
Viungo vya nje
- Tovuti rasmi ya Halmashauri ya Wilaya ya Nzega
- Nzega District Profile kwa Redet Ilihifadhiwa 27 Machi 2009 kwenye Wayback Machine.
Kata za Wilaya ya Nzega Vijijini - Mkoa wa Tabora - Tanzania | ||
---|---|---|
Budushi | Bukene | Igusule | Ikindwa | Isagenhe | Isanzu | Itobo | Kahamanhalanga | Karitu | Kasela | Lusu | Magengati | Mambali | Mbagwa | Mbutu | Milambo Itobo | Mizibaziba | Mogwa | Muhugi | Mwakashanhala | Mwamala | Mwangoye | Mwantundu | Mwasala | Nata | Ndala | Nkiniziwa | Puge | Semembela | Shigamba | Sigili | Tongi | Uduka | Ugembe | Utwigu | Wela |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Tabora bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Wilaya ya Nzega Vijijini kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno. |