Open main menu

Kalenda ya Juliasi ni kalenda iliyoanzishwa kwa amri ya Julius Caesar mnamo mwaka 46 KK katika Dola la Roma. Ilichukua nafasi ya kalenda ya Kirumi iliyotangulia. Kalenda ya Juliasi ilibadilishwa na kalenda ya Gregori kuanzia karne ya 16 BK lakini ilikuwa kalenda rasmi katika nchi mbalimbali kama Urusi hadi karne ya 20. Mpaka leo ni kalenda ya liturgia katika kanisa la Kiorthodoksi.

Matengenezo ya mwaka 46 KKEdit

Kaisari Juliusi alikuwa mtawala wa Kirumi aliyeamua kubadilisha kalenda ya kale iliyokuwa kalenda ya mbalamwezi. Majira yalikosa tarehe kamili katika kalenda hiyo hali iliyosababisha matatizo ya kiutawala.

Hivyo Caesar alimwajiri mtaalamu Mmisri Sosigenes atunge kalenda mpya inayofuata mzunguko wa jua. Kalenda hii iliitwa kwa heshima yake Kalenda ya Juliasi. Ilikuwa na miezi 12 yenye siku 30 au 31 na kipindi kimoja kifupi chenye siku 28 ambacho ni mwezi wa Februari ili kukamilisha siku 365 za mzunguko wa jua. Vipindi hivi viliendela kuitwa "mwezi/miezi" ingawa havikufuata tena mwendo wa mwezi mwenyewe. Kwa sababu muda wa mwaka wa jua ilijulikana kuwa na siku 365 1/4 kila mwaka wa nne siku ya nyongeza iliingizwa kama siku ya 29 ya mwezi wa Februari.

Mwaka 46 KK mwenyewe ilirefushwa kwa ajili ya sahihisho lile likawa na siku 445 ikiwa Warumi waliikumbuka kama "mwaka uliochanganyikiwa".

Majina na hesabu ya mieziEdit

Sosigenes alitumia majina ya miezi ya kalenda ya kale yanayoendela kutumikwa hadi leo. Isipokuwa mwaka 44 KK baada ya kifo cha Caesar mwezi wa "Quintilis" ilipewa jina la marehemu ikaitwa "Julius" ndiyo Julai kwa Kiswahili. Mtwala mkubwa aliyefuata baada ya Julius Caesar alikuwa Augusto (anayehesabiwa kuwa Kaisari wa kwanza wa Kirumi) na mwezi wa Sextilis ulipewa jina lake kwa heshima yake ni mwezi wa Agosti kwa Kiswahili. Hata watawala wengine walijaribu kupachika majina yao kwenye mwezi fulani lakini ni majina ya Kaisari Juliusi na Augusto pekee yaliyodumu.

Miezi ya Septemba hadi Desemba inatunza kumbukumbu ya kwamba ilikuwa miezi ya saba hadi kumi katika kalenda ya kale ya kirumi.

Jina la mwezi - Neno la nambari la Kilatini

Septemba - septem (7)

Oktoba - octo (8)

Novemba - novem (9)

Desemba - decem (10)

Lakini hapakuwa na mapatano kuhusu mwanzo wa mwaka ni mwezi gani. Maeneo mbalimbali yalitumia mwanzo tofauti. Ni tangu karne ya 13 BK tu ya kwamba 1 Januari ilianza polepole kukubaliwa kuwa mwanzo wa mwaka katika nchi za Ulaya.

Kasoro za Kalenda ya JuliasiEdit

Kalenda ya Juliasi ilikuwa na kasoro ambayo haikujulikana mwanzoni. Muda wa mwaka wa jua si siku 365 1/4 kamili. Hivyo mwaka wa kalenda ya Juliasi ulipita muda kamili ya mwaka wa jua kwa dakika 11 na sekunde 14.

Hadi karne ya 14 BK tofauti hii ilikuwa imefikia tayari jumla ya siku 7. Haya yalionekana hasa wakati wa Pasaka ambayo haikufuata tena utaratibu uliowekwa na Mtaguso wa kwanza wa Nisea.

Kwa sababu hiyo Mtaguso wa Trento wa Kanisa Katoliki uliamua kusahihisha kalenda. Ni Papa Gregori XIII aliyeita wataalamu waliofanya makadirio mapya.

Tangu mwaka 1582 kalenda ya Gregori ilipoanzishwa ikawa leo kalenda ya kimataifa.