Ogu ni jina la mfalme wa Waamori aliyetawala sehemu za Bashani. Ogu anatajwa katika Biblia kwenye vitabu vya Hesabu 21 na Kumbukumbu la Torati 3, kwa kifupi pia katika Zaburi 135:11 na 136:20. Inawezekana ya kwamba kutajwa kwa "Mwamori" katika Amosi 2:9 ni pia kuhusu Ogu.

Milki za wafalme Ogu na Sihoni wa Waamori upande wa mashariki wa mto Yordani wakati wa Biblia

Ogu katika Biblia

hariri

Katika vitabu vya Hesabu na Kumbukumbu la Torati anaonyeshwa kama mfalme ambaye aliyekataa ombi la Wanaisraeli la kupita katika nchi yake wakitokea Misri na kuelekea Kanaani. Ogu alikataa akakusanya jeshi lake na kuwashambulia Wanaisraeli. Karibu na mji wa Ederei (leo: Dar'a nchini Syria) alishindwa. Wanaisraeli waliteka nchi yake ikawa makazi ya kabila la Manase.

Ogu anakumbukwa katika masimulizi ya Biblia kama jitu akiwa na kitanda chenye urefu wa mikono yaani dhiraa 10[1], sawa na mita 4-5.

Katika masimulizi ya Wayahudi sifa hiyo iliendelea kuongezeka; katika Kitabu cha Amosi 2,9 anatajwa (bila kusema jina) kama "Mwamori" "nalimwangamiza Mwamori mbele yao, ambaye urefu wake ulikuwa kama urefu wa mierezi, tena alikuwa na nguvu kama mialoni".

Ogu katika mapokeo ya Kiyahudi

hariri

Wataalamu Wayahudi wa baadaye waliona ya kwamba vipimo vya Kumb. 3 kuhusu kitanda chake chenye urefu wa mikono yaani dhiraa 10, sawa na mita 4-5, vilihusu mkono wa hilo jitu lenyewe, hivyo walimwona mkubwa zaidi tena.

Kwenye kitabu Berakhot cha Talmudi Ogu anasimuliwa ya kwamba aliweza kuinua mlima aliotaka kurusha dhidi ya Wanaisraeli, lakini Mungu alimzuia[2]. Katika kitabu cha Nidah katika Talmudi Ogu anasemekana ni mtu aliyeishi kabla ya gharika kuu ya Nuhu akiwa ni mmoja wa wale ambao walitunzwa.[3]

Ogu nje ya Biblia

hariri

Kwa jumla habari haba zilizohifadhiwa juu ya Ogu ziko ndani ya Biblia. Nje yake jina la Ogu linaonekana kwenye kigae cha mwandiko wa kikabari kutoka mji wa Biblos[4].

Ogu katika Uislamu

hariri

Masimulizi ya Kiyahudi yalipokewa na Waislamu na kubadilishwa tena. Hapa anajulikana kwa Kiarabu kama ‘Uj bin Unuq / ‘Anaq عوج بن عنق. Ushahidi uko kwa Al Tabari aliyeandika ya kwamba maiti ya Udj ilikuwa kama daraja juu ya mto Naili, pia wengine.[5]

Kutoka mapokeo hayo ya Kiislamu jina lilifika pia katika hekaya za Waswahili kwa umbo la Unju bin Unuq.

Marejeo

hariri
  1. "mikono kenda", Kumb. 2:11-12
  2. Berakhot 54b, Babylonian Talmud: Tractate Berakoth
  3. Talmud - Mas. Nidah 61a,English Babylonian Talmud, SEDER TOHOROTH, tractate Nida
  4. Wolfgang Roellig in "Eine neue phoenizische Inschrift aus Byblos," (Neue Ephemeris für Semitische Epigraphik, vol 2, 1-15 and plate 1)
  5. Angalia makala UDJ katika Encyclopedia of Islam, uk. 777

Tazama pia

hariri

Kujisomea

hariri
  • Admiel Kosman: The Story of a Giant Story. The Winding Way of Og King of Bashan in the Jewish Aggadic Tradition. In: HUCA 73 (2002), S. 157–190.

Viungo vya nje

hariri