Baba yetu

(Elekezwa kutoka Baba Yetu)

Baba yetu (kwa Kigiriki Πάτερ ἡμῶν, Pater emon) ni maneno ya kwanza ya sala inayotokana na Yesu mwenyewe. Kwa sababu hiyo inaitwa pia "Sala ya Bwana".

Kimataifa kuna pia jina la "Paternoster" kutokana na umbo la Kilatini la sala (Baba = "Pater"; yetu = "noster").

Ndiyo sala ya Kikristo inayojulikana zaidi. Madhehebu mengi huitumia katika kila ibada.

Maneno yake katika Biblia

hariri
 
Hotuba ya mlimani, mchoro wa Carl Heinrich Bloch (1890).
 
Pater Noster ikiwa na noti za muziki wa Kigregori.

Kufuatana na taarifa za Injili ya Luka (11:2-4) maneno ya sala hii yalitolewa na Yesu Kristo alipoombwa na wanafunzi wake awafundishe jinsi ya kusali baada ya wao kutambua kidogo anavyosali vizuri.

Katika Agano Jipya la Biblia ya Kikristo tunakuta sala hiyo kama kiini cha Hotuba ya mlimani (Injili ya Mathayo mlango wa 6, aya 13-19). Ni kama ifuatavyo:

Πάτερ ἡμῶν ὁ ἐν τοῖς οὐρανοῖς
ἁγιασθήτω τὸ ὄνομά σου
ἐλθέτω ἡ βασιλεία σου·
γενηθήτω τὸ θέλημά σου,
ὡς ἐν οὐρανῷ καὶ ἐπὶ τῆς γῆς·
τὸν ἄρτον ἡμῶν τὸν ἐπιούσιον δὸς ἡμῖν σήμερον·
καὶ ἄφες ἡμῖν τὰ ὀφελήματα ἡμῶν,
ὡς καὶ ἡμεῖς ἀφίεμεν τοῖς ὀφειλέταις ἡμῶν·
καὶ μὴ εἰσενέγκῃς ἡμᾶς εἰς πειρασμόν,
ἀλλὰ ῥῦσαι ἡμᾶς ἀπὸ τοῦ πονηροῦ.
ἀμήν.

Inasomeka:

Pater hēmōn, ho en tois ouranois
hagiasthētō to onoma sou;
elthetō hē basileia sou;
genēthētō to thelēma sou,
hōs en ouranōi, kai epi tēs gēs;
ton arton hēmōn ton epiousion dos hēmin sēmeron;
kai aphes hēmin ta opheilēmata hēmōn,
hōs kai hēmeis aphiemen tois opheiletais hēmōn;
kai mē eisenenkēs hēmas eis peirasmon,
alla rhusai hēmas apo tou ponērou.
Amēn.

Toleo la Luka ni fupi zaidi, likiwa na maombi 5 tu badala ya 7.

Tafsiri za Kiswahili

hariri

Kwa Kiswahili kuna maumbo tofauti kwa sababu sala ilitafsiriwa na wamisionari mahali mbalimbali kwa wakati tofauti na kuwa kawaida kimahali. Haikusanifishwa hadi leo kwa Wakristo wote wanaotumia Kiswahili. Maumbo mawili yanayotumiwa zaidi ni kama ifuatavyo:

Sala ya Bwana (umbo la Kiprotestanti jinsi inavyotumiwa na Walutheri na Wamoravian)

hariri
Baba yetu uliye mbinguni,
Jina lako litukuzwe,
Ufalme wako uje,
Mapenzi yako yatimizwe,
hapa duniani kama huko mbinguni.
Utupe leo riziki yetu.
Utusamehe makosa yetu,
kama sisi tunavyowasamehe waliotukosea.
Na usitutie majaribuni,
lakini utuokoe na yule mwovu.
Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele.
Amin.

Sala ya Bwana (umbo linalotumika katika Kanisa Katoliki)

hariri
Baba Yetu uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe;
ufalme wako ufike,
utakalo lifanyike
duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku,
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea.
Usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni.
Amina.

Ufafanuzi wake uliotumiwa na Fransisko wa Asizi

hariri

BABA YETU mtakatifu kabisa: muumba, mkombozi, mfariji na mwokozi wetu.

ULIYE MBINGUNI: katika malaika na katika watakatifu, ukiwaangazia wawe na ufahamu, kwa sababu wewe Bwana ni mwanga; ukiwawasha wawe na upendo, kwa sababu wewe Bwana ni upendo; ukikaa ndani mwao na kuwajaza furaha, kwa sababu wewe Bwana ni wema mkuu kabisa, wema wa milele, ambaye kwako hutoka mema yote, na bila yako hakuna jema.

JINA LAKO LITUKUZWE: ujuzi wetu juu yako uwe wazi zaidi na zaidi, tuweze kujua upana wa baraka zako, urefu wa ahadi zako, kimo cha ukuu wako, kina cha hukumu zako.

UFALME WAKO UFIKE: utawale ndani yetu kwa njia ya neema yako na kutuwezesha kuingia katika ufalme wako ambapo unaonekana kama ulivyo, unapendwa kikamilifu, unatia heri ya kukaa nawe, unatia raha ya kukufurahia milele.

UTAKALO LIFANYIKE DUNIANI KAMA MBINGUNI: tuweze kukupenda kwa moyo wetu wote, kwa kukuwaza wewe daima; kwa roho yetu yote, kwa kukutamani wewe daima; kwa akili yetu yote, kwa kuelekeza nia zetu zote kwako na kwa kutafuta utukufu wako katika yote; kwa nguvu zetu zote pia, kwa kutumia uwezo na hisia zote za roho na mwili katika kuhudumia upendo wako na si chochote kingine; na tuweze kuwapenda majirani wetu kama tunavyojipenda, kwa kuwavuta wote kwa nguvu zetu zote kwenye upendo wako, tukifurahia mema ya wengine kama tunavyofurahia ya kwetu, na tukihuzunika pamoja na wengine kwa mabaya yanayowafikia, bila ya kumuudhi yeyote.

MKATE WETU WA KILA SIKU: Mwanao mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo.

UTUPE LEO: kwa ukumbusho, ufahamu na heshima ya upendo ule aliokuwanao kwetu sisi na ya mambo yale ambayo alisema na kutenda na kuteseka kwa ajili yetu.

UTUSAMEHE MAKOSA YETU: kwa huruma yako isiyosemeka, kwa nguvu ya mateso ya Mwanao mpendwa, pamoja na stahili na maombezi ya Bikira mbarikiwa daima na ya wateule wako wote.

KAMA TUNAVYOWASAMEHE NA SISI WALIOTUKOSEA: na lolote tusilosamehe kikamilifu, wewe Bwana utuwezeshe kulisamehe kabisa, tuwapende kweli maadui wetu kwa ajili yako, na tuwaombee kwa bidii mbele zako, bila ya kumlipa yeyote ovu kwa ovu, bali tukijitahidi kumsaidia kila mmoja katika wewe.

NA USITUTIE KATIKA VISHAWISHI: kilichofichika au cha wazi, cha ghafla au cha muda mrefu.

LAKINI UTUOPOE MAOVUNI: yaliyopita, ya sasa na yajayo.

ATUKUZWE BABA NA MWANA NA ROHO MTAKATIFU KAMA MWANZO, NA SASA NA MILELE. AMINA.

Mengineyo

hariri
 
Baba Yetu kwa Kiswahili mjini Yerusalemu.

Baba Yetu kwa lugha nyingi

hariri

Katika "Bustani ya ufufuo" (Resurrection Gardens) mjini Nairobi, mtaa wa Karen, kuna maonyesho ya tafsiri ya Baba Yetu katika lugha mamia. Maneno yamechongwa na wasanii katika mawe, katika ubao au kuchorwa kwenye vigae. Hii inafuata mfano wa kanisa la Paternoster mjini Yerusalemu lenye tafsiri za Baba Yetu kwa lugha 140 kwenye vigae vya rangi (tazama Viungo vya Nje hapo chini).

Wimbo wa Baba Yetu kwa Kiswahili

hariri

Kuna wimbo wa Baba Yetu katika muziki wa mchezo wa kompyuta "Civilization IV". Wimbo huu unasikika kila wakati wa kuanza mchezo. Ulitungwa na Christopher Tin kutoka Marekani.

Wimbo ni wa kuvutia lakini kwa bahati mbaya maneno ya sala yamefupishwa kwa namna inayodokeza kwamba mhariri aliyepanga maneno kwa tuni na pia waimbaji hawakuelewa Kiswahili.

Viungo vya Nje

hariri
  Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Baba yetu kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.