Milima ya Lebanoni

Milima ya Lebanoni ni safu ya milima katika nchi ya Lebanoni inayoanza katika Syria. Inaelekea sambamba na pwani ya Mediteranea na milima ya Lebanoni ndogo. Mwelekeo wa safu ni kutoka kaskazini kwenda kusini kwa urefu wa kilomita 240. Kati yake, kilomita 160 ziko ndani ya Lebanoni na kilomita 80 ndani ya Syria.

Mwerezi kwenye milima ya Lebanoni.
Mwerezi kutoka milima ya Lebanoni ni nembo ya kitaifa ya nchi ya Lebanoni.

Upande wa magharibi kuna tambarare nyembamba kando ya pwani ya bahari na upande wa mashariki ni bonde la Beka'a na ng'ambo yake ni safu ya Lebanoni ndogo.

Sehemu ya juu ni mlima Qurnat as Sawda' wenye kimo cha mita 3,088 juu ya UB. Kuanzia mwezi Novemba hadi Aprili milima ya juu hufunikwa na theluji iliyosababisha milima kuitwa "leban" yaani nyeupe.

Zamani palikuwa na misitu minene lakini miti imekatwa tangu nyakati za kale na leo hii ni miti michache iliyobaki. Taarifa nyingi za Biblia zinataja miti ya Lebanoni iliyotumiwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, hekalu la Yerusalemu na pia kwa meli (kwa mfano Kitabu cha kwanza cha Wafalme 5:20 au Ezekieli 27:5). Mti maarufu zaidi wa Lebanoni ni mwerezi.

Milima ilikuwa kimbilio la vikundi vingi vilivyoteswa penginepo, kwa mfano Wakristo Wamaroni, Waislamu Washia na Wadruzi.

Makala hii kuhusu maeneo ya Asia bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Milima ya Lebanoni kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.