Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania

(Elekezwa kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania)

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) (kwa Kiingereza Tanzania People's Defense Force TPDF) ni jeshi lililoanzishwa mnamo mwezi Septemba katika mwaka wa 1964. Ilichukua nafasi ya jeshi la Tanganyika Rifles lililorithiwa na ukoloni wa Waingereza.

Maandamano ya JWTZ wakati wa sikukuu ya Mapinduzi ya Zanzibar, 2000.
Askari wa King's African Rifles mnamo 1944.

Historia ya awali[1]

Kabla ya ukoloni

 
Kikosi cha Warugaruga waliosaidia Schutztruppe ya Kijerumani wakati wa Vita Kuu ya Kwanza

Kabla ya ukoloni jumuiya za watu katika eneo la Tanzania walikuwa na jeshi lililojumuisha wanaume wote hasa vijana. Lakini baada ya vita kila mtu alirudi kwa kazi yake ya kawaida hapakuwa na askari wa kudumu. Katika karne ya 19 mfumo mpya wa vita ulienea baada ya kufika kwa Wangoni waliopanga askari kufuatana na umri kwa vikosi ("impi") na vikosi hivi vilikutana kwa mazoezi hata nje ya vita yenyewe.

Tangu kuenea kwa silaha za moto viongozi kadhaa kama Mirambo waliunda vikosi vya rugaruga waliokusanya vijana kutoka makabila mbalimbali kwa ajili ya vita.

Sultani wa Zanzibar alikuwa na wanajeshi wa kudumu. Mwanzoni alitumia mamluki walioajiriwa kutoka Uarabuni na Uajemi, hasa Baluchistan, pamoja na watumwa[2]. Kuanzia mwaka 1877 alianzisha kikosi kipya cha askari mia kadhaa chini ya afisa Mwingereza Lloyd Mathews waliofundishwa kufuatana na utaratibu wa Kizungu; askari hao waliteuliwa chini ya Waafrika wa Unguja.[3]

 
Askari wa Schutzruppe akishika Bendera ya Ujerumani

Schutztruppe ya Kijerumani

Makala kuu: Schutztruppe

Koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani ilianzishwa kwa njia ya vita kadhaa ambako jeshi la Kijerumani lilishinda upinzani wa wenyeji. Wajerumani walitumia askari kutoka kwao pamoja na askari waliokodiwa kutoka Sudani na Wazulu kutoka Afrika Kusini. Waliendelea kuajiri Waafrika wazalendo na kujenga jeshi la Schutztruppe (tamka shuts-tru-pe) lililokuwa hasa na askari Waafrika waliohudumia chini ya maafisa Wajerumani. Jeshi hilo liliimarisha utawala wa kikoloni. Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, liliweza kuzuia mashambulizi ya Waingereza hadi mwaka 1916 likaendelea kujitetea hadi mwisho wa vita 1918. Jeshi hili lilivunjwa baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

King's African Rifles ya Kiingereza

Mwaka 1919 Uingereza ilikabidhiwa utawala juu ya Tanganyika na Shirikisho la Mataifa. Waingereza waliwahi kuanzisha mfumo wa King's African Rifles kabla ya vita katika koloni yao ya Kenya. Askari wa kawaida walikuwa Waafrika waliosimamiwa na maafisa Waingereza. Baada ya kutwaa utawala juu ya Tanganyika walieneza mfumo huo pia huko. Jeshi la Kings African Rifles lilikuwa na vikosi (battalions) 6 ambazo viwili vilikuwepo Kenya, vitatu Tanganyika na kimoja huko Uganda. Katika kikosi cha sita cha King's African Rifles kilichoanzishwa mwaka 1917 kwa kuajiri askari kutoka Tanganyika walikuwepo pia askari wa awali wa jeshi la Kijerumani la Schutztruppe waliowahi kukamatwa kama wafungwa na kukubali kuendelea upande wa Waingereza.

Tanganyika Rifles baada ya uhuru

Makala kuu: Tangayika Rifles

Baada ya uhuru mwaka 1961 vikosi vya Kings African Rifles katika Tanganyika vilibadilishwa jina na kuwa Tangayika Rifles (TR). Pamoja na kubadilika jina Tanganyika Rifles ilikuwa na muundo sawa na Kings African Rifles (KAR). Maafisa wenye mamlaka bado walikuwa Waingereza, pamoja na Waafrika watano waliopandishwa cheo wakati wa uhuru na kupokea mafunzo katika vyuo vya kijeshi vya Kiingereza. Jeshi jipya lilipangwa katika vikosi viwili vyenye makao makuu huko Dar es Salaam na Tabora. Afisa mkuu alikuwa Brigedia Jenerali Patrick Sholto Douglas.

