Mark Richard Shuttleworth (* 18 Septemba 1973) ni mjasiriamali kutoka nchini Afrika Kusini aliyekuwa Mwafrika wa kwanza kufika kwenye anga-nje.

Mark Shuttleworth kwenye kituo cha ISS

Familia na elimu

hariri

Alizaliwa mwaka 1973 kwenye Dola Huru la Oranje akiwa mtoto wa daktari na mwalimu. Baada ya kumaliza shule 1991 alisoma biashara kwenye Chuo Kikuu cha Cape Town akapokea digrii ya kwanza mwaka 1996.

Wakati bado alikuwa mwanafunzi alishiriki kwenye ukuzaji wa programu ya Debian, nakala moja ya Linux.

Mwaka 1995 aliunda kampuni ya Thawte Consulting iliyokuza programu za usalama wa intaneti. Mwaka 1999 aliuza kampuni yake kwa dolar milioni 575 kwa kampuni ya Marekani Verisign[1].

Mwekezaji katika programu huria

hariri

Miaka iliyofuata aliwekeza pesa kwenye miradi mbalimbali inayolenga kusaidia wajasiriamali wapya. Mwaka 2001 aliunda Taasisi ya Shuttleworth inayosaidia miradi ya kuboresha jamii ya Afrika Kusini, hasa miradi huria ya intaneti inayojenga elimu[2].

Tangu mwaka 2005 Shuttleworth alijishughulisha na programu dijitali huria akawekeza pesa ya kukuza Ubuntu, nakala ya Debian. Aliunda Taasisi ya Ubuntu inayoendelea kukuza programu hiyo huria[3].

Usafiri wa anga-nje

hariri

Shuttleworth alipata umaarufu wa kimataifa aliporushwa kwenye anga-nje tarehe 25 Aprili 2002. Alilipa dolar milioni 20 akasafiri kama abiria kwenye chombo cha anga-nje cha Kirusi Soyuz TM 34 akafika kwenye Kituo cha Anga cha Kimataifa (ISS) alipokaa siku 7 na kushiriki katika majaribio ya kisayansi. Kutoka kwenye anga-nje aliongea na rais Thabo Mbeki, Nelson Mandela na binti wa Afrika Kusini Michelle Foster aliyekuwa na miaka 14 akipambana na kansa[4]. Michelle alikuwa na ndoto ya kuwa mwanaanga, hivyo akapewa nafasi ya kuongea na Mandela na Shuttleworth kabla hajaaga dunia.

Marejeo

hariri
  1. VeriSign Buys South Africa's Thawte for $575 Million Archived 22 Juni 2011 at the Wayback Machine., tovuti ya internetnews.com ya December 23, 1999
  2. "Tovuti ya Shuttleworth Foundation". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2014-09-16. Iliwekwa mnamo 2019-05-28.
  3. Ubuntu carves niche in Linux landscape, tovuti ya cnet.com ya 21 Juni 2006, kupitia web.archive.org
  4. Nelson Mandela Chats With Shuttleworth, taarifa ya Associated Press ya 2 Mei 2002, kupitia web.archive.org
  Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mark Shuttleworth kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.