Tanganyika Rifles
Tanganyika Rifles ilikuwa jina la jeshi la Tanganyika kuanzia uhuru wa nchi mwaka 1961 hadi uasi wake na mwisho mwaka 1964. Iliendeleza mfumo wa King's African Rifles wa awali. Nafasi yake baada ya 1964 ilichukuliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
Historia
haririTanzania bara ilipata uhuru wake kutoka ukoloni wa Kiingereza mwaka 1961 kwa jina la Tanganyika. Zanzibar bado ilikuwa nchi ya pekee.
Hadi mwaka ule kulikuwa na jeshi la kikoloni katika Afrika ya Mashariki lililokuwa la askari Waafrika waliosimamiwa na maafisa Waingereza na jeshi hilo liliitwa King's African Rifles (KAR). Vikosi viwili vya jeshi hili ambavyo askari hao waliwahi kuajiriwa katika eneo la Tanganyika vilitengwa na KAR na kukabidhiwa kwa taifa jipya. Kikosi cha Dar es Salaam kiliitwa sasa "1st Tanganyika Rifles" na kikosi cha Tabora kilikuwa "2nd Tanganyika Rifles".
Maafisa Waingereza wa vikosi hivyo waliajiriwa pia na serikali ya Tanganyika. Afisa mkuu alikuwa Brigedia Jenerali Patrick Sholto Douglas.
Uasi wa 1964
haririKatika miaka ya kwanza baada ya uhuru Waafrika wachache walipelekwa masomoni kwenye vyuo vya kijeshi huko Uingereza na kupandishwa cheo kuwa maafisa. Waziri wa mambo ya nje Oscar Kambona alituma vijana wa TANU kwenda Israel kwa masomo ya kijeshi.
Kati ya askari Waafrika wa siku nyingi uchungu ulianza kuenea kwa sababu walikuwa na tumaini uhuru utaleta nafasi za kupandishwa cheo, lakini waliendelea kusimamiwa na maafisa Wazungu. Pia waliona mishahara yao ilibaki kama awali ilhali Waafrika katika huduma ya serikali nje ya jeshi walipandishwa vyeo na mishahara.[1]
Usiku wa tarehe 19 Januari 1964 kundi la askari Waafrika walijipatia silaha wakakamata maafisa wote Wazungu na Waafrika na kusambaa mjini wakitangaza madai yao. Tarehe 20 Januari kikosi cha pili katika Tabora kiliwafuata. Maafisa Waingereza walipelekwa Kiwanja cha Ndege na kutumwa Kenya. Mawaziri wa serikali pamoja na rais Julius Nyerere walijificha, isipokuwa waziri Kambona alipatikana kujadiliana na waasi.
Baada ya Kambona kutia sahihi na kukubali madai ya waasi, Nyerere aliamua kuomba msaada wa Uingereza. Kikosi cha askari Waingereza kilifika kwa meli kutoka Aden na kumaliza uasi katika saa chache. Kikosi cha pili huko Tabora baada ya kusikia habari hizi walitangaza ya kwamba waliacha uasi wakakabidhi silaha kwa kikundi kidogo cha Waingereza.
Uasi huo wa askari Waafrika ulifuatwa na wenzao huko Uganda na Kenya. Tarehe 22 Januari askari wa Uganda Rifles katika kambi la Jinja walikatama maafisa wao na tarehe 24 Januari kikosi kimoja cha Kenya Rifles huko kambi ya Lanet (Nairobi) walijipatia silaha na kupeleka madai kwa serikali. Serikali za Jomo Kenyatta (Kenya) na Milton Obote (Uganda) zilipaswa kufuata mfano wa Nyerere na kuomba msaada wa jeshi la Uingereza kukandamiza uasi.
Mwisho wa Tanganyika Rifles
haririHapo serikali ya Tanzania iliamua kuachisha askari wote na kumaliza Tanganyika Rifles kabisa. Jeshi jipya likaundwa katika Septemba 1964. Maafisa Waafrika waliweza kurudi na pia askari wengi wa Tabora waliajiriwa upya.
Lakini jeshi jipya liliundwa kama taasisi chini ya usimamizi raia, yaani chini ya amri ya wanasiasa na jeshi hili linajulikana kama Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
Marejeo
hariri- ↑ Linganisha madai ya askari wakati wa uasi jinsi kiongozi wao Iloga alimwambia waziri Kambona, ling T. Parsons uk 111
Viungo vya nje
haririKujisomea
hariri- Timothy Parsons The 1964 Army Mutinies and the Making of Modern East Africa (inapatikana kupitia google books).
- Tanzania People's Defence Force Tanganyika rifles mutiny: January 1964 Dar es Salaam University Press, 1993, ISBN 9976601875, 9789976601879 (177 pages)
- Tony Laurence The Dar Mutiny of 1964 2nd ed. AuthorHouse, 2010, ISBN 9781449098759 (249 pages)
- Christopher Gallop Letters from East Africa Grosvenor House, 2013, ISBN 9781781486283 (242 pages)
Vyanzo hasa kuhusu uasi wa 1964
hariri- Tanganyika Embarrassed By Need for British Assistance; Calls For Pan-African Force To Aid In Future Crises, by John D. Gerhart; The Harvard Crimson, March 10, 1964
- British Troops quell Mutiny in Tanganyika; The Chicago Tribune 26 Januari 1964 Archived 29 Aprili 2017 at the Wayback Machine.
- Timothy Parsons, The 1964 Army Mutinies and the Making of Modern East Africa, Greenwood Publishing Group, 2003, iliangaliwa Juni 2015
- Tony Laurence, The Dar Mutiny of 1964, AuthorHouse, 2010, iliangaliwa Juni 2015