Borenga ni kijiji cha kata ya Kisaka, wilaya ya Serengeti, mkoa wa Mara, nchini Tanzania.

Kijiji hicho kipo mashariki mwa kata, kwa upande wa kusini na magharibi kimepakana na kijiji cha Kisaka, kaskazini kimepakana na kijiji cha Nyamongo na mashariki kimepakana na kijiji cha Morito.

Katika kijiji cha Borenga jamii yake ni kabila la Wangoreme na asilimia ndogo sana ni Wajaluo, ambao wengi wao wanaishi kitongoji cha Biasuma.

Wangoreme wanaoishi Borenga wanatoka katika koo za Wahiri Saroti na Wahiri Matiti.

Wahiri Saroti ndio ukoo mkubwa kuliko zote ambao ndio wenye majina kama Mchanake, Masiana, Saroti, Ole Munye, Nkombe, Kitang'ita, Wandwe na Chacha, kwa majina ya kike kuna majina mengi sana, lakini maarufu sana ni Nyamboge.

Wahiri Saroti ni wale wenye asili ya Kimasai, kutokana na mwasisi wao ambaye anaitwa Saroti,

Saroti alikuwa kijana wa Kimasai aliyeachwa na wenzake porini akaamua kuanzisha makazi mapya katika eneo moja linaloitwa Kisima cha Kiru.

Katika kisima kile alikuwa anakula matunda na mwili wake ulikuwa na vinywelea au nywele nyingi sana. Alikula matunda kwa muda mrefu sana, lakini kadiri alivyoishi pale aliweza kufanikisha kupata mbegu za ulezi akaanza maisha ya ukulima.

Siku moja Mzee Matiti na familia yake, wakiwa katika harakati za kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine, walijipumzisha kichakani wakalala ili kesho yake waendelee na safari yao, lakini ilipofika alfajiri, majira kama saa kumi na mbili kasoro, akiwa ametoka kichakani aliweza kuona moshi unafuka mlimani: ndipo wakapata hisia, kumbe kuna watu wanaishi eneo lile, wakaufuatilia ule moshi wapate kujua ni nani yupo pale, kumbe alikuwa ni Saroti, amewasha moto akijiandaa kwenda shambani. Ghafla mzee Matiti na familia yake wakamkuta Saroti ambaye aliwakaribisha na kuwapatia utaratibu wa maisha.

Basi kwa vile yalikuwa ni maisha mapya kwa mzee Matiti, ilibidi Saroti awasaidie chakula pamoja na kuwapatia mbegu za ulezi.

Msimu ulipofika wote wakavuna chakula, lakini kwa vile mzee Matiti alikuwa na familia kubwa, chakula chao kiliwahi kwisha mapema na msaada wao ukabaki kwa Saroti, kijana wa Kimasai.

Siku moja mzee Matiti alimweleza binti yake mkubwa aolewe na Saroti ili awapatie mahari ya chakula. Yule binti alikataa kwa sababu Saroti alikuwa na nywele mwili mzima, lakini mdogo wake, ambaye alikuwa anaitwa Nyamboge, alikubali kwa sharti moja: kuwa Saroti akubali kunyoa zile nywele. Saroti akakubali kunyolewa akakubali kutoa mahaRi ya ghala moja la chakula (Eghitara).

Basi hiyo ikawa mwanzo wa maisha ya Saroti na ndoa yake na Nyamboge, binti Matiti. Walifanikisha kupata mtoto aliyeitwa Kitang'ita. Kitang'ita akamzaa Gogai, naye pia akamzaa Wandwe, Wandwe akamzaa Masiana, Masiana akamzaa Chacha, naye akamzaa Bochoke, ndipo akapatikana Mchanake na Mchanake pia akamzaa Masiana.

Kwa upande wa familia ya mzee Matiti, wao waliendelea na maisha yao na wakawa koo kubwa ambazo ni akina Matuki, Magere, Maituki, Charwe na wengine wengi.

Koo kubwa katika kijiji cha Borenga ni hizo mbili, ingawa kuna koo ndogongogo kama Waihindi na Walomole ambao asili yao ni Buchanchari.

Kimaendeleo kijiji cha Borenga hakipo nyuma sana, kwani wakazi hujishughulisha sana na kilimo, wanakijiji wake hutumia eneo lenye rutuba nzuri kandokando ya mto Mara: maeneo kama Buhabu, Kerende, Gwitura, Lenyamheta na Kenyangi, hayo ni baadhi ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo na huwapatia wananchi wa Borenga mavuno mengi.

Maeneo hayo vilevile hutumiwa kwa ajili ya malisho au ufugaji.

Kisiasa kijiji cha Borenga hakipo nyuma, kwani kina wanasiasa machachari kama Nashon Masiana aliyewahi kuwa diwani wa kwanza wa kata ya Kisaka. Pia kuna wazee kama Raphael Mosimbete aliyepata kuwa mwenyekiti wa kijiji machachari sana, na marehemu Yusuph Nyamhanga Masiana.