Mgomo na uasi wa Tanganyika Rifles

Kwa jumla kulikuwa na hali ya kutoridhika kati ya askari wa TR. Sababu yake ilikuwa matumaini ya kwamba uhuru ungeleta mabadiliko makubwa zaidi na nafasi za kupanda cheo baada ya kuondoka kwa maafisa wazungu. Lakini maafisa Waingereza waliendelea kuajiriwa na serikali ya Nyerere na tofauti kubwa katika mapato na hali ya makazi ya Wazungu na Waafrika ziliendelea. Hata kinyume askari waliowahi kuwa na mshahara wa juu kulingana na watumishi Waafrika wengine ya serikali waliona ya kwamba mapato yao hayakupanda ilhali mishahara kwa jumla iliongezeka zaidi. Zaidi ya hapo, serikali ya TANU ilituma vijana kutoka Umoja wa Vijana wa TANU kwa mafunzo ya kijeshi huko Israeli na baada ya kurudi walipewa ajira jeshini na wengine wao kupandishwa vyeo kupitia askari waliowahi kuhudumia miaka mingi.

Katika Januari 1964 matokeo mawili yalijadiliwa sana kati ya askari moja ilikuwa tangazo la Nyerere alikotamka mwisho wa siasa ya "Africanization" katika utumishi wa serikali[4]. Tangazo hili lilisababisha viongozi wa umoja wa wafanyakazi kulalamika. Tukio lingine likawa habari za mapinduzi ya Zanzibar yaliyoanza tarehe 12 Januari 1964.

Tarehe 20 Januari 1964, bado wakati wa usiku, kikosi cha kwanza cha TR kwenye kambi la Colito Barracks[5] mjini Dar es Salaam kiliasi na kujipatia silaha kutoka ghala. Maafisa Waingereza walikamatwa na kufungwa lakini mkuu Douglas aliweza kujificha. Waasi walivamia kituo cha redio, uwanja wa ndege, ikulu na ofisi ya posta na simu. Maafisa Waingereza na Waafrika wasioshiriki na waasi walisafirishwa Kenya. Rais Nyerere alipelekwa na walinzi wake kwa siri Kigamboni katika jitihada ya siri iliyojulikana baadaye kwa jina la operesheni Magogoni. Alifichwa mwanzoni katika nyumba ya raia binafsi, baadaye katika Kanisa Katoliki. Akamwachia waziri Oskar Kambona[6] kazi ya kuwasiliana na wanajeshi. Madai ya wanajeshi yalikuwa kuachishwa kwa maafisa Waingereza na kupandishwa kwa mishahara. Siku za kwanza ya mgomo wa jeshi ilifuatwa na vipindi vya fujo mjini vilivyobadilika na vipindi vya kimya, mashambulizi dhidi ya maduka ya Wahindi na kukamatwa kwa Wazungu wachache. Hata balozi wa Uingereza alikamatwa kwa kipindi kifupi.

Waziri Kambona alianza kujadiliana na wanajeshi na kuwaahidi ongezeko la mapato na kutoa vyeo vya juu kwa Waafrika kadhaa. Nyerere alirekodi hotuba iliyotangazwa redioni alipokosoa wanajeshi na kudai utulivu. Askari walirudi kwenye kambi lakini wakarudi mjini siku iliyofuata. Pia huko Nairobi na Kampala ulitokea uasi wa wanajeshi - wote askari wa KAR wa awali. Marais Milton Obote na Jomo Kenyatta hawakusita kuomba vikosi vya jeshi la Uingereza vilivyokuwa bado na vituo kwa kuzima ghasia. Hatimaye Nyerere alianza mawasiliano na Uingereza iliyotuma manowari na wanajeshi kutoka Aden kuelekea Dar es Salaam.[7] Polisi ya siri ya Tanzania ilianza kupata habari ya kwamba pia kati ya askari ya Field Force unit majadiliano yalikuwa yameanza kuunga mkono na juhudi za wanajeshi, pia harakati kati ya wafanyakazi bandarini na hofu ilikuwa ya kwamba sehemu ya viongozi wa umoja wa wafanyakazi walikuwa na mipango ya kujiunga nao.

