Kisiwa cha Toten
Kisiwa cha Toten ni kisiwa kimojawapo cha Tanzania ambacho kinapatikana katika hori ya Tanga kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi.
Kisiwa kina eneo la takriban hektari 16. Kinasemekana kuwa na umbo la tanga la jahazi na hapo ni asili ya jina la mji wa Tanga.
Historia
haririKulikuwa mahali pa makazi ya Waswahili wa kale katika pwani ya kaskazini ya Tanzania kwenye Bahari ya Hindi.
Kisiwa hiki ni asili ya mji wa Tanga, kwa kuwa mji wenyewe ulikuwepo hapa na maghofu yaliyobaki ni ushuhuda wake.
Tangu pwani ya Mrima, pamoja na Tanga, lilipowekwa chini ya utawala wa sultani Seyyed Said wa Zanzibar, wakazi wapya waliohamia Tanga walianza kujenga nyumba zao barani. Watu wa kisiwani waliwafuata. Mmisionari Ludwig Krapf aliyetembelea Tanga mnamo 1854 alikuta bado watu wengi kisiwani. Burton aliyemfuata miaka michache baadaye aliona wakazi wachache tu. Baumann aliandika mwaka 1891 kwamba wakazi wa mwisho waliondoka mnamo 1885 wakihamia bara sehemu za mji wa leo.[1]
Kuna magofu ya msikiti ya karne ya 17 na makaburi ya karne za 18 na 19. Vipande vya vyungu vimepatikana pia ambavyo vyote ni dalili ya kwamba kisiwa kilikaliwa na watu walioondoka baadaye. [2]
Kabla ya kufika Wazungu kilijulikana kama kisiwa cha Changa. Kumbe jina lililozoeleka sasa linatokana na Kijerumani "Toteninsel" likimaanisha "Kisiwa cha Wafu". Kwasababu Wajerumani walipofika Tanga walisumbuliwa sana na ugonjwa wa malaria, ambao kwa wakati huo haukuwa na tiba, hivyo walitumia kisiwa cha Changa kuwatenga watu wanaougua malaria huku wakifanya utafiti wa tiba ya kufaa ila watu waliofariki wakizikwa kisiwani hapo.
Waingereza walipochukua utawala kutoka kwa Wajerumani walikiita "Toten Island": wakichukua "Toten" kama jina hawakutafsiri maana yake.
Tazama pia
haririMarejeo
hariri- ↑ Oscar Baumann, Usambara und seine Nachbargebiete, Berlin 1891, uk 89-90
- ↑ Tanga Attractions, Toten Island Island in Tanga, "Lonely Planet Tanzania", tovuti iliangaliwa Februari 2018
Viungo vya nje
haririMakala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Tanga bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Kisiwa cha Toten kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno. |