Dizasta Vina

Msanii wa muziki

Edger Vicent (anafahamika zaidi kwa jina la kisanii kama Dizasta Vina; amezaliwa 17 Februari 1993) ni msanii wa muziki wa Hip Hop na mtayarishaji wa muziki kutoka nchini Tanzania.

Dizasta Vina
Dizasta Vina akiwa Stejini—Septemba 2018, Dar es SalaamTanzania.
Taarifa za awali
Jina la kuzaliwaEdger Vicent
Pia anajulikana kamaFundi Vina
Professor Tungo
The Black Maradona
Amezaliwa17 Februari 1993 (1993-02-17) (umri 27)
Iringa,Tanzania
Kazi yakeMchanaji, mtunzi, mshairi, Mtayarishaji
AlaSauti, keyboards, sampler
Miaka ya kazi2007-hadi leo
StudioPanorama Authentik
Ameshirikiana na

Ni msanii ambaye muundo wa mashairi yake huwasilisha visa, matukio na hadithi katika njia ya kupendeza na kumvutia msikilizaji kuendelea kusikiliza. Tungo zake zinatazamia zaidi maisha halisi ya raia wa Tanzania na Afrika kwa ujumla. Pia anapenda kufanya muziki unaogusa harakati za wanajamii, kukemea maovu na kusimamia misingi ya utetezi wa wanyonge.

Maisha ya awaliEdit

Dizasta vina alizaliwa mnamo tarehe 17 Februari ya mwaka wa 1993, katika Mkoa wa Iringa, Tanzania. Kiasili, ni Mnyakyusa wa Mbeya. Ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia yake na ni mwanamume pekee akiwa na dada zake wawili.

Elimu yake ya msingi aliipata katika shule ya msingi ya Kimanga iliyopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam aliandikishwa katika shule hiyo mnamo mwaka wa 2001. Mwaka wa 2007 alijiunga na masomo ya sekondari katika shule binafsi ya White Lake High School iliyopo eneo la Changanyikeni jijini Dar es Salaam kisha kumaliza masomo ya sekondari katika shule ya Southern Highlands Secondary School iliyopo Soweto jijini Mbeya — mnamo mwaka wa 2O1O. Aliendelea na masomo ya elimu ya juu katika shule ya Kigoma High School, Kigoma ambapo alisoma kwa muda wa miezi minne tu kabla ya kumalizia katika shule ya Mbeya High School na kisha kujiunga na masomo ya elimu ya juu katika Chuo cha usimamizi wa fedha IFM mwaka 2013.

Kazi ya muzikiEdit

 
Dizasta vina katika Pozi — 2019.

Alianza kuupenda muziki tangu akiwa mtoto,anasema "familia yetu inapenda muziki sana, mama na dada zangu wote waliimba kwaya katika vipindi tofauti,na wengine bado wanaimba mpaka sasa". Dizasta Vina alikuwa anakariri nyimbo za wasanii mbalimbali wakubwa hapa Tanzania kama Professor Jay, Afande Sele, Juma Nature na Solo Thang na hata watu walikuwa wakimpa pesa ili awaimbie baadhi ya nyimbo zilizotamba wakati huo. Anasema "Nilipata msukumo mkubwa wa kufanya muziki kutoka katika album ya Machozi Jasho na Damu ya Professor Jay".

Dizasta vina alianza rasmi kujihusisha na kazi ya sanaa mnamo mwaka wa 2007 kwa kushiriki katika matamasha na mashindano mbalimbali ikiwa ni pamoja na SM Straight Music Freestyle Battle mwaka 2010 mkoani Iringa. Hapa ndipo alipoanza hamasa ya kutaka kuwa MC. Vuguvugu hili liliendelea hadi kufikia kuwa huyu Dizasta Vina wa leo.[1]

Mnamo mwaka wa 2011 alikutana na mtayarishaji wa muziki aliyemwinua kisanaa, Duke Touchez.", Duke alimpa mwongozo wa jinsi ya kujiunga na Tamaduni Muzik ambayo kwa kipindi hicho ilikuwa inatafuta vipaji vipya kwa ajili ya "Tamaduni Foundation" Dizasta alishiriki mashindano ya kughani katika tamasha la kuachia Santuri 5 kwa mpigo (African Son ya Stereo, Sauti ya Jogoo ya Nikki Mbishi, Mzimu wa Shabaan Robert ya Nash Mc,Underground Legendary ya Duke Touchez na Mathematrix ya Songa na Ghetto Ambassador) na kufanikiwa kujiunga rasmi na Tamaduni Muzik .

Mwaka 2012 alifanikiwa kuachia wimbo wake rasmi Harder na kushiriki katika nyimbo kadhaa za kushirikiana ikiwa ni pamoja na The ultimate, Sauti ya Mtaa na nyinginezo kwa kipindi cha kati ya mwaka 2012 na 2013. Mwaka 2013 aliachia nyimbo zingine kama vile Tega sikio, Goli la ushindi, Nyumba Ndogo na Sister, pia alishiriki kwenye "Underground Project" ya mtayarishaji wa muziki anayefahamika kwa jina la AK 47, katika wimbo unaoitwa Heavyweight akishirikiana na msanii wa kike Tifa Flows.

