Muda sanifu wa dunia

(Elekezwa kutoka Coordinated Universal Time)

Muda sanifu wa dunia (kufupi cha kitaalamu ni UTC kwa "universal time coordinated") ni utaratibu wa kulinganisha saa na wakati kote duniani. Unarejea wakati kwenye longitudo ya Greenwich karibu na London na longitudo hii huitwa pia meridiani ya sifuri.

Kanda muda duniani; namba zinaonyesha tofauti na saa ya Greenwich = meridiani ya sifuri

Hesabu ya muda kulingana na kanda Edit

Kutokana na meridiani ya Greenwich dunia imegawiwa kwa kanda muda ambazo ni kwa sasa 40. Ndani ya kila kanda muda wa saa ni uleule. Saa ya Greenwich au meridiani sifuri ni wakati wa marejeo. Kutoka mstari wake kila mahali ina saa yake kama kuongezekewa au kupungukiwa kutoka wakati huu. Wakati wa Afrika ya Mashariki unatangulia masaa 3 mbele ya wakati wa Greenwich.

Mfano mtu anapiga simu ya nje kutoka Tanzania saa 2 usiku atampata mwenzake pia saa 2 kama yuko huko Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudani au Uarabuni maana wote wako katika kanda muda moja. Saa ya marejeo, yaani, Greenwich ni sasa saa 11 jioni. Lakini akipiga simu huko China atapampata mwenzake saa 8 usiku maana huko saa inatangulia masaa 5; kinyume akipiga wakati huohuo New York ya Marekani ataongea na mtu aliye kwenye saa 6 mchana.

Kwa lugha ya muda sanifu wa dunia Mtanzania wetu alipiga simu saa "17.00 UTC+3" yaani saa 11 jioni kwenye meridiani ya sifuri ongeza masaa matatu. Wenzake huko Beijing wako kwenye saa "17.00 UTC+8" (mahali pa kuongeza masaa 8 kwenye saa ya meridiani ya sifuri) na rafiki pale New York yuko saa "17.00 UTC-5" (mahali pa kutoa masaa 5 kwenye saa ya Greenwich). Kwa hiyo tofauti kati ya Dar es Salaam au Nairobi ni masaa 8 maana masaa 3 kutoka Afrika ya Mashariki hadi meridiani ya sifuri na tena masaa 5 hadi New York. Tukipiga simu mahali mbali zaidi upande wa magharibi mfano Los Angeles tofauti huwa kubwa zaidi.

Nchi kubwa kama Urusi na Marekani huwa na kanda muda tofauti ndani ya taifa kati ya mashariki na magharibi; nchi ndogo zaidi kwa kawaida zimepangwa katika kanda ileile.

Sababu za kugawa dunia kwa kanda muda Edit

Kanda hizi ni mapatano ya kisiasa kwenye msingi wa kisayansi. Sababu yake ya kimsingi ni ya kwamba wakati uleule kuna mchana upande mmoja wa dunia na usiku upande mwingine. Mtanzania anayepiga simu saa mbili usiku yuko gizani lakini mwenzake New York yuko mchana akiona jua juu yake angani.

Ugawaji wetu wa saa za siku na usiku kiasili unafuata mwendo wa jua na nuru. Kuna mstari kuanzia kaskazini hadi kusini ya dunia unaotembea juu ya uso wa dunia ambako kunakucha wakati huohuo. Kwa kupata saa inayolingana na mwanga na nuru ingekuwa vema kama miji na vijiji vyote vinavyokaa kwenye kwenye mstari 1 wa kucha vingekuwa na wakati huohuo na hivi kama kanda muda moja.

Hapa siasa inaingia maana watu wanaokaa nchi moja wanapendelea kuwa na saa ileile. Hata kama tofauti ya saa ya kucha kati Zanzibar na Kigoma ni karibu saa moja miji yote miwili imepangwa ndani ya kanda muda ileile kwa sababu zote mbili ziko Tanzania.

Zamani hapakuwa muhimu kusanifisha wakati kwa sababu watu walisafiri au waliwasiliana polepole. Hali halisi kila mahali palikuwa na wakati wake; watu waliangalia jua wakasema sasa saa 1 asubuhi au saa 6. Hata baada ya kutokea masaa ya kwanza vifaa hivi viliwekwa muda kutokana na kutokea kwa jua mahali penyewe.

Ni tangu kuanzishwa kwa usafiri wa reli na mawasiliano kwa simu ya kwamba haja ilitokea kulinganisha muda wa kila mahali. Maana kama zamani mtume alitembea kwa miguu au kupanda farasi kubeba barua tangu karne ya 19 ujumbe ulifika kwa simu mara moja kwenye mahali penye saa tofauti.

Hapo majaribio ya kulinganisha na kusafisha wakati yalitokea.

Nchi ya kwanza kufanya hivyo ndani ya taifa ilikuwa Uingereza na hapo ni asili ya kipaumbele wake wa kihistoria inayoonekana katika chaguo la Greenwich kama rejeo la meridiani ya sifuri. Greenwich ilikuwa na kituo bora cha kuangalia nyota na kazi ya kupima nyota ni muhimu wa kulinganisha wakati kikamilifu hadi leo.