Mambo ya Nyakati

ya kumi na tatu kitabu Biblia, mchanganyiko tu 29 sura ya

Mambo ya Nyakati ni jina la maandiko yanayoheshimiwa na dini za Uyahudi na Ukristo kama matakatifu, yaani yenye uvuvio wa Roho Mtakatifu wa Mungu.

Mazingira ya vitabu vya Mambo ya Nyakati

hariri

Kama ilivyokuwa kwa vitabu vya Samweli na vitabu vya Wafalme, Mambo ya Nyakati ni vitabu viwili katika Biblia ya Kikristo, lakini katika Biblia ya Kiebrania (Tanakh) ni kitabu kimoja tu.

Mwandishi (labda ni zaidi ya mmoja) hakutaja jina lake, ingawa alitaja majina ya baadhi ya vitabu na maandiko mengine alipopata habari zake (1 Nya 9:1; 27:24; 29:29; 2 Nya 9:29; 16:11; 24:27; 33:19; 35:25), akiandika kwenye karne ya 5 K.K.

Katika Mambo ya Nyakati tunapata masimulizi ya matukio yaliyotokea Israeli wakati uleule wa vitabu vya Samweli na vya Wafalme, lakini vitabu hivyo vinatofautiana katika mtindo wa uandishi na mambo yaliyomo, hasa kwa sababu mwandishi wa Mambo ya Nyakati aliandika kwa ajili ya watu wa wakati maalumu akiwa na makusudi yake ya pekee.

Hali ya wakati ule

hariri

Kitabu cha Mambo ya Nyakati kiliandikwa miaka mingi baada ya Israeli na Yuda kupelekwa uhamishoni Babeli.

Watu wengi wa ufalme wa kaskazini waliopelekwa sehemu mbalimbali za ufalme wa Ashuru miaka 732 na 722 K.K., walitawanyika miongoni mwa watu wa sehemu zile, na kwa jumla walipoteza ufahamu wa taifa lao.

Kumbe watu wa ufalme wa kusini waliopelekwa Babeli katika awamu mbalimbali kati ya 605 na 582 K.K., kwa jumla walikumbuka asili yao.

Waajemi waliposhinda na kuteka Babeli mwaka 539 K.K., waliwapa Wayahudi ruhusa ya kurudi katika nchi yao. Waliorudi walikuwa toka kundi hilo la pili. Wengine walirudi baadaye.

Watu wengi kati ya wale waliorudi walikuwa hawajaona nchi ya Palestina hapo awali, na bila ya shaka walijua kidogo sana kuhusu hekalu na ibada zake.

Wajukuu wao ndio watu ambao mwandishi wa Mambo ya Nyakati aliwaandikia ili kuwapa ujuzi wa mazingira ya nchi na dini yao. Zaidi ya hayo, alitaka waelewe kwamba walikuwa zaidi kuliko kikundi cha watu waliohamia ili waishi katika nchi ya mababu wao.

Kwa njia ya watu hao, taifa lililokuwepo kabla ya uhamisho liliendelea, na maisha yao yalijengwa juu ya msingi wa ufalme wa Daudi na ukuhani wa Walawi.

Shabaha kubwa za Mambo ya Nyakati

hariri

Mungu alikuwa na makusudi yake alipotaka kuwaimarisha watu wake katika nchi yao tena. Alikuwa bado anatawala historia yao, na ahadi zake alizowapa Daudi na watu wa nasaba yake zilihitaji kutimizwa.

Kwa hiyo mwandishi wa Mambo ya Nyakati alichagua na kupanga masimulizi yake kwa uangalifu, ili wasomaji wake waweze kuona umuhimu wa kujengewa taifa lao upya kufuatana na makusudi ya Mungu.

Ingawa alifuatia historia ya Israeli kuanzia mfalme wa kwanza (Sauli) hadi wakati wa uhamisho wa Babeli, alimtaja Sauli kwa kifupi tu. Hali kadhalika alisema maneno machache tu kuhusu ufalme wa kaskazini. Alishughulika hasa na nasaba ya ufalme wa Daudi na hekalu la Yerusalemu ambalo wafalme hao walihusika nalo.

Ufalme wa kaskazini ulitokana na farakano na ufalme uliochaguliwa na Mungu, yaani wa Daudi, na kwa kiasi fulani dini yake ilikuwa ya maasi dhidi ya ibada ya kweli ya Mungu ambayo mahali pake rasmi palikuwa Yerusalemu. Mwandishi wa Mambo ya Nyakati hana nia ya kuwavutia wasomaji wake kuhusu ufalme wa kaskazini na mambo yake ya dhambi. Kwake ufalme wa Daudi ni wa pekee uliothibitishwa, na Yerusalemu ni jiji kuu la pekee lililochaguliwa. Alifanya bidii nyingi kuonyesha kutokana na historia ya ufalme wa kusini (chini nasaba ya Daudi) jinsi dini pekee iliyokubaliwa na Mungu ilivyokuwa na maana sana kwa maisha ya watu wa kweli wa Mungu.

Kutokana na lengo kuu la mwandishi, hata maelezo ya Mambo ya Nyakati yanatofautiana na maelezo ya matukio yaleyale katika vitabu vya Samweli na vya Wafalme. Kwa mfano, habari kama zile za dhambi ya Daudi na Bethshebea na zile zinazohusu matatizo ya nyumbani mwake hazikuandikwa.

Madhumuni ya mwandishi hayakuwa kuchunguza maisha ya watu binafsi, bali kuonyesha jinsi ufalme wa Daudi ulivyoimarishwa pamoja na mpango wa dini na maisha ya kitaifa ya Israeli kuwa mambo yasiyoweza kutenganishwa.

Kwa upande mwingine, mwandishi aliongeza mambo mengi yasiyoandikwa katika Samweli na Wafalme, hasa mambo yanayohusu mpango wa dini ya Israeli wakati wote wa ufalme huo.

Hamu kubwa ya mwandishi ni kwamba, watu waishio katika Israeli baada ya uhamisho wa Babeli wapange maisha yao juu ya msingi wa dini ya kweli. Kwa sababu hiyo Walawi ambao hawakutajwa sana katika vitabu vya Wafalme walitajwa mara nyingi katika Mambo ya Nyakati.

Kwa mwandishi wa Mambo ya Nyakati, dini ya pekee inayofaa kuipokea ni ile iliyojengwa juu ya msingi wa kanuni za Walawi, yaani ukuhani wa Haruni na hekalu la Yerusalemu.

Muhtasari wa Kitabu cha kwanza cha Mambo ya Nyakati

hariri

1:1-9:34 Orodha za vizazi (nasaba) vya makabila ya Israeli

9:35-22:1 Utawala wa Daudi

22:2-29:30 Maandalizi kwa hekalu

Muhtasari wa Kitabu cha pili cha Mambo ya Nyakati

hariri

1:1-9:31 Utawala wa Sulemani

10:1-36:23 Wafalme wa Yuda

Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki

Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.