Pia alishiriki katika santuri ya Uwezo ya mtayarishaji wa muziki Ngwesa katika wimbo wa Miss tamaduni akishirikiana na Jeff Duma. Mwaka huo huo alishiriki katika albumu ya upande wa pili wa sarafu ya muandaaji wa muziki Abby Mp, kazi ya kilinge ya Duke Touchez, albumu ya Kiutu Uzima ya msanii Kadgo, Kanda mseto ya Slow Jams ya muandaaji wa muziki - Innocent Mujwahuki, Tamaduni Foundation ya Ngwesa na Representing Africa Popote ya One the Incredible.

Mwaka 2015 alitoa wimbo unaoitwa Kijogoo na kushiriki katika wimbo wa Siku Nikifa wa Kipepe.

Dizasta Vina anatajwa kuwa ni miongoni mwa wasanii wa kizazi kipya wanaoleta heshima ya hip hop Tanzania na kibao chake kinachojulikana kama Kanisa kilifanya vizuri ambapo ndani yake kuna uandishi wa kipekee ambao umeenda tofauti na ule uliokuwa umezoeleka (masimulizi/mipasho).[2]

Mara kadhaa amekuwa akitajwa kama mwanahip hop bora na mtunzi mzuri wa nyimbo za masimulizi nchini Tanzania.[3]

Kutayarisha muzikiEdit

 
Dizasta Vina akiwa katika studio za Panorama Authentik jijini Dar es Salaam, Tanzania— mnamo tarehe 17 Februari, 2018.

Miaka ya karibuni amekuwa akitayarisha muziki wake mwenyewe, hii ni baada ya kuamua kukaa chini na kuanza kusoma jinsi ya kutayarisha muziki na kufanya uhandisi wa sauti. Baadhi ya vibao vyake mashuhuri alivyotayarisha mwenyewe ni pamoja na Fallen Angel iliyotoka Julai 23 2016, Kanisa iliyotoka Novemba 13 2016 na The Lost One iliyotoka Aprili 2017.

Uwezo wake mkubwa kama mtayarishaji ulianza kuonekana kupitia mfululizo wa nyimbo zake kama vile Hatia, Nobody is Safe, Hatia II, Hatia III na Kikaoni, kibao ambacho kimejizolea umaarufu mkubwa kwa wapenzi wa utamaduni wa handakini kutokana na kugusa maisha ya familia na ndoa. Wimbo huu ulipotoka ulileta sura mpya kwa wasikilizaji wa hip hop ya Tanzania. Dizasta kwa mara ya kwanza alipata mwaliko kwenye Dakika 10 za Maangamizi kipindi kidogo ndani ya kipindi cha Planet Bongo cha East Africa Radio kinachoongozwa na mtangazaji Abdallah Khamis Wambuwa. Ndani ya kipindi, mistari ya wimbo wa Kanisa ilifanya kila mtu kumsikiliza Dizasta Vina kwa umakini na mistari hiyo imesisimua watu wengi sana na kuamsha maswali mengi baada ya kulizungumzia kanisa kwa mapana zaidi[4].

Anakubali kuwa amepata sana utaalamu na mbinu za kutayarisha muziki kutokana na kufanya kazi na watayarishaji wengine wa muziki wa Kitanzania kama Duke Touchez, Ray Teknohama na Ringle Beats. Dizasta anaamini kuwa na taaluma ya kutayarisha muziki wake mwenyewe kuna faida kubwa kwani kunafanya afikie hisia halisi za wimbo tofauti na pale anapotafuta na kujenga mahusiano ya kimuziki na mtayarishaji mwingine.

Dizasta Vina na Tamaduni MuzikEdit

Tamaduni ni lebo ambayo Dizasta Vina alifanya nayo kazi baada ya uwezo na uelewa wake kuhusu utamaduni wa Hiphop kumvutia Duke Touchez ambaye alifanikisha Dizasta kujiunga na "Tamaduni Foundation" akiwa na wasanii kama One the Incredible, Nikki Mbishi, Boshoo na wengineo. Kupitia Tamaduni Muzik waliweza kubadilisha na kutimiza nguzo karibia zote za hip hop zinavyotaka. Maoni ya Dizasta Vina kuhusu Tamaduni Muzik ni kwamba ndio wao waliobadilisha mtazamo na mwelekeo mzimaa wa muziki wa hip hop ya Tanzania. Kupitia wao, tuliweza kuona kutolewa kwa albamu kwa sana hata kwa wasanii wachanga, kutoa kandamseto, kurudisha maonesho ya hip hop kukusanya wasanii “Kilingeni” huko Msasani Club.

Kifupi Tamaduni Muzik imehakikisha sanaa ya muziki wa hip hop inapata nafasi kubwa katika jamii ya Watanzania. Wameutetea mno muziki huu.

MarejeoEdit

  1. Dizasta Vina: Zawadi nyingine kwa wapenda HipHop Tanzania (en-US). JamiiForums. Iliwekwa mnamo 2019-05-06.
  2. Dizasta Vina anaweza akawa ndio best rapper Tanzania (en-US). JamiiForums. Iliwekwa mnamo 2019-05-06.
  3. Best 5 Storytelling Rap Songs (en-US). JamiiForums. Iliwekwa mnamo 2019-05-06.
  4. EastAfricaRadio (2018-02-13), Dakika 10 Za Maangamizi- Dizasta Vina | Planet Bongo I, retrieved 2019-05-06 

Viungo vya njeEdit

  Makala hii kuhusu mwanamuziki/wanamuziki fulani wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Dizasta Vina kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.