Kaboni
Kaboni (kutoka Kilatini carbo, kwa kupitia Kiingereza carbon) ni elementi yenye namba atomia 6 na uzani atomia 12 kwenye mfumo radidia. Alama yake ni C.
Kaboni (Carbon) | |
---|---|
Jina la Elementi | Kaboni (Carbon) |
Alama | C |
Namba atomia | 6 |
Mfululizo safu | Halojeni |
Uzani atomia | 12,0107 u |
Valensi | 2,4 |
Ugumu (Mohs) | grafati: 1–2 almasi: 10 |
Kiwango cha kuyeyuka | 3820 K (3550 °C) |
Kiwango cha kuchemka | 5100 K (4800 °C) |
Inapatikana peke yake kwa maumbo mbalimbali, kama vile makaa au almasi, lakini mara nyingi zaidi katika michanganyiko ya kikemia. Inapatikana kwa umbo la isotopi tatu; kati ya hizi 12C na 13C ni thabiti, lakini 14C ni nururifu.
Moja ya tabia za kaboni ni uwezo wake wa kuungana na elementi nyingi, na hivyo kuunda molekuli kubwa.
Kaboni, pamoja na oksijeni, ni elementi muhimu zaidi katika viumbe hai wote, wakiwa pamoja na mimea na wanyama. Iko katika idadi kubwa ya kampaundi ogania yaani kaboni ni sehemu ya kampaundi hizo zote.
Katika teknolojia kaboni ni muhimu kwa sababu ni msingi wa aloi zote za chumapua na hivyo teknolojia ya kisasa. Kwa upande mwingine kaboni iko pia katika aina zote za plastiki.
Nyuzi nyembamba za kaboni zinatumiwa pamoja na rezini[1] ya plastiki katika utengenezaji wa sehemu za bodi za ndege, motokaa au vifaa vya kijeshi ambapo uzito mdogo pamoja na uthabiti ni muhimu. Nyuzi za kaboni zinapitisha vizuri joto na umeme. Kwenye mwelekeo wa urefu ni imara sana na pia nyepesi kuliko nyuzi nyingine, kama vile nyuzi za kioo, metali au plastiki. Hivyo zinafaa kuunda dutu thabiti yenye uzito mdogo.
Katika teknolojia ya nano mabomba membamba mno ya kaboni yameanza kutumiwa kwa kutengeneza vifaa imara na vyepesi sana.
Fani ya akiolojia hutumia mbunguo nururifu wa 14C kutambua umri wa dutu ogania. Mbinu ya rediokaboni[2] inaruhusu kujua umri wa ubao, mifupa na mabaki mengine ya viumbehai hadi muda wa miaka 60,000 iliyopita.
Picha
hariri-
Makaa ya mawe (bituminous)
-
Makaa ya mawe (anthracite)
Marejeo
hariri- ↑ rezini ni pendekezo la KAST kwa ing. resin
- ↑ http://www.dummies.com/how-to/content/nuclear-chemistry-halflives-and-radioactive-dating.html Nuclear chemistry halflives and radioactive dating
Makala hii kuhusu mambo ya kemia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kaboni kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |