Kanisa Kuu la Azania Front
Kanisa Kuu la Azania Front (kwa Kiingereza Azania Front Cathedral) ni kanisa kuu la Walutheri lililopo jijini Dar es Salaam katika wilaya ya Ilala na ni moja kati ya vivutio vya jiji hilo la Tanzania.
Kanisa hili lipo katika barabara ya Kivukoni karibu na Waterfront, mkabala na hoteli ya New Africa na feri kuelekea mji wa Kigamboni.
Jina la Azania Front linatokana na jina la awali la barabara ya Kivukoni Front iliyopo baina ya kanisa na ufukwe wa bahari.
Historia
haririKanisa hili lilijengwa kwa gharama za mark 180,000 kuanzia mwaka 1899 baada ya kufika kwa mchungaji wa kwanza aliyetumwa kwa ajili ya Wajerumani wa Dar es Salaam. Ilifunguliwa rasmi tarehe 21 Mei 1902 ikawa kanisa la Walutheri Wajerumani katika mji mkuu wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.
Baada ya kufukuzwa kwa Wajerumani wa mwisho mwaka 1920 jengo lilitumiwa na ushirika wa Kianglikana. Tangu mwaka 1925 Wajerumani waliruhusiwa kurudi Tanganyika iliyokuwa sasa chini ya Uingereza na kanisa likarudi mikononi mwa kanisa la Kilutheri likatumiwa kwa ibada za Wajerumani na pia za ushirika wa Kiafrika.
Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia Wajerumani walifukuzwa tena na tangu siku zile hilo ni kanisa kuu la Waluteri Waafrika. Hadi sasa linasimama kama alama katika mji na hivyo limeorodheshwa kati ya kumbukumbu za taifa.
Altari ya kanisa lina maandishi kwa lugha ya Kijerumani: "Den Frieden lasse ich euch, meinen Frieden gebe ich euch" ("Amani nawaachieni; amani yangu nawapa", Yoh 14:27)
Upekee wa ujenzi wa kanisa hili unashuhudia utajiri wa ujenzi katika mji.
Picha
hariri-
Kanisa la Azania Front mnamo mwaka 2010
-
Ukumbi wa kanisa la Azania Front mnamo mwaka 1910
-
Kanisa la Azania Front mnamo mwaka 1910
Marejeo
hariri- H. Tscheuschner, Geschichte der Deutschen Gemeinde in Dar es Salaam von 1886 bis 1969, Dar es Salaam 1970 (Historia ya Ushirika wa Kijerumani wa Dar es Salaam 1886 hadi 1969, mswada)
Viungo vya nje
hariri- Tovuti rasmi ya kanisa
- Azania Front Lutheran Church kwenye tovuti ya kitalii planetware.com