Julius Caesar

Jenerali wa Kirumi, kiongozi wa serikali na Dikteta wa mwisho

Gaius Julius Caesar (tamka gayus yulius kaesar[1] - 100 - 44 KK) alikuwa kiongozi wa kisiasa na wa kijeshi wa Roma ya Kale.

C. Iulii Caesaris quae extant, 1678

Anakumbukwa hasa kwa mafanikio mbalimbali yanayoonekana kuathiri dunia hadi leo.

Baadhi ya mafanikio hayo ni:

  • Waroma wa Kale walimheshimu kushinda viongozi wote waliomfuata au kutangulia akatangazwa kuwa mungu. Jina lake lilipata kuwa neno kwa ajili ya cheo cha watawala wa Kiroma waliomfuata. Kutokana na badiliko hilo la jina "Caesar" kuwa cheo, lugha mbalimbali zilipokea cheo hicho kama vile Kijerumani ("Kaiser"), Kirusi ("Tsar") na Kiswahili ("Kaisari" - kutokana na neno la Kijerumani).

Kupanda ngazi hariri

Alizaliwa katika familia ya makabaila wenye nafasi katika Senatus ilivyoitwa bunge la Roma. Aliingia katika siasa, akachaguliwa kwa vyeo mbalimbali kwa vipindi vya kawaida wa miezi kadhaa hadi mwaka moja.

Cheo chake muhimu cha kwanza kilikuwa mkuu wa koloni la Kiroma la Hispania. Alifaulu kushinda ghasia ya Wahispania wenyeji waliojaribu kuwafukuza Waroma kutoka nchini mwao. Caesar aliporudi Roma alitajirika na kujipatia sifa kama kiongozi wa kijeshi pia mwanasiasa aliyeokoa koloni muhimu la Hispania.

Baadaye Caesar alijiunga na wanasiasa wawili wengine: Gnaeus Pompeius Magnus aliyekuwa mkuu wa wanajeshi na Marcus Licinius Crassus aliyekuwa tajiri kushinda Waroma wote. Wote watatu waliunda umoja ulioitwa "triumviratus", yaani umoja wa wanaume watatu, wakashika mamlaka katika dola. Caesar alichaguliwa kwa cheo kikuu yaani Konsul kwa mwaka 59 KK. Baada ya mwisho wa kipindi chake alijipatia cheo cha Prokonsul au gavana wa eneo la Gallia ya Kiroma (Italia ya Kaskazini na eneo dogo la Ufaransa ya Kusini).

Vita ya Gallia hariri

Alitumia nafasi hii kuanzisha vita dhidi ya makabila ya Gallia huru yaani eneo lote la Ufaransa, Uswisi na Ubelgiji ya leo. Katika miaka minane ya 58 - 51 KK alitwaa Gallia yote. Aliingia pia ndani ya Germania (Ujerumani) na kuvuka bahari aliposhambulia upande wa kusini wa Britannia. Aliandika kitabu cha "De bello gallico" (yaani Vita ya Gallia) akieleza mapigano yake. Kitabu hicho kina habari muhimu za kihistoria juu ya utamaduni wa makabila ya Gallia, Germania na Britannia aliyopigana nayo.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe hariri

Baada ya kufanikiwa Gallia na kujenga jeshi kubwa tena hodari, wanasiasa wengine huko Roma walianza kumwogopa wakajaribu kumzuia asirudi Italia. Mwenzake Crassus alikuwa amekufa tayari vitani mashariki mwa dola; mwenzake Pompeius aliomwogopa Caesar akajaribu kushawishi viongozi wengine kumsimamisha.

Lakini mwaka 49 KK Caesar aliongoza wanajeshi lake warudi Italia. Pompeius na wapinzani wake walitoka Roma wakaenda Ugiriki iliyokuwa jimbo la Kiroma. Mwaka 48 KK Caesar akachaguliwa tena kuwa Konsul. Akamfuata Pompeius kwa jeshi lake akamshinda katika mapigano. Pompeius alikimbia kwenda Misri lakini mfalme Ptolemaio XIII alimwogopa Caesar akamwua Pompeius akampatia Caesar kichwa chake alipofika Misri. Caesar alikutana na dada yake Ptolemaio Kleopatra akampenda na kuzaliana naye mwana wake pekee. Akamsaidia Kleopatra kuwa malkia na mtawala wa Misri.

Kuchaguliwa dikteta hadi kifo hariri

 
Caesar alikuwa binadamu wa kwanza aliyeonyeshwa kwenye sarafu za Roma

Caesar alirudi Roma kutoka Misri akiwa mshindi dhidi ya wapinzani wote. Bunge la Senatus lilimpa cheo na madaraka ya dikteta kwa miaka 10. Baada ya ushindi mwingine dhidi ya wapinzani huko Hispania bunge lilibadilisha azimio hilo kumpa cheo cha dikteta wa maisha. Caesar alipokea azimio hili.

Sasa sehemu ya wabunge waliogopa ya kwamba nia yake ilikuwa kuwa mfalme wa Roma - jambo lililokuwa marufuku katika jamhuri ya Roma. Kikundi cha wabunge -wote makabaila wa familia za kale- kiliunga mikono wakamwua Caesar bungeni tarehe 15 Machi 44 KK kwa kumdunga kisu mara 23. Caesar anasemekana alimtambua mpwa wake Brutus akamwuliza kwa maneno yake ya mwisho: "Hata wewe mwanangu?"

Caesar hakuwa na watoto ila huyu mwana wa Kleopatra asiyekuwa Mroma. Kabla ya kifo chake alikuwa amempanga mtoto mpwa wake Oktaviano. Huyu Oktaviano -aliyejulikana baadaye kama Augusto na mtawala wa kwanza wa Dola la Roma- alilipiza kisasi chake katika kipindi cha vita ya wenyewe kwa wenyewe na kuua wapinzani wote wa Caesar.

Miaka miwili baada ya kifo chake bunge lilimtangaza Caesar kuwa mungu.

Marejeo hariri

  1. Kwa matamshi ya Kilatini sanifu cha Kale herufi "C" ilikuwa na matamshi ya "K"; katika matamshi ya karne za baadaye ilikuwa zaidi "Ch" kwa hiyo "Chesar"; kutoka hapo yametokea matamshi ya Kiingereza "Sizar"