Danieli (kwa Kiebrania na Kiaramu דָּנִיֵּאלdāniyyēl) ni mhusika mkuu wa Kitabu cha Danieli kwenye Biblia. Wayahudi wanamwona kama mtu mwenye hekima kubwa, Wakristo na Waislamu wanamjua kama nabii.

Katika simulizi la Kitabu cha Danieli yeye ni kijana Myahudi kutoka Yerusalemu anayekamatwa na mfalme Nebukadreza pamoja na wakazi wengine wa mji na kupelekwa uhamishoni Babeli. Hapo anamhudumia mfalme na wafuasi wake hadi wakati wa mfalme Koreshi wa Uajemi anayeshinda Babeli na kuwapa Wayahudi uhuru wao tena.

Wataalamu wa siku hizi wanaona kwamba kitabu si taarifa ya kihistoria bali masimulizi ya kishairi yaliyotungwa karne kadhaa baadaye katika mazingira ya mashambulizi ya wafalme Wagiriki katika nchi ya Israeli. Uwezekano mkubwa ni kwamba Danieli hakuwa mtu wa kihistoria bali mhusika katika masimulizi yanayolenga kujenga imani katika mazingira ya kiadui.

Hata hivyo, kuna miji sita ambako wenyeji wanaonyesha kaburi la Danieli. Maarufu zaidi liko huko Shushani, kusini mwa Iran.

Jina la Danieli linamaanisha "Mungu (El) ndiye hakimu wangu". Pamoja na huyo Danieli, mhusika katika kitabu chake, Biblia inataja watu walioitwa kwa jina hilo kwenye nafasi tatu nyingine:

  1. Kitabu cha Ezekieli (14:14, 14:20 na 28: 3) kinamrejelea Danieli mmoja mashuhuri aliyejulikana kwa hekima na haki. Katika aya ya 14:14, Ezekieli anasema juu ya nchi yenye dhambi ya Israeli kwamba "wajapokuwa watu hawa watatu, Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kuwamo ndani yake, wangejiokoa nafsi zao wenyewe tu kwa haki yao". Katika sura ya 28, Ezekieli anamdhihaki mfalme wa Tiro, akiuliza kwa maneno ya kejeli, "wewe una hekima kuliko Danieli?" Kama kitabu cha Danieli si cha kihistoria, basi mwandishi wake anaonekana alichukua sura hii ya hadithi, mashuhuri kwa hekima yake, kutumika kama mhusika wake mkuu.
  2. Ezra 8: 2 inamtaja kuhani aliyeitwa Danieli ambaye alitoka Babeli kwenda Yerusalemu na Ezra.
  3. Daniel alikuwa mwana wa mfalme Daudi aliyetajwa kwenye 1 Mambo ya Nyakati 3: 1.

Marejeo

hariri

Vitabu juu yake

hariri

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Danieli (Biblia) kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.