Tarehe 24 Januari serikali ya Tanzania iliomba rasmi Uingereza kuingia kati na kuzimisha uasi. Asubuhi ya 25 Januari kikosi kidogo cha wanajeshi wa Kiingereza waliondoka kwa njia ya helikopta kwenye meli iliyokaa baharini karibu na Dar es Salaam wakavamia kambi la Colito Barracks. Jenerali Douglas alihutubia askari kwa kipazia sauti akadai wanajeshi wajisalimishe. Mwanzoni walikataa lakini baada ya mashambulio mafupi ya Wingereza walio wengi walijisalimisha wengine wakakimbia na viongozi walikamatwa. Vilevile askari wa Dodoma na Nachingwea waliowahi kujiunga na uasi walijisalimisha bila upinzani baada ya kufika kwa askari Waingereza wachache.

Wakazi wengine wa Dar es Salaam walikuwa na hofu ya kwamba Uingereza ulikuwa umerudi ili kurudisha ukoloni lakini baada ya kusita masaa machache Nyerere alieleza kwa njia ya redio ya kwamba kuingilia kwa Uingereza ulifuata ombi la serikali yake.

Watu wengi walikamatwa baada ya matukio haya na kufanyiwa utafiti kama walikuwa na uhusiano na uasi.[8]

Askari Waingereza waliondoka kwenye Aprili 1964 na nafasi yao ilichukuliwa na kikosi kutoka Nigeria iliyofika kwa niaba ya Umoja wa Afrika kufuatana na ombi la serikali ya Tanganyika. [9]

Kuanzisha jeshi jipya la wananchi

Baada ya uasi, jeshi la TR lilivunjwa. Askari wote waliachishwa kazi. Sehemu ya askari wa Dodoma waliajiriwa tena katika jeshi jipya lakini hao wa Dar es Salaam hawakurudishwa. Maafisa Waafrika ambao kwa jumla walisimama upande wa serikali na kutoshiriki katika uasi waliajiriwa tena.

Jeshi la kisiasa chini ya TANU/CCM

Jeshi jipya lilijengwa kwa kuajiri hasa wanachama wa umoja wa vijana wa TANU likapewa jina la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ("Tanzania People’s Defence Force" - TPDF).[10] Jeshi hili jipya liliwekwa chini ya usimamizi ya chama cha TANU (baadaye CCM) kwa kufuata mtindo wa nchi kama Urusi na China. Kamanda wa kwanza alikuwa Mrisho Sarakikya aliyewahi kusimama upande wa serikali wakati wa uasi akapandishwa cheo kutoka luteni hadi kanali, baadaye kuwa jenerali. Nyerere alitaka jeshi lenye tabia ya kisiasa. Kila askari alitazamiwa kuwa kada wa TANU, na TPDF ilihesabiwa ndani ya "Mkoa wa Majeshi" wa TANU pamoja na polisi na magereza. Mkoa wa Majeshi ulihesabiwa sawa na mikoa mingine ya kijiografia na kiutawala wa nchi.

 
Askari wa JWTZ wakivaa kofia za UM

JWTZ katika mfumo wa vyama vingi

Mwaka 1991 Tume ya Nyalali ilipendekeza kubadilisha utaratibu wa kisiasa wa Tanzania na kuhamia mfumo wa vyama vingi; mwaka 1992 pendekezo hilo lilipokewa, hivyo katiba ya nchi ilibadilishwa ipasavyo. Ibara 147 ya katiba inakataza wanajeshi wote kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa. [11]

Kupanuliwa kwa JWTZ

Mwanzoni JWTZ ilikuwa jeshi dogo lenye askari wachache kuliko TR lakini hadi 1967 lilipanuliwa kuwa na vikosi 4. Mnamo 1972 JWTZ lilikadiriwa kuwa na askari 10,000 katika vikosi vinne pamoja na vifaa vya vifaru 20 aina ya Kifaru T-59, 14 Kifaru T-62, mizinga ya Kirusi na Kichina. Vipuli vilikuwa haba na sehemu ya vifaa haikuweza kutengenezwa. [12]

Vita za JWTZ

Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania lilipiga vita mara mbili.

Uganda

Vita kubwa inayojulikana zaidi ilikuwa Vita ya Uganda na Tanzania kwenye miaka ya 1978–1979. Ilianza wakati wa utawala wa dikteta Idi Amin na uvamizi wa jeshi la Uganda katika Mkoa wa Kagera wa Tanzania tarehe 25 Oktoba 1978. Katika muda wa wiki chache Tanzania ilipanua idadi ya jeshi hadi kufikia 100,000 kwa kuingiza askari polisi, wa huduma ya magereza, kutoka Jeshi la Kujenga Taifa na wanamgambo, likisaidiwa na vikundi vya wapinzani wa Idi Amin. Katika Novemba jeshi la Tanzania lilianza kushambulia Wauganda. Hadi mwanzo wa Disemba 1978 Mkoa wa Kagera ulikuwa tena mkononi mwa Tanzania. Tarehe 21 Januari 1979 askari wa Tanzania walivuka mpaka wa Uganda, na tarehe 11 Aprili 1979 walivamia Kampala. Idi Amin alikimbia Libya na JWTZ ilibaki Uganda kwa muda hadi serikali mpya ya Uganda iliimarika.

Msumbiji

Vita isiyojulikana sana wakati wake ilikuwa kuingilia kwa JWTZ katika nchi jirani ya Msumbiji kwa shabaha ya kusaidia serikali ya chama cha Frelimo. Kulikuwa na vipindi viwili vya usaidizi huu.

Kipindi cha kwanza kilikuwa 1977-78 wakati jeshi la Rhodesia iliingia ndani ya Msumbiji. Rhodesia (leo:Zimbabwe) ilitawaliwa wakati ule na serikali ya walowezi Wazungu chini ya Ian Smith. Warhodesia walijaribu kuangamiza vikundi vya wapinzani kutoka kwao waliotafuta kupindua serikali ya walowezi wakijificha katika Msumbiji na kushambulia kutoka huku. Hapo vikosi vya Rhodesia viliingia mara kadhaa ndani ya Msumbiji halafu Rhodesia ilianzisha harakati ya Renamo kwa kukusanya wapinzani dhidi ya Frelimo na kuwapa silaha. Baada ya kuenea kwa vita ndani ya Rhodesia jeshi lake lilishambulia kambi kubwa ya wapinzani chini ya Robert Mugabe katika Mkoa wa Manica wa Msumbiji. Hapo Tanzania ilituma wanajeshi wake kwa shabaha ya kuimarisha utawala wa Frelimo wakarudi kwao mwaka ufuatao 1978.[13]

Baada ya Mapatano ya Lancaster House ya mwaka 1979 vita ya Rhodesia - Zimbabwe ilikwisha. Sasa ilikuwa serikali ya apartheid ya Afrika Kusini iliyochukua nafasi ya mdhamini wa Renamo. Miaka iliyofuata iliona vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Msumbiji kati ya Frelimo iliyosaidiwa na Urusi ikifaulu kutetea miji na Renamo iliyosaidiwa na Afrika Kusini ikifaulu kutawala sehemu kubwa ya mashambani na vijiji vingi. Mwaka 1982 maraisi Machel wa Msumbiji na Nyerere walipatana kutumwa kwa kikosi kidogo cha askari 200 wa JWTZ kwa kazi ya washauri kwenda Msumbiji.[14] Mwaka 1987 Tanzania iliamua tena kutuma askari wengi wa JWTZ hasa kwa kusudi la kutetea Mkoa wa Zambezia dhidi ya Renamo. Waliondoka tena mwaka 1988.[15]

Mpangilio wa JWTZ wa kisasa

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limegagiwa kwa matawi matatu:

  • Kamandi ya Nchi Kavu
  • Kamandi ya Jeshi la Majini
  • Kamandi ya Jeshi la Anga.

Nchi Kavu

Mnamo mwaka 2012 Jeshi la Nchi Kavu la JWTZ lina vikosi vifuatavyo:

  • 5 × brigedi za askari wa miguu
  • 1 × brigedi ya vifaru
  • 3 × batalioni ya mizinga
  • 2 × batalioni za mizinga ya ulinzi wa hewani
  • 1 × batalioni ya mizinga ya mortar
  • 2 × batalioni za kupambana na vifaru
  • 1x rejimenti ya uhandisi
  • 1 × kundi la logistic na akiba

Vyeo katika JWTZ

Amiri jeshi mkuu wa JWTZ ni rais wa Tanzania.

Maafisa

(Cheo cha Kitanzania - (Cheo cha Kiingereza)

Vyeo vya chini

           
Afisa Mteule Daraja la Kwanza
(Warrant Officer Class 1)
Afisa Mteule Daraja la Pili
(Warrant Officer Class 2)
Sajinitaji
(Staff Sergeant)
Sajini
Sergeant)
Koplo
(Corporal)
Koplo Usu
(Lance Corporal)

Maofisa wenye kamisheni

(Cheo cha Kitanzania - (Cheo cha Kiingereza)

                     

Jenerali
(General)

Luteni Jenerali
(Lieutenant General)

Meja Jenerali
(Major General)

Brigedia Jenerali
(Brigadier General)

Kanali
(Colonel)

Luteni Kanali
(Lieutenant Colonel)

Meja
(Major)

Kapteni
(Captain)

Luteni
(Lieutenant)

Luteni usu
(Second lieutenant)
Ofisa Mteule
Officer candidate)

Wajibu wa JWTZ

Wajibu wa JWTZ ni rasmi[16]:

  • Kulinda Katiba na Uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  • Ulinzi wa mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  • Kufanya mafunzo na mazoezi ili kujiweka tayari kivita wakati wote.
  • Kufundisha umma shughuli za ulinzi wa Taifa.
  • Kushirikiana na mamlaka za kiraia katika kutoa misaada ya kibinadamu na uokoaji wakati wa maafa
  • Kutoa huduma mbalimbali za kijamii.
  • Kukuza elimu ya kujitegemea na uzalishaji mali kupitia Jeshi la Kujenga Taifa.
  • Kushiriki ulinzi wa amani kimataifa.

Tanbihi

  1. "Linganisha "Historia ya JWTZ" kwenye tovuti rasmi (yenye makosa madogo, kama kuchanganya Vita Kuu ya kwanza na ya pili)". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2015-06-26. Iliwekwa mnamo 2015-06-17.
  2. Richard F. Burton: Zanzibar; City, Island, and Coast, vol I, London 1872, uk. 266., online hapa
  3. Robert Nunez Lyne, Zanzibar in Contemporary Times, 1905 Hurst And Blackett, London, uk. 100, online hapa
  4. Nyerere alitangaza ya kwamba wananchi wote wangetumiwa kulingana na elimu na uwezo wao kama ni Waafrika wazalendo au Wazungu au Wahindi waliochagua uraia wa Tanganyika, bila kujali rangi ya ngozi. Linganisha Race, Nation, and Citizenship in Post-Colonial Africa: The Case of Tanzania, by Ronald Aminzade, uk. 86 (google books, tazamiwa Juni 2015
  5. Jina la "Colito" lilitunza kumbukumbu ya ushindi wa kikosi kutoka Tanganyika juu ya Waitalia katika mapigano ya Alaba Kulito pale Ethiopia tarehe 19 Mei 1941. (tazama pia Taarifa juu ya mapigano ya Kulito/Colito Archived 6 Julai 2018 at the Wayback Machine.)
  6. Kambona alishika ofisi mbili za mambo ya nje na ulinzi wa taifa
  7. Tanganyika Mutini stirs British action; Pittsburgh Post-Gazette - 21. Jan. 1964
  8. [ https://books.google.com/books?id=b-wWAwAAQBAJ&pg=PA68&lpg=PA68&dq=tanganyika+mutiny&source=bl&ots=Z1izRjQYtE&sig=TdFOGyNb_gPUg4nfNQgBDxmEFqg&hl=de&sa=X&ei=f62BVYuNCcWesgG_obqYBg&ved=0CBwQ6AEwADgU#v=onepage&q=tanganyika%20mutiny&f=false The Military Intervenes: Case Studies in Political Development ed. Henry Bienen, uk. 68, footnote 43 (google book search, ilitazamiwa Juni 2015)]
  9. Life in Tanganyika in the Fifties , by Godfrey Mwakikagile; uk. 83 (google books, ilitazamiwa Juni 2015)
  10. Nestor Luanda, A changing conception of defence:A historical perspective of the military in Tanzania; mlango wa 11 katika Martin Rupiya, Evolutions and revolutions: a contemporary history of militaries in Southern Africa Institute for Security Studies, Pretoria 2005, online hapa
  11. Article 147 (3): "It is hereby prohibited for any member of the defence and security forces to join any political party, save only that he shall have the right to vote which right is specified under Article 5 of this Constitution", Constitution of the United Republic of Tanzania 1977, as amended to 2005, iliangaliwa Mei 2020
  12. International Institute for Strategic Studies, 1972-73, p. 40
  13. Mozambique to return bodies of Tanzanian soldiers, tovuti ya UPI News 22 Februari 1987, iliangaliwa Januari 2017
  14. TANZANIAN MILITARY ADVISERS WILL BE SENT TO MOZAMBIQUE By ALAN COWELL, New York Times, 23 Februari 1982
  15. Tanzanian troops aiding Mozambican army, Pana Press 14 Agosti 2004, iliangaliwa Januari 2017
  16. Tovuti la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania

Marejeo

Historia ya JUWTz

Vyanzo kuhusu uasi wa 1964

Viungo vya nje

  Makala hii kuhusu maeneo ya Tanzania